Nov 10, 2022 17:22 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (41)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 41 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia nukta nyingine za kiuchumi za Akhlaqi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia maudhui moja kuu na ya msingi; nayo ni ya kwamba, kwa mtazamo wa Uislamu, suhula za vitu na za kiuchumi inapasa zitumike kama nyenzo za kuyafikia malengo ya kidini na kiutu; na kwamba suhula hizo inatakiwa ziwe mithili ya daraja la kumvusha na kumfikisha mtu kwenye upeo wa juu kabisa wa ukamilifu katika ulimwengu wa baada ya kifo. Ni kutokana na mtindo huu wa maisha ndipo msingi wa uadilifu wa kiuchumi unapojitokeza na kudhihiri katika jamii. Na huo ni msingi muhimu unaoufanya mfumo wa kiuchumi wa jamii ya wanadamu uwe na hali ya kadiri na mlingano na kuepusha kutokea aina yoyote ile ya mwenendo wa kufurutu mpaka.

Bila shaka uadilifu ni msingi ambao hauhusiani na masuala ya kiuchumi pekee, bali inatakiwa uthibiti katika masuala yote ya kijamii, kiutamaduni, kisheria na kisiasa. Ili kutubanishia wigo mpana na jumuishi wa uadilifu, Mwenyezi Mungu Mola Muadilifu na apendaye uadilifu, ameutaja uadilifu kuwa ndio falsafa ya harakati iliyoendeshwa na Mitume wake wateule, kama inavyoeleza sehemu ya mwanzo ya aya ya 25 ya Suratul-Hadid ya kwamba: "Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu..."Bwana Mtume SAW, naye pia ameeleza kwamba amekuja kuendeleza harakati za Mitume waliomtangulia za kueneza uadilifu, aliposema: "Mola wangu ameniamuru nisimamishe haki na uadilifu".

Pamoja na hayo, tajriba ya historia imeonyesha kuwa, ili mabepari madhalimu wanaonyonya damu za wanyonge na walalahoi waendelee kuishi maisha yao ya kiashrafu na kifahari, tokea huko nyuma na hadi sasa, wanapiga vita harakati zozote za kutetea uadilifu. Pengine ni kwa sababu hiyo, ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akaeleza yafuatayo katika sehemu ya mwisho ya aya tuliyosoma ya 25 ya Suratul-Hadid: "na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda".

Sehemu hii ya aya ya 25 ya Suratul-Hadid inatupa ujumbe na somo kwamba haitawezekana kusimamisha haki na uadilifu pasi na kutumia nguvu kukabiliana na upinzani wa waliotajirika na kuishi katika raha na uneemevu, kwa gharama ya kupora na kunyonya mali na rasilimali za umma na za wanyonge katika jamii.

Mapambano na makabiliano ya mtawalia yaliyotokea baina ya mabwanyenye wa Makka na Bwana Mtume SAW ambaye alikuwa akitaka kusimamisha mfumo wa haki na uadilifu, ni moja ya mifano hai inayoonyesha kwamba, mihimili ya utajiri na madaraka ilipinga na kukabiliana vikali na harakati ya kusimamisha na kutekeleza uadilifu, kwa kutumia vitisho, kurubuni, kuchafua shakhsia za watu na hata kuwasha moto wa vita. Ni mpaka pale Mtume wa Mwenyezi Mungu alipoasisi utawala, ndipo alipoweza kutumia nguvu ili kupambana na upendeleo wa kidhalimu na tofauti za kimatabaka na kuzuia unyonyaji dhidi ya matabaka ya wanyonge. Na sababu ni kuwa, mtukufu huyo alikuwa akijua vyema kwamba, itakapotamalaki haki na uadilifu, ndipo kila mtu ataweza kunufaika inavyostahiki na jitihada zinazokubalika na sahihi za kiuchumi anazofanya, bila ya kuwepo ndani ya jamii ya Kiislamu, ishara yoyote ya uburuzaji usio wa kiutu na wa kidhalimu unaofanywa na wanaojilimbikizia mali, wala umasikini na ufukara wa wanyonge ndani ya jamii hiyo.

