Dec 13, 2022 07:14 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 6

Kama ilivyokuwa katika vipindi vilivyopita, kipindi hiki pia kitaendelea kuchambua na kujadili kwa undani kidogo fikra na mielekeo ya Uwahabi ili tupate kuujua vizuri zaidi na pia wale wanaoufuata.

Bismillahir Rahmanir Raheem. Tunaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu mjuzi wa siri zote ambapo yaliyopita na yanayokuja yote ni mamoja Kwake na hakuna kinachofichika Kwake. Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi hivi vya Hakika ya Uwahabi.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulijaribu kuchambua baadhi ya itikadi za pote hili potofu linalowakufurisha Waislamu ambapo tulisema kuwa Mawahabi kama walivyo Mayahudi wanaamini kuwa Mwenyezi Mungu ana mwili kama wa mwanadamu. Kundi hilo linayakufurisha madhehebu mengine yote ya Waislamu na kuhalalisha mali na damu zao. Linawajibisha kuuawa kwao na kuamini kwamba hakuna tofauti kati ya Masuni na Mashia kuhusu hilo. Kwa msingi huo tuna lengo la kuchambua kwa kina kidogo fikra na mielekeo ya Uwahabi ili tupate kuujua vizuri zaidi na pia wale wanaoufuata.

************

Moja ya mitazamo na fatwa za Ibn Taymiyyah ni kwamba ni haramu kujenga kuba, ngome au jengo lolote juu ya makaburi ya manabii, mawalii na watu wema. Kwa mtazamo wake, ni wajibu kuyabomoa majengo kama hayo. Ibn Qayyim, mwanafunzi wa Ibn Taymiyyah anasema: “Ni wajibu kubomoa jengo lililojengwa juu ya makaburi, na wala haijuzu kuliacha katika hali hiyo hata kwa siku moja, baada ya kuwa na uwezo wa kulibomoa."

Fatwa kama hizo zinatolewa katika hali ambayo mijengo kwenye makaburi ya viongozi wa kidini, kisiasa, kisanaa, kifasihi au mashujaa wa kitaifa ni jambo la kawaida kabisa katika jamii na mataifa karibu yote ambapo watu hulipa jambo hilo heshima kubwa. Kwa mfano, kati ya mwaka 1844 na 1851, Wakristo walijenga "Makaburi ya Stalino" kwenye mteremko wa kilima kimoja, ambayo yanajumuisha sehemu ya utalii, masanamu, mabustani na makanisa ya Kiprotestanti.

Makaburi ya Stalino 

Wahindu walijenga jengo juu ya kaburi la mkewe Shah Jahan kwa jina la Adhim ambalo ni mashuhuri kwa jina la Taj Mahal ambalo leo linahesabiwa kuwa moja ya mijengo mashuhuri zaidi ya kisanaa na usanifu majengo. Kanisa la Kaburi Takatifu limejengwa juu ya kaburi ambalo linaaminika na Wakrito kuwa ndiko alikozikwa Nabii Issa Masih (as) na wengine kuitakidi kuwa ndiyo sehemu alikosulubiwa na kisha kupaa mbinguni. Kufikia mwaka 2008, karibu piramidi 138 ziligunduliwa nchini Misri, nyingi ambazo zilikuwa makaburi ya mafarao na wake zao, ambayo yalijengwa wakati wa Ufalme wa Kale na wa Kati. Wachina walijenga kaburi lenye eneo la kilomitamraba 52 kwa ajili ya kumuenzi mfalme wao wa kwanza, ambaye aliondoa uhasama baina yao na kuwaletea umoja na uadilifu, na kujenga hapo masanamu ya askari wengi wa mawe ili wamlinde na kumsaidia mfalme huyo. Kaburi hilo ni moja ya maajabu ya ulimwengu wa mwanadamu na bila shaka inachukuliwa kuwa kazi ya kushangaza katika ulimwengu wa sanaa.

Jengo la kihistoria la Taj Mahal nchini India

Katika dunia nzima mataifa tofauti hugharamika pakubwa kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi turathi zake za kihistoria na pia kuziarifisha kwa walimwengu. Kimsingi athari za watu wa kale huwa ni sehemu ya turathi za kiutamaduni za taifa lolote lile ambazo huarifisha utambulisho wa kidini na kiutamaduni wa taifa hilo, utambulisho ambao ndio hujenga maisha ya vizazi vya leo na vijavyo. Je, si ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona kwamba licha ya ukweli huo baadhi ya watu huamua kuharibu utamaduni na ustaarabu huo wenye thamani kubwa ya kihistoria kwa mikono yao wenyewe?

