Akhlaqi Katika Uislamu (25)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 25 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitatupia jicho baadhi ya nukta kuhusu mtazamo wa Uislamu juu ya Akhlaqi katika Familia. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Bila shapa mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa, katika vipindi kadhaa vilivyopita tumezungumzia sifa za akhlaqi za kijamii. Katika sehemu hii ya 25 ya kipindi hiki, na kama tulivyotangulia kueleza, tutadondoa machache kuhusu "Akhlaqi katika Familia". Kimsingi, na ndivyo ulivyo mtazamo wa wataalamu, ilipasa tutangulie kuizungumzia maudhui hii kabla ya ile ya akhlaqi za kijamii, kwa sababu muundo wa kijamii wa mfumo wowote ule unategemea sana taasisi muhimu ya familia.
Hakuna shaka kuwa, familia ndio msingi mkuu zinaosimamia juu yake nguzo za akhlaqi za kijamii. Na ni kwa sababu hiyo, ndio maana katika utamaduni wa Uislamu wa asili uliofunzwa na Bwana Mtume Muhammad SAW, familia ina hadhi na nafasi makhususi na yenye umuhimu wa kipekee. Lakini nukta ya kuzingatiwa zaidi katika muktadha wa mazungumzo yetu ni kwamba, lengo na msukumo wa kufunga ndoa na kuanzisha familia inapasa utokane na usuli na msingi wa kiakili na kimantiki.
Kuna baadhi ya watu huchagua mke au mume kwa sababu na kwa matashi ya kighariza tu; yaani kwa kupendezwa na kuvutiwa na sura na dhahiri ya mtu, pasi na kuzingatia hata chembe uzuri wa batini wa mtu. Kuna kundi jengine la watu ambao wanakutazama kuoa na kuolewa na kuanzisha familia kwa jicho la maslahi ya kiuchumi, pato na utajiri wa mtu. Wapo pia watu ambao wanachagua wenza wao katika ndoa kwa sababu ya kunufaika kimadaraka na kisiasa katika chaguo wanalofanya; na vilevile kuna baadhi ya watu wanaoshawishika kufunga ndoa na kuanzisha familia kwa sababu ya moto mkali wa jazba na mhemko wa mapenzi ambao huzimika baada ya muda mfupi tu wa maisha ya ndoa. Kila moja kati ya sababu zote hizi tulizotaja huwa mithili ya jengo lililosimamishwa juu ya msingi unaolegalega, ambao upatwapo na mtetemeko au mtikisiko mdogo tu humong'onyoka na kudidimia. Kusema kweli moja ya sababu muhimu zaidi inayochangia ongezeko la kila uchao la talaka, kuvunjika ndoa na kusambaratika familia ni huko kulegalega kwa msingi wa kichocheo hicho cha kufungia ndoa, kinachotokana na vivutio vya dhahiri ya mtu, jazba na mhemko tu wa mapenzi au maslahi ya kiuchumi na kisiasa.
Ikiwa ndoa na familia ni kitu chenye hadhi ya juu na nafasi maalumu katika Uislamu, ni kwa sababu ya familia hiyo kuanzishwa kwa kuzingatia misingi imara ya pamoja ya kiimani na kiitikadi waliyonayo watu wanaofunga ndoa. Qur'ani tukufu inaitaja misingi hiyo ya pamoja kama inavyoeleza aya ya 35 ya Suratul-Ahzab ya kwamba: "Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa."
Aya hii inabainisha kwa uwazi kabisa misingi ya pamoja ya kiitikadi, kiakhlaqi, kitabia na kimatendo ambayo inapasa kuzingatiwa na kutiliwa maanani katika masuala yote, hasa wakati wa kuanzisha familia, inayotarajiwa kuwa chombo madhubuti na cha kudumu. Nukta hizi za pamoja ndizo zinazojenga hali chanya na mazingira mwafaka katika taasisi ya ndoa ya kuwawezesha mke na mume walio na hisia na fikra zinazoafikiana kupiga hatua kwa pamoja katika kukwea na kufikia vilele vya mafahamiano na ukamilifu wa kimaada na kimaanawi. Si hayo tu, lakini pia kupitisha maisha yao katika anga iliyojaa manukato ya imani na utulivu wa kinafsi, kiakili na kiakhlaqi na kuepukana na matatizo ya tafrani za kifikra na msongo wa mawazo yanayozitaabisha na kuziyumbisha ndoa nyingi katika dunia yetu hii ya leo.
Nukta yenye umuhimu mkubwa na wa aina yake iliyoashiriwa katika aya tuliyosoma ya Suratul Ahzab ni kwamba, Waislamu wanaume na Waislamu wanawake walio waumini huwa wanamdhukuru na kumkumbuka sana Mwenyezi Mungu; nukta inayotufikisha kwenye hitimisho kwamba, imani juu ya Allah ni msingi mkuu unaopasa kuzingatiwa kila mara na kwa uzito mkubwa wakati wa shida na raha na katika utulivu na misukosuko ya maisha ya ndoa.
Qur'ani tukufu inatubainishia matokeo na matunda yanayopatikana kwa kushikamana na njia hiyo, kama inavyoeleza aya ya 97 ya Suratu-Nahl ya kwamba: "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini,tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda."
Kwa hivyo, kama taasisi ya ndoa na familia itanyunyiziwa marashi na manukato ya dini; na nuru ya imani safi na matendo mema ikatanda kwenye anga ya maisha ya mke na mume, hapana shaka familia hiyo itanyeshewa na mvua ya rehma na kumiminikiwa na kheri na baraka za Mola. Lakini mbali na hayo, ndani ya taasisi kama hiyo iliyojawa na uchangamfu, furaha na upendo, si rahisi kushuhudiwa ndani yake harufu chafu ya khulka mbaya katika kauli na matendo ya watu; bali kinyume chake, uturi wa huba, huruma na masikilizano ndio unaotanda na kuzagaa ndani yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatubainishia taswira ya kupendeza ya taasisi ya ndoa, kama isemavyo aya ya 21 ya Suratu-Rum ya kwamba: “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.”
Kwa hivyo lengo la ndoa katika Uislamu ni kuasisi taasisi ambayo ndani yake yatajengwa mazingira ya kupatikana watu walio na fikra moja kimaelewano na wenye muelekeo mmoja katika kuzijenga nafsi zao kimaada na kimaanawi; na wakati huohuo kulelewa na kukuzwa ndani yake kizazi kitakachopambika kwa sifa aali za kiakhlaqi na kiutu. Ni kizazi kitakachoandaliwa kwa lengo maalumu la kuandaa wasomi na watu waliotukuka kimaanawi na kuwa kigezo na mfano wa kuigwa na vizazi vya baada yao.
Ni kinyume na ilivyo katika zama zetu hizi, ambapo kutokana na kusambaratika taasisi ya familia kunakosababishwa na ndoa za kiholela zinazochochewa na utamanifu na mapenzi ya kijazba na kimihemko; huruma, huba na mapenzi ya kweli huwa hayashuhudiwi baina ya mke na mume, huku watoto pia wanaolelewa na kukulia katika familia hizo zinazolegalega kimaadili, huwa ni wa kizazi kisicho na utambulisho, kinachotangatanga na kushughulishwa zaidi na pumbao na upuuzi. Ni cha watu wanaoiga na kufuata kila wanachosikia na kuona na wenye irada dhaifu kiasi cha kushindwa kuwa na uwezo hata wa kuchagua aina sahihi ya kivazi, mtindo ufaao wa maisha na muonekano unaopendeza wa sura zao. Kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba sehemu ya 25 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 26 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/