Dec 17, 2022 18:39 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (60)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 60 kitaendelea kumzungumzia Mulla Muhammad Ali Kani, alimu, mwanazuoni mkubwa na mwanamapambano aliyeishi mwishoni mwa karne ya 13 na mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria ambaye kama tulivyosema katika kipindi chetu kilichopita alikuwa na taathira kubwa mno katika matukio ya kisiasa na kiutamaduni ya Iran. Jiungeni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegelea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Tulisema kuwa, Amir Kabir alikuwa mtu huru, mwenye imani, muenezaji wa elimu na mwenye kupenda utamaduni na anahesabiwa kuwa mmoja wa waasisi wa marekebisho na waenezaji wa fikra bora katika uwanja wa ufundishaji, malezi na utamaduni nchini Iran. Amir Kabir alifanya juhudi kubwa katika njia ya mafanikio ya wananchi wa Iran na katika kipindi alichokuwa Kansela alitoa huduma na kufanya marekebisho mengi. Aidha alifanya juhudi kubwa za kuzuia uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Iran. Baada ya hapo, kulifanyika njama nyingi dhidi ya Amir Kabir. Hatimaye baada ya miaka miwili tangu kunyongwa kiongozi wa Babiya, Kansela Amir Kabir aliuzuliwa katika cheo chake na kupelekwa uhamishoni huko Kashan. Baadaye Amir Kabir akauawa. Mirza Khan Nuri yule yule mtu ambaye akipata himaya na uungaji mkono wa Waingereza aliandaa mazingira ya kuuzulia na hatimaye kuuawa Amir Kabir akachukua hatamu za uongozi na kuwa Kansela wa Pili wa Nasser al-Din Shah

Katika zama za Ukansela wa Mirza Nuri Waingereza walitenganisha na Iran eneo la Haraat na Afghanistan na hili lilitokana na uongozi mbaya na usio na ustahiki wa Kansela wa wakati huo wa Iran mkabala na Waingereza.

Kansela wa tatu alikuwa Mirza Hosein Khan Moshir od-Dowleh Sepahsalar. Bwana huyu alikuwa akieneza fikra zilizo dhidi ya dini akitumia visingizio mbalimbali. Moja ya sababu muhimu zilizokuwa zikitumiwa kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu ni neno uhuru. Kama ilivyo hii leo pia suala la uhuru limekuwa likitumiwa vibaya na kwa ajili ya matashi ya kisiasa. Kupitia kisingizio hicho walikusudia kukabiliana na vazi la hijabu na sheria nyingine za kidini zinazohusiana na ndoa na familia. Kansela Mirza Hussein Khan Sepahsalar akamuandalia mfalme kijana wa wakati huo safari kadhaa za Ulaya na mfalme huyu ambaye alikuwa ameathirika na dhahiri ya tamaduni na staarabu za Kimagharibi alikuwa amekusudia kutoa amri ya kupigwa marufuku vazi la hijabu nchini Iran. Alikuwa ameanza kulijadili na kulizungumzia hilo ndani ya baraza lake la mawaziri ingawa alikabiliwa na upinzani mkali na wanawake waumini ndani ya utawala huo.

Kansela Mirza Hussein Khan Sepahsalar

 

Mulla Ali Kani akamuandikia barua Shah Qajar na kumtahadharisha juu ya kuchukua hatua hiyo. Katika barua hiyo, Mulla Ali Kani alisema, uhuru ambao ni sababu ya mtu kuachana na dhati ya kimaumbile hauna matokeo mengine ghairi ya kutumbukia katika uchafu wa kimaadili na kuabudu matamanio ya nafsi. Alimtahadharisha mfalme huyo kwamba, dhahiri ya neno uhuru licha ya kuwa linafurahisha na lenye kuhadaa lakini batini yake lina lengo baya na chafu. Natija ya barua hiyo iluiyokuwa na indhari na hekima kubwa ikawa ni kumfanya Nasser al-Din Shah asichukue uamuzi wa kutoa amri ya kuruhusu kuondolewa vazi la hijabu. Hata hivyo, wakoloni hawakuacha njama na mipango yao michafu kwani walifanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, wanafikia malengo yao. 