***********

Kisingizio kinachotolewa na Mawahabi katika kuhalalisha kitendo chao hicho cha kuaibisha na kusikitisha kwa wakati mmoja ni kwamba hudai kuwa Waislamu huzuru makaburi ya watutufu na viongozi wao wa kidini wakiwemo, Mitume, Maimamu na mawalii wema kwa madhumuni ya kufungamana nao, jambo ambalo wanalichukulia kuwa ni shirki. Wanadai kwamba hufika kwenye makaburi hayo kwa lengo la kuwaswalia, kusoma Qur'ani na kuomba dua na mahitaji yao kutoka kwa watu waliozikwa kwenye makaburi hayo. Kwa matazamo wa Mawahabi, wafu hawana athari tena humu duniani hivyo hawawezi kujibu dua na maombi na kwa hivyo kuwaomba mahitaji na haja hakuna maana. Wanadai kuwa kuswali na kuwasomea Qur'ani wafu ni bida' ambayo ni haramu. Kwa mtazamo wa Mawahabi, kuzuru makaburi na kutabaruku na maeneo matakatifu walikozikwa mawalii ni haramu na mtu anayefanya kitendo hicho au hata kufunga safari kwa ajili ya kuyatembelea maeneo hayo yakiwemo ya Maimamu watoharifu, huwa ni kafiri anayepasa kuuawa.

Kubomolewa maeneo matakatifu na misikiti na Mawahabi

Swan'ani, mmoja wa mamufti wa Kiwahabi anasema: “(Mji wa) Mashhad ni sawa na sanamu. Hawa wanayafanyia  makaburi ya mawalii wao yaleyale waliyokuwa wakiyafanyia washirikina masanamu yao katika zama za ujahiliya...” Pia kwa mujibu wa Baraza la Kudumu la Fatwa la Mawahabi, "Kujenga juu ya makaburi ni bida' mbaya, ambapo shirki hufanyika kwa kuwaadhimisha waliozikwa humo. Hiyo ni njia inayoelekeza kwenye shirki na kwa hivyo ni wajibu kwa mtawala wa Waislamu au naibu wake kutoa amri ya kubomolewa majengo yaliyojengwa juu ya makaburi na kuyasawazisha na ardhi, ili kukabiliana vilivyo na uzushi huo na kufunga njia ya ushirikina." Naseer ad-Din Albani, mufti mwingine wa Kiwahabi, alitoa pendekezo kwa utawala wa Saudi Arabia uharibu kuba la kijani lililoko kwenye Msikiti wa Mtume (saw). Alisikitishwa sana na ukweli kwamba kuba hilo lingalipo kwenye msikiti huo hadi sasa.

Mawahabi walitumia visingizio na fatwa hizo hizo zisizo na msingi, kubomoa na kuharibu mahali alipozaliwa Mtume Mtukufu (saw), nyumba yake na mkewe Bibi Khadija (sa), nyumba ya Imam Ali  na mkewe Bibi Fatima (as), makuba na makaburi ya Maimamu, masahaba  na viongozi wengine mashuhuri wa kidini waliozikwa kwenye makaburi ya Baqee na pia kuharibu madhihirisho mengine mengi ya kihistoria ya Uislamu. Lakini je, ni kweli kuwa kuzuru makaburi ya Maimamu na wakuu wa kidini, kuwaswalia, kuwasomea Qur'ani, kushikamana na kutawasali nao ni shirki? Je, mambo hayo yalikatazwa na Mtume au kuarifishwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyoharamishwa?

Makaburi ya Baqee kabla ya kuharibiwa na Mawahabi

Katika Aya ya 32 ya Surat al-Haj, Mwenyezi Mungu anatuamuru tuheshimu nembo zake na kusema kuwa kufanya hivyo ni katika takwa ya nyoyo.

Anasema: Ndio hivyo! Na anayetukuza nembo za Mwenyezi Mungu, basi hiyo ni katika takwa ya nyoyo.