Moja ya alama za usimamishaji haki na uadilifu wa kiuchumi ni kuziba ufa wa kimatabaka baina ya matajiri na wanyonge. Katika hatua iliyolenga kuifunza na kuionyesha jamii ya wanadamu kwamba uadilifu wa kiuchumi katika Uislamu una malengo na mapiganio ya kiutu tofauti na ilivyo mifumo yote ya ubepari, siku moja Bwana Mtume SAW alimtuma mmoja wa masahaba zake, ambaye alikuwa kijana masikini sana na asiye na hadhi yoyote, akampose binti wa mmoja wa matajiri. Sahaba yule alitekeleza agizo la Mtume, akaenda kumposa binti wa ukoo wa maashrafu na matajiri. Baba wa binti huyo alimuuliza yule sahaba kwa mshangao, ni kweli Mtume wa Allah amekutuma kwa ajili ya jambo hili? Alipopewa jibu la 'ndiyo', yule bwana alisema, itabidi mimi mwenyewe niende kwa Mtume na kumuuliza kama ni kweli yeye ametoa pendekezo hilo. Wakati alipobaini kuwa ni kweli Mtume alipendekeza posa hizo, yule bwana akawa angali ana hatihati kama je akubali kumuozesha binti yake kijana yule au la? Akiwa katika hali hiyo, binti yake ambaye alikuwa mtoto mwenye basira alimwambia baba yake: Unataka kulikataa ombi la Mtume wa Allah? Mimi niko tayari kuolewa na kijana huyo maadamu ndio mtazamo wa Mtume; na wewe pia furahia ndoa hii kwa ajili ya kupata radhi za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Al Kafi 5/34

Na naam mpendwa msikilizaji, ikiwa utamaduni wa kupigania uadilfu utarasimishwa katika kila jamii, aina zote za upendeleo wa kidhalimu na ubaguzi wa kiuonevu pamoja na majivuno na uwekaji mipaka bandia kati ya matabaka tofauti ya jamii vitafifia, na moyo wa muawana na ushirikiano, kusaidiana wakati wa shida, umoja na mshikamano vitahuika miongoni mwa wanajamii wote.

Ni kwa kusimamia mtazamo huu wa msingi na wa kiuadilifu, ndipo Bwana Mtume SAW akaweza kuziunganisha kiudugu nyoyo za Waislamu na kujenga jamii ya Kiislamu ya kupigiwa mfano, ambayo ndani yake, waumini walisaidiana katika upeo wa juu kabisa wa udugu, huruma na upendo katika utumiaji nyenzo na suhula zao zote za maisha. Na kwa ajili ya kutatua shida na mahitaji waliyokuwa nayo, wakawa wanatumia bila wasiwasi wowote suhula zao za pamoja. Na hata katika wakati wa Jihadi, Muislamu mmoja alibeba jukumu la kuihudumia familia ya ndugu yake Muislamu aliyekuwa kwenye Jihadi na kuikidhia mahitaji yote iliyokuwa nayo. Lakini mbali na hayo, wakati Waislamu walipokabiliwa na vitisho, kususiwa katika biashara na kuandamwa na anuai za maudhi na mateso ya mabwanyenye wa Makka waliokuwa wakipiga vita uadilifu; na hivyo kulazimika kuhajiri kuelekea Madina huku wakiacha nyuma mali zao na kila kitu chao, watu wa Madina waligawana nao mali na suhula zao zote ndugu zao hao, bila kinyongo wala kuwa na tamaa ya chochote. Mtindo huo wa maisha ya kiutu na uadilifu ulijenga hatua kwa hatua utamaduni wa "kujitolea", wa mtu kutanguliza kwanza na kujali zaidi mahitaji ya wengine kuliko yake mwenyewe, ambao uliifikisha jamii ya Kiislamu kwenye kilele cha uadilifu na moyo wa kujitoa mhanga. Katika aya ya tisa ya Suratul-Hashr, Qur'ani tukufu inaielezea sifa hiyo tukufu na yenye kutoa ilhamu kwa kusema: " …wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji…" Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kuwa, sehemu ya 41 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 42 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/