Jan 08, 2023 11:45 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 8

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba Mawahabi wanaharamisha kutawasali na Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu (as) na hivyo kuharibu majengo yanayojengwa kwenye makaburi yao na wakati huo huo kuhalalisha damu na mali za Waislamu wanaozuru maeneo hayo matakatifu.

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba Mawahabi wanaharamisha kutawasali na Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu (as) na hivyo kuharibu majengo yanayojengwa kwenye makaburi yao na wakati huo huo kuhalalisha damu na mali za Waislamu wanaozuru maeneo hayo matakatifu.

 

Tulijadili baadhi ya dalili na hoja zisizo na msingi za Mawahabi kuhusu suala hilo na tukaahidi kuendelea kujadili hoja zao nyingine katika kipindi hiki. Hivyo endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika na tutakayoyajadili humu, karibuni.

Bismillahir Rahmanir Raheem. Tunaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye aliteremsha Qur'ni Tukufu ili iwe wasila na njia ya wongofu kwa wanadamu wote, wanadamu ambao hutumia akili na hisia zao za kimaumbile kwa ajili ya kujiweka mbali na mambo yanayokwenda kinyume na thamani zao za utu.

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjii Tehran. Hii ni sehemu ya nane ya kipindi hiki cha Hakika ya Uwahabi ambapo tunajadili humu jinsi Uwahabi ulivyoanzishwa na baadhi ya fikra na itikadi zao potofu kuhusiana na suala zima la Uislamu na Waislamu.

************

Moja ya dalili zinazotolewa na Mawahabi kwa ajili ya kuharamisha tawassul ni kwamba wanadai kuwa Waislamu wanaofanya hivyo hutawasali na watu ambao tayari wameaga dunia na ambao hawawezi kuwasaidia kwa lolote lile. Kwa mtazamo wa Mawahabi kutawasali na wafu kwa hakika ni kuzungumza na kuomba msaada kutoka kwa kitu au mtu asiyekuwepo na kwamba kufanya hivyo ni jambo lisilo na athari yoyote na kuwa ni upuuzi mtupu. Muhammad bin Abdul Wahhab anasema: 'Hakuna tatizo lolote katika kutawasali na mtu aliye hai; lakini kutawasali na mfu ni kuzungumza na kitu kisichokuwepo na hivyo ni jambo la upuuzi, baya na linalokemewa.'

Sasa baada ya kusikiliza maneno hayo yasiyo na mantiki hebu sikiliza Aya ifuatayo ya 169 ya Surat Aal Imran katika Qur'ani Tukufu inavyosema: Na usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa wamekufa, bali wako hai mbele ya Mola wao wanaruzukiwa.

Sikiliza pia maneneo yenye maana kama hiyo kutoka kwenye vitabu vya kutegemewa vya Ahlu Sunna kama vile Swahih Bukhari, Swahih Muslim na vinginenvyo ambavyo vinasema: "Baada ya kumalizika vita vya Badr, Mtume Mtukufu (saw) alimuita kila mmoja wa mashahidi waliouawa na maadui na kisha kuwaambia wote: Je, mmefikia yale mliyoahidiwa na Mola wenu? Mimi nimeyapata kuwa ya kweli yale yote niliyoahidiwa na Mola wangu. Kisha aliwalaumu wale waliokadhibisha Uislamu na waliyoambiwa na Mtume wao. Walipoyaona hayo na kwamba Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akizungumza na watu waliouawa kwenye medani ya vita, masahaba walishangaa sana na kumuuliza: Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, unawaita wafu na kuzungumza nao? Akawajibu: Watu hawa waliouawa wanasikia vizuri zaidi ninayoyasema kukulikoni nyinyi ila tu hawana uwezo wa kujibu."

Hivyo hatuwezi kuwaita waliokufa kuwa ni watu ambao hawako tena na kuwa si chochote, bali wao, iwe ni katika wale waliofanya mema au katika makafiri waliokana na kupinga dini, wako hai katika ulimwengu wa Barzakh ambapo wanapata malipo ya matendo yao. Wakiwa huko wanapata kushuhudia hakika ya matendo yao yawe ni mazuri au mabaya, na kuona kwa karibu hakika ya mambo ambayo walighafilika nayo walipokuwa humu duniani kabla ya kufa kwao. Kwa maelezo hayo na kwa msingi wa mafundisho ya Uislamu, wafu hutambua na kudiriki vyema zaidi hakika ya mambo ya ulimwengu kuliko wanavyoyajua wengi wa watu ambao wangali wanaishi maisha ya kimaada humu duniani.

