Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (59)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 59 kitamtambulisa kwenu Mulla Muhammad Ali Kani, alimu na mwanazuoni mkubwa na mwanamapambano aliyeishi mwishoni mwa karne ya 13 na mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria ambaye alikuwa na taathira kubwa mno katika matukio ya kisiasa na kiutamaduni ya Iran. Jiungenii nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegelea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Mulla Ali Kani alizaliwa 1220 Hijria katika familia ya kijijini ambayo kazi yake kuu ilikuwa ni kilimo. Familia hii ilikuwa na ushirikiano mkubwa katika kutekeleza mambo yao kuanzia mke, mume na watoto. Familia hii ilikuwa ikifanya kazi na hima na kuweza kujipatia kipato cha kuendeshea maisha katika mazingira magumu ya maisha. Katika zama hizo kuwa na elimu ya msingi ilikuwa ikitosha kwa ajilii ya kujidhaminia maisha na hakukuwa na haja ya kuwa na elimu ya kiwango cha juu kama sekondari na Chuo Kikuu. Hivyo hata familia ya Mulla Ali Kani haikuwa ikiona udharura na haja ya yeye kuendelea na masomo ya juu baada ya kukamilisha masomo ya elimu ya msingi. Hata hivyo shauku na mapenzi makubwa ya kusoma aliyokuwa nayo yalimfanya ang'ang'anie kuendelea na masomo ya juu. Baada ya miaka 20 hatimaye alifanikiwa kuikinaisha familia yake ambayo ilimruhusu aendelee na masomo ya ngazi za juu.

Mulla Ali ambaye alizaliwa katika kijiji cha Kan moja ya vijiji vya kando kando ya Tehran, ajiunga na shule ya Marwi moja ya shule mashuhuri za kidini na zilizokuwa na itibari kubwa. Katika zama hizo shule hiyo ilikuwa ikiendeshwa chini ya usimamizi wa Mirza Masih Mujtahid, fakihi, mujtahidi na mwanazuoni ambaye alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano na watawala madhalimu na wa kikoloni wa Uingereza na Urusi ya Tsar. Muda mfupi baada ya kukamilisha masomo yake ya dini, Mulla Ali Kani alielekea katika Chuo cha Kidini (Hawza) katika mji wa Isfahan Iran na baadaye Najaf na Karbala huko Iraq. Ali Kani ambaye alisoma masomo yake ya awali katika kijiji alichozaliwa, alikuwa na maisha ya kimasikini mno. Akiwa Najaf Iraq pia, hali yake ya maisha ilikuwa mbaya na ngumu kiasi kwamba, alikuwa akiishi kwa kula mikate mikavu aliyokuwa akiikusanya kando kando ya Haram ya Imam Ali (as) na Masjid Sahlah. Hata hivyo ugumu huo wa maisha katu haukudhoofisha irada na azma yake ya masomo na hakuwa akifikiria kitu kingine ghairi ya kukidhi na kukata kiu yake ya elimu.
Hata hivyo nukta muhimu ya kuashiria hapa ni kuwa, Ali Kani yeye ndiye aliyeamua kuishi maisha haya ya kimasikini. Kwani nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, hata alipokuwa akipatiwa chakula kizuri hakuwa tayari kukila. Daima alikuwa akijiepusha kula vyakula vitamu na vya aina kwa aina.

Mulla Ali Kani alisoma elimu na taaluma mbalimbali kwa walimu kama Sheikh Hassan Kashiful Ghitaa, Sayyid Ibrahim Qazvini Hairi, Sheikh Murtadha Ansari na Muhammad Hassan Najafi mashuhuri kwa jina la Swahib al-Jawahir. Baada ya miaka mingi ya hima na idili katika kutafuta elimu, hatimaye akafanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad. Mwaka 1262 Hijria alirejea Tehran. Katika zama hizo, Ali Kani alikuwa mmoja wa Maulamaa wanne wakubwa wa Iran katika zama hizo ambao daraja yao ya kielimu iliungwa mkono na kuidhinishwa na Swahib al-Jawahir na Ijtihadi yao kubainishwa wazi.
Akiwa mjini Tehran, Mulla Ali Kani alijishughulisha na kuandika vitabu na hatua kwa hatua akawa akitumia kipato kilichotokana na kuuza vitabu vyake katika njia ya kujenga na kuboresha vijiji. Hilo lilimbadilisha na kumuondoa katika mwanafunzi masikini wa masomo ya dini na kuwa alimu na msomi tajiri. Pamoja na hayo aliendelea kuishia maisha ya kimasikini na kujinyima na kujiepusha kabisa na anasa, starehe na mambo ya mapambo yasiyo ya lazima. Aliutumia utajiri wake kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya masikini na kutatua matatizo yao ya kimaisha sambamba na kuhudumia kueneza mafundisho ya Uislamu. Ali Kani alitambulika baina ya watu katika jamii kwa ukarimu na kusaidia watu wasiojiweza. Hakuna mtu ambaye alikuwa akimuendea na shida na kurejea mikono mitupu. Hata zawadi alizokuwa akipatiwa na watu alikuwa akiwapatia wenye kuhitaji na yeye kubakia mikono mitupu.
Hatua kwa hatua Mulla Ali Kani akaondokea na kufahamika kuwa alimu na msomi mwenye satwa na ushawishi katika mji wa Tehran na akthari ya watu wakawa wakimkalidi na kumfuata katika hukumu za Kiislamu. Alimu huyo alikuwa na ushawishi mkubwa kiasi kwamba, watawala wa wakati huo walikuwa wakimrejea kwa ajili ya kutatua hitilafu zao za kisheria.