Neno "Sha'air" lina maana ya ishara na alama  na "Sha'air Allah' inamaanisha mambo ambayo ni alama na ishara za dini ya Mwenyezi Mungu. Ishara hizo ni mwongozo kwa watu wanaotaka kuufikia ukweli wa dini ya Mwenyezi Mungu. Qur’ani Tukufu inaiarifisha milima miwili ya Swafa na Marwa pamoja na ngamia ambao hutayarishwa kwa ajili ya kuchinjwa siku ya Eid al-Adha, kuwa miongoni mwa alama za kiungu. Itawezekana vipi mlima au ngamia kutajwa kuwa ni alama ya dini ya Mwenyezi Mungu, lakini kaburi au nyumba ya Mtume wa Rehema aliyetumwa kuwaongoza wanadamu, au makaburi ya watoto wake watoharifu, ambao walistahimili matatizo na mateso mengi kwa ajili ya kulinda dini ya Mwenyezi Mungu, wasichukuliwe kuwa sehemu ya alama za dini hiyo?!

Milima ya Swafa na Marwa katika mji mtakatifu wa Makka

Qur'ani Tukufu inatuamuru moja kwa moja kutii, kupenda na kuwaheshimu watoto na jamaa wa Mtume Mtukufu (saw) ambapo inasema katika Aya ya 23 ya Surat ash-Shura: "Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika ndugu."

Haitoshi kwa mapenzi na upendo kutimia nyoyoni tu bali mapenzi hayo yanapaswa kuonyeshwa kwenye tabia na matendo yetu. Moja ya madhihirisho ya mapenzi hayo ya dhati ni kutii amri ya Mtume na Maimamu Watoharifu (as), na dhihirisho jingine la hilo ni ujenzi wa majengo juu ya makaburi ya Mtume na jamaa zake, na pia makaburi ya viongozi wengine wa dini. Kwa kuzingatia hayo, ni vipi kufuata amri hiyo ya Mwenyezi Mungu iliyo wazi ndani ya Qur'an' Tukufu kutachukuliuwa kuwa ni bida' na kuwatuhumu wale wanaoitekeleza kuwa ni makafiri?!!

*************

Kuna dalili nyingine nyingi katika Qur'ani Tukufu zinazothibitisha usahihi wa vitendo na amali hizo. Miongoni mwa dalili hizo, tunaweza kuashiria Aya ya 36 ya Surat Noor, ambapo Mwenyezi Mungu anaashiria juu ya utukufu wa nyumba ambazo ndani yake Mwenyezi Mungu hukumbukwa na kutukuzwa. Nyumba za wanaume na wanawake ambao biashara zao haziwasahaulishi kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Je, Mtume wa Allah (saw), Imam Ali (as), Bibi Khadijah na Bibi Fatima (as) si mifano ya watu kama hao? Je, hatupaswi kuheshimu nyumba zao?

Nyumba ya Mtume (saw) na Bibi Khadija (sa) ambayo iliharibiwa na Mawahabi

Maqam Ibrahim ni jiwe lililo pembeni ya al-Kaaba ambako kuna alama za nyayo za Nabii Ibrahim (AS) juu yake. Katika Aya ya 125 ya Surat al-Baqarah na Aya ya 97 ya Surat Aal-Imran, mahali hapo pametambuliwa kuwa moja ya alama na ishara za Mwenyezi Mungu ambapo waumini wametakiwa kuswali na kutekeleza ibada zao hapo. Katika hali hiyo, je mahali ambapo Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu aliomba na kutekelezea ibada zake hapo asubuhi na jioni si katika ishara zake Mungu Muumba? Je, mahala hapo hapapaswi kuthaminiwa? Je, waumini hawapaswi kutamani kuwepo mahala patakatifu kama hapo na kusimama mbele ya Muumba wao kwenye maombi na ibada zao? Je, maeneo kama hayo yanastahili kuharibiwa?

Maqaam Ibrahim (as) pembeni ya al-Kaaba

Tutazungumza zaidi kuhusu itikadi nyingine potofu za Mawahabi katika vipindi vijavyo Inshallah. Tutabainisha iwapo ni kweli kama wanavyoamini wao kwamba Mtume mpendwa wa Uislamu (saw) na Maimamu Watoharifu (as) hawana athari yoyote baada ya wao kuaga na kuondoka kimwili duniani na kuwa kutawasali nao hakujuzu na ni mfano wa ushirikina, au dini tukufu ya Uislamu ina maoni tofauti kuhusu jambo hilo?