Ni kwa msingi huo ndipo mwanzuoni wa madhehebu ya Shafi, Imam Ghazali, akaamini kuwa wale wanaodai kuwa mauti ni kitu kitupu na kisichokuwepo ni watu wasio na dini na wanaopinga uwepo wa Mwenyezi Mungu na Akhera. Kama wangekuwa wanaamini ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa kuna maisha baada ya mauti, kamwe hawangepinga wala kudai kuwa kifo ni sawa na mwisho wa kila jambo na maisha.

Vilevile Imam Nawawi, ambaye ni mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shafi wa nchini Syria anawausia Waislamu katika kitabu chake kwamba wanaposimama pembeni ya makaburi ya Manabii na hasa Mtume Mtukufu (saw) ni mustahabu, yaani ni jambo linalopendekezwa, kwamba wawaombe watukufu waliozikwa kwenye makaburi hayo, wawaombee wao dua mbele ya Mwenyezi Mungu ili apate kujibu maombi na kuwatekelezea haja zao kwa sababu wako hai mbele ya Muumba wao.

**********

Ibn Taymiyya na Ibn Abdul Wahhab wanasema kuwa masahaba walikuwa wakiomba kukidhiwa haja kutoka kwa Mtume (saw) alipokuwa hai lakini kwamba hawakufanya hivyo kando ya kaburi lake alipoaga dunia bali hata kwamba walikuwa wakiwazuia watu kusimama pembeni ya kaburi lake kwa makusudio ya kuomba dua. Kwa hakika haijulikana waasisi hao wa Uwahabi walitegemea msingi gani kuthibitisha madai yao hayo kwa sababu wanazuoni wa kuaminika na wapokezi mashuhuri wa hadithi kama vile Abulfadhl Baihaqi, Ibn Abi Shaiba na Ahmad Zayni Dahlani wamenukuu hadithi nyingi sana zinazothibitisha kuwa masahaba wa Mtume (saw) walikuwa wakitawasali naye hata baada ya mtukufu huyo kuaga dunia.

Kwa mfano wananukuu Hadithi inayosema kuwa wakati wa ukhalifa wa Omar, watu walikumbwa na baa la njaa. Bilal bin Harith alienda pembeni ya kaburi la Mtume (saw) na kuomba: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Uombee umma wako mvua kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu watu wote wanakaribia kuhiliki. Hapo Mtume (saw) alimdhihirikia ndotoni akimwambia kwamba mvua itanyesha. Vile vile katika zama za ukhalifa wa Othman masikini mmoja alimwendea na kumuomba haja fulani. Othman alimwambia: Nenda ukatie udhu kisha uswali msikitini na useme baada ya kuswali: Ewe Mwenyezi Mungu! Ninakuelekea Wewe kupitia Mtume wetu Muhammad (saw) ambaye ni Mtume wa rehema. Ewe Muhammad! Ninamuelekea Mwenyezi Mungu kupitia kwako na ninakuomba uweze kunitimizia haja yangu. Mtu huyo alimfanya Mtume (saw) kuwa mwombezi wake naye akatimiziwa haja yake."

Kuna Riwaya nyingine ambayo inasema kwamba Mtume Mtukufu (saw) alitawasali na mitume wengine waliokuja kabla yake. Imenukuliwa kuwa Fatwimah bint Asad, mama yake Imam Ali (as) na ambaye alikuwa mama ya Mtume (as) baada ya mtukufu huyo kuondokewa na mama yake mzazi Amina (sa), Mtume aliomba dua ifuatayo wakati wa maziko yake: "Eeh Mwenyezi Mungu! Kwa baraka za Mtume wako na baraka za Mitume waliokuja kabla yangu! Msamehe mama yangu Fatwimah bint Asad na papanue mahala pake."

Kwa msingi wa yale yote ambayo tumeyazungumzia hadi sasa, tawassul yaani kuwatumia Mitume na Maimamu watoharifu (as) kama njia ya kutimiziwa haja haraka na Mwenyezi Mungu kutokana na utukufu mkubwa walionao mbele Yake, ni jambo linaloambatana kikamilifu na sira pamoja na mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw) ambapo masahaba pia walilifanya, kinyume na madai yasiyo na msingi yanayotolewa na Mawahabi, na wala hawakulikataza jambo hilo.