Katika zama hizo Allama Mulla Ali Kani alikuwa ngao na kizingiti imara dhidi ya mkoloni Muingereza na alisimama kidete kukabiliana na njama na mipango michafu ya mkoloni huyo dhidi ya taifa hili. Baada ya utawala wa kifalme wa Iran wakati huo kutiliana saini mkataba wa kuchimba madini na Myahudi mmoja Muingereza kuliibuka upinzani dhidi ya mkataba huo. Lord Curzon, mmoja wa wanasiasa wa Uingereza wakati huo ameandika: Mkataba huu ulikuwa na maana ya kukabidhiwa kikamiilifu vyanzo vyote kwa maajinabi ambapo mkataba huu hauna mfano wake katika historia."

Maulamaa wa wakati huo wakiongozwa na Mulla Ali Kani nao walikuwa mstari wa mbele kupinga khiyana na usaliti huo uliofanywa na utawala wa wakati huo wa Iran wa kukabidhi vyanzo vyote vya utajiri wa madini kwa maajinabi. Waliamua kumuandikia barua mtawala Nasser al-Din Shah kwa saini ya Mulla Ali Kani. Barua hiyo ikamfikkia mfalme ambapo ndani yake alionywa na kutahadharishwa kuhusiana na mkataba huo. Mbali na kulaumiwa kwa lugha kali, mtawala huyo alikumbushwa kwamba, yeye siyo mmiliki wa mali na utajiri wa Wairani na kwamba, kama utawala wake una uhalali basi hilo linalotokana na himaya na idhinisho la Maulamaa wa Kiislamu. Aidha sehemu moja ya barua hiyo ilieleza kuwa, licha ya kuwa, Nasser al-Din Shah ndiye kiongozi lakini hana ruhusa ya kuuza mali za taifa na za wananchi bila idhini ya Maulamaa na mafakihi wa Kiislamu.

 

Katika sehemu nyingine ya barua yake hiyo, Mulla Ali Kani alimwambia mfalme Shah: Mkataba kama huu ni chimbuko la wageni kuwa na udhibiti kwa ardhi za Kiislamu, jambo ambalo halikubaliwi katu na Maulamaa wa Kiislamu na watu ambao walikuwa na mchango katika mchakato wa kutiwa saini mkataba huo bila shaka ni maadui wa damu wa Uislamu na Iran. Pamoja na mambo mengine, barua hiyo ilitaka kuuzuliwa Kansela Mirza Hussein Khan Sepahsalar.

Barua ya Mulla Ali Kani ilikuwa na taathira mno kiasi kwamba, wakati Mfalme Nasser al-Din Shah anarejea Tehran kutoka katika safari yake ya Ulaya hakuthubutu kurejea pamoja na Kansela wake huyo. Kabla ya kurejea Tehran Nasser al-Din Shah alimuuzulu Mirza Hussein Sepahsalar kutoka katika cheo chake cha Ukansela na kufuta mkataba huo uliokuwa umezusha makelele mengi.

Baada ya kuwasili Tehran Mfalme huyo alikwenda kuonana na Haj Mulla Ali Kani ambapo sambamba na kumuomba msamaha alimpa habari ya kufutwa mkataba huo.

 

Kuanzia wakati huo, mbinu ya Mulla Ali Kani ya kutetea vyanzo vya utajiri vya Iran na kukabiliana na uvamizi wa kigeni ikawa imejengeka juu ya msingi wa hatua za Maulamaa katika medani ya siasa nchini Iran. Mbinu ambayo haikutoa fursa kwa wafalme ya kuwa na utulivu wa kufanya watakacho.

Hatimaye baada ya miaka mingi ya hima na idili mtawalia iliyoambatana na mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu, Mulla Ali Kani aliaga dunia 1306 Hijria akiwa na umri wa miaka 86. Mazishi yake yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu katika miji ya Tehran na Rey. Mwanazuoni huyu amezikwa katika Haram ya Shah Abdul-Adhim Hassani iliyoko katika mji wa Rey nje kidogo ya jiji la Tehran. Umashuhuri wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, hata wafuasi wa dini nyingine walishiriki katika shughuli ya kuuaga na kuusindikiza mwili wake.

Kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.