Ili tutambue vyema nafasi muhimu na mchango wa Mulla Ali Kani katika uga wa kijamii na losiasa tunapaswa kufahamu kwa namna fulani hali ya mambo na anga ya kisiasa na kiutamaduni iliyokuwa ikitawala katika zama hizo nchini Iran.
Miaka miwili kabla ya kurejea Tehran Mulla Ali Kani, mwishoni mwa duru ya mtawala wa tatu wa ukoo wa Qajar na mwanzoni mwa utawala wa kifalme wa Nasser al-Din Shah kulikuwa kumedhihiri kundi jipya la kidini kwa jina la Babiya. Kundi hili lilikuwa mfuasi wa Ali Muhammad Shirazi ambaye awali alikuwa akijiita kuwa mlango wa Imamu aliyeko ghaibu na kisha baadaye akadai kwamba, bali yeye mwenyewe ndiye Imamu Mahdi aliyeahidiwa. Hatua kwa hatua Ali Muhammad Shirazi akaanzisha sheria mpya na akasema na kuandika mambo ambayo kimsingi hayakuwa tofauti na kudai Uungu. Maulamaa wa Shiraz wakaitisha kikao ili kutahini madai yake. Ali Muhammad Shirazi alidai katika kikao hicho kwamba, kutokana na kuweko dini yake mpya, hivyo dini ya Uislamu na sheria zake zimefutwa. Hata hivyo hakuweza kutoa majibu kwa maswali aliyoulizwa na Maulamaa ili athibitishe madai yake. Kwa muktadha huo, serikali ikajibu takwa la Maulamaa na kumtia mbaroni na kisha kumpeleka uhamishoni. Hata hivyo, wafuasi wake ambao waliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Babiya walianzisha harakati za umwagaji damu katika miji mbalimbali ya Iran na kuuawa shakhsia wakubwa wa kidini na kisiasa.

Katika mazingira kama haya, Mulla Ali Kani akiwa mmoja wa wanazuoni mahiri wa Iran na aliyekuwa akikubaliwa mno mjini Tehran na wananchi na serikali kutokana na nafasi yake muhimu ya kijamii, alifanya mdahalo mara kadhaa na kundi la Babiya akifanya juhudi za kuwarejesha katika Uislamu. Hata hivyo baada ya kuona kung’ang’ania kwao katika mambo ya kikafiri alitoa hukumu kwamba, ni makafiri na wametoka katika dini, hukumu ambayo ilikuwa imetolewa hapo kabla pia na Shahidi wa Tatu.
Hatimaye Ali Muhammad Shirazi aliuawa kwa kunyongwa na kundi la Babiya likawa limetokomezwa kutokana na uwepo wa Kansema mwenye ustahiki kama Amir Kabir. Amir Kabir alikuwa mtu huru, mwenye imani, muenezaji wa elimu na mwenye kupenda utamaduni na anahesabiwa kuwa mmoja wa waasisi wa marekebisho na waenezaji wa fikra bora katika uwanja wa ufundishaji, malezi na utamaduni nchini Iran. Amir Kabir alifanya juhudi kubwa katika njia ya mafanikio ya wananchi wa Iran na katika kipindi alichokuwa Kansela alitoa huduma na kufanya marekebisho mengi.

Aidha alifanya juhudi kubwa za kuzuia uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Iran. Baada ya hapo, kulifanyika njama nyingi dhidi ya Amir Kabir. Hatimaye baada ya miaka miwili tangu kunyongwa kiongozi wa Babiya, Kansela Amir Kabir aliuzuliwa katika cheo chake na kupelekwa uhamishoni huko Kashan. Taathira chanya ya alimu huyu mwanamapambano katika medani ya kisiasa na kijamii ya Iran haiishi hapa. Hata hivyo kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu kwa leo, sina budi kuishia hapa, tukutane tena katika sehemu ijayo ambapo tutaendelea na maudhui hii.
Hadi wakati huo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Kwaherini.