***********

Inawezekanaje kuwa Tawassul na Maimamu pamoja na Mtume Mtukufu (saw) ni jambo linalokemewa na kukatazwa katika hali ambayo hata kabla ya kuzaliwa watukufu hao Mwenyezi Mungu aliwazingatia na kuwaenzi mno kiasi kwamba Manabii na Mitume wengine walikuwa wakitawasali nao kwa ajili ya kumkurubia Mwenyezi Mungu. Tunathibitisha jambo hilo kwa Aya ya 37 ya Surat al-Baqarah ambayo inasema: Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake akakubali toba yake. Hakika Yeye ni Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.

Tukiachilia mbali mtazamo na tafsiri za wanazuoni wa Kishia kuhusu Aya hiyo, wanazuoni wengi mashuhuri wa Kisunni wanaamini kuwa maneno aliyopokea Nabii Adam (as) na kupelekea kukubaliwa toba yake ni majina matano ya watukufu wa Aal Kisaa (as). Jalal Deen Suyuti, mmoja wa wafasiri mashuhuri wa Ahlu Sunna anasema katika sehemu ya tafsiri ya Aya hiyo kwamba: Ibn Najjar ananukuu Hadithi kutoka kwa Ibn Abbas akisema kwamba alipomuuliza Mtume Mtukufu (saw) maana na hakika ya maneno hayo alimjibu kwa kusema: "Nabii Adam (as) alipoomba toba, Mwenyezi Mungu alimuapisha kwa hakika ya Muhammad, Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as) na ndipo akakubali toba yake."

Vile vile Mwenyezi Mungu anazungumzia katika Aya kadhaa za Surat al-Qamar kisa cha kaumu ya Nuh na adhabu aliyowateremshia na kisha kusema: Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na misumari.

Mtume Mtukufu (saw) anasema ifuatavyo kuhusu Aya hii: "Katika Aya hii makusudio ya neno 'alwaah' ni mbao za safina na makusudio ya 'dusur' ni sisi (watu watano wa Aal Kisaa). Kama tusingelikuwa ni sisi, safina haingelikwenda (haingelitembea/haingelipata mwendo) juu ya maji. Ukweli huo pia umethibitishwa na machimbo ya kale kihistoria. Kuna mabaki ya safina kubwa yaliyogunduliwa katika milima ya Ararat, safina ambayo ni sawa na manowari ya vita ambapo vyuma vingi vilitumika katika utengenezaji wake. Wataalamu wa mambo ya kale walipata pembeni ya safina hiyo ya kushangaza, mabaki ya kitu (loho) ambacho juu yake kulikuwa na maandishi ambayo, licha ya kupita maelfu ya miaka, lakini bado yalikuwa yanaweza kusomeka vizuri. Wataalamu wa hati na lugha kutoka Russia na China waliweza kutarjumu hati na maandishi hayo na kupta matokeo ya kuvutia na kushangaza sana. Maandishi yaliyokuwa kwenye loho hiyo ya kale yalisema: Ewe Mungu wangu! na Ewe Msaidizi wangu! Tusaidie kwa rehema na baraka zako! Na kwa jaha ya roho hizi takatifu: Muhammad, (Ilyaa) Ali (Shabar) Hassan, (Shubair) Hussein na Fatwimah, wao ambao ni wakubwa na watukufu na ambao ulimwengu umesimama kutokana na baraka zao. Tusaidie kwa heshima ya majina yao! Ni Wewe tu ndiye unayeweza kutuongoza kwenye njia nyoofu."

 

Loho iliyogunduliwa pembeni ya safina ya kale inayonasibishwa kwa Nabii Nuh (as)

Baada ya kuona ushahidi wote huu, je kunabakia hoja yoyote ya kudai kuwa tawassul ni bida' na kwamba wale wanaofuata sunna na mafundisho haya ya Uislamu ni makafiri na washirikina?!

Huenda madai hayo yasiyo na msingi yakawa yanatokana na itikadi na imani zisizo na msingi katika Uislamu na huenda walio na imani hizo potofu wakawa wanafuatilia malengo mengine ya siri.