Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (61)
Ahlan Wasahlan wapenzi wasikilizaji wa Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilimalizia kumzungumzia Mulla Muhammad Ali Kani, alimu na mwanazuoni mkubwa na mwanamapambano aliyeishi mwishoni mwa karne ya 13 na mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria ambaye kama tulivyosema alikuwa na taathira kubwa mno katika matukio ya kisiasa na kiutamaduni ya Iran. Sehemu ya 61 ya mfululizo huu juma hili itatupia jicho historia na maisha ya Mirza Shirazi mmoja wa wanazuoni na wanamapambano wakubwa na mashuhuri katika ulimwengu wa Kishia na katika historia ya mapambano ya Iran. Jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Ilikuwa katikati ya Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1230 Hijria wakati katika nyumba ya mmoja wa masharifu na watu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na aliyekuwa mmoja wa Maulamaa wa watajika wa Shiraz Iran, alipozaliwa mtoto wa kiume ambaye alipewa jina la Muhammad Hassan. Mtoto huyu yaani Sayyid Muhammad Hassan alimpoteza baba yake akiwa na umri wa miaka mitatu tu ambaye aliaga dunia na hivyo kuanza maisha ya uyatima. Mjombake aliyejulikana kwa jina la Majd al-Ashraf alichukua jukumu la usimamizi na malezi yake. Kutokana na kumuona ana kipaji na akili isiyo na mithili alianza kumfundisha Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kifarsi akiwa na umri wa miaka minne tu. Ilimchukua miaka miwili tu kwani mtoto huyu alifanikiwa kuhitimu masomo ya msingi ya fasihi ya lugha ya Kifarsi. Alipofikisha umri wa miaka minane tayari kijana huyu mdogo alikuwa akipanda mimbari na kutoa mawaidha.

Katika kipindi cha ujana na ubarobaro wake, Sayyid Muhammad Hassan alisoma kitabu cha sherh ya Lum'a kwa mwalimu mahiri na mtajika zaidi wa masomo ya dini katika mji wa Shiraz wakati huo. Kitabu hiki ambacho ni cha mustawa na kiwango cha juu kielimu kinahesabiwa kuwa moja ya vyanzo muhimu zaidi vya fikihi ya Kishia. Hima, bidii na kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho ni mambo ambayo yalimfanya afikie daraja ya kuwa mwalimu akiwa na umri wa miaka 15 na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza). Hata hivyo hilo halikukata kiu yake ya kutafuta elimu. Akiwa na umri wa miaka 15 Mirza Shirazi alielekea katika mji wa Isfahan. Akiwa huko alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo katika mji huo kama Sayyid Hassan Bidabadi na kufanikiwa kupata daraja ya Ijtihadi kabla ya kufikisha umri wa miaka 20. Licha ya kufikia daraja hiyo ya juu ya kielimu lakini katu hakuacha kusoma na kujisomea.
Akiwa na umri wa miaka 29, Sayyid Muhammad Hassan alifunga safari pamoja na mkewe na watoto wake na kuelekea Najaf, Iraq. Hii ni katika hali ambayo, ilikuwa imepita miaka zaidi ya 9 tangu afanikiwe kufikia daraja ya Ijtihad na wakati huo huo mwenyewe alikuwa mwalimu mahiri, lakini alikuwa akihudhuria kwa unyenyekevu kabisa vikao vya elimu na darsa za Maulamaa wakubwa kama Muhammad Hassan Najafi mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir, Hassan Kashiful-Ghitaa na Sheikh Murtadha Ansari. Ni katika vikao vya masomo vya Sheikh Murtadha Ansari ndipo alipofahamiana na Sayyid Jamalud-Din Asadabadi mwanafunzi wa masomo ya dini aliyekuwa chuki dhidi ya ukoloni na mujahidi Muafghani ambaye ni mashuhuri kwa kupigania umoja wa Kiislamu. Kufahamiana huku kulikuja kuwa na matunda mengi katika miaka iliyofuata.

Akiwa katika mji mtakatifu wa Najaf, Sayyid Muhammad Hassan aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Mirza Shirazi na baada ya muda akaondokea kuwa miongoni mwa wanafunzi mahiri na watu waliokuwa wakiambatana na Sheikh Murtadha Ansari. Mirza Shirazi hakuwa na mithili yake katika kuamiliana vyema na watu na kuzungumza nao kwa maneno matamu. Aidha alikuwa na kifua kipana chenye uwezo wa kusikiliza ya wengine kiasi kwamba, hakukuweko na mtu mfano wake. Hakuzembea hata kidogo katika kusimamisha nara na kaulimbiu za dini na kusimama kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kisheria na watu wote walikuwa wakimtambua na kumfahamu kwa sifa hii kiasi kwamba, Maulamaa wa zama zake walimpatia lakabu ya Mujadid al-Madh'hab yaani mhuishaji wa madhehebu.
Mwaka 1281Hijria, Sheikh Murtadha Ansari aliyekuwa Marjaa mutlaki wa Mashia aliaga dunia. Wanafunzi wake wakakusanyika na baada ya mashauriano waliafikiana wote kwa pamoja juu ya Mirza Shirazi kuchukua jukumu la uongozi wa Mashia. Wakiwa na lengo la kumkinaisha Mirza Shirazi akubali kuchukua jukumu hilo walijadiliana naye kwa masaa kadhaa. Hatimaye Mirza Shirazi akiwa anabubujikwa na machozi alikubali kuchukua jukumu hilo. Hivyo ndivyo Mirza Shirazi alivyoondokea kuwa baba wa Umma asiye na mpinzani, mtu ambaye alikipitisha kipindi cha utoto wake katika maisha ya uyatima. Baba ambaye alikuwa msomi, shujaa, mahiri katika uchukuaji maamuzi, asiyetereka na mwenye kuchukia dhulma. Katika kipindi chake cha uongozi, alifanikiwa kutoa huduma nyingi kwa Umma wa Kiislamu kuanzia kujenga msikiti, madrasa na soko mpaka katika kukabiliana na ada za serikali zisizofaa. