Jumapili, 08 Januari, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 15 Mfunguo Tisa Jamaduthani 1444 Hijria sawa na tarehe 8 Januari 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali bin Abi Twalib na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu. ***
Tarehe 15 Jumadithani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 673 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah. ***
Miaka 381 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78. Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya Abu Raihan Biruni msomi mashuhuri wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake. ***
Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na maulamaa wapigania uhuru wa Iran. Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran. ***
Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza. Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapigano dhidi ya utawala wa Othmania mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 na kupata ushindi. Mwaka 1903 mtawala wa Kiothmania alitimuliwa katika eneo la ya al-Ahsa huko Hijazi na tukio hilo lilikuwa jiwe la msingi wa kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cga Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala Hussein Bin Ali Sharif aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na akatwaa kwa nguvu eneo hilo la Hijaz. Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mtawala huyo huyo wa Kiwahabi, Abdul-Aziz Ibn Saud alijitangaza kuwa kiongozi wa Hijaz. Mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mtawala wa Hijaz na Najd na tarehe 8 Januari mwaka 1932 Abdul Aziz alitangazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hadi kutwaa madaraka ya eneo lote la Hijaz, watu wa kizazi cha Aal Saudi walifanya mauaji mengi na umwagaji damu mkubwa na kuwalazimisha watu wa maeneo hayo kufuata fikra na itikadi potufu za kiwahabi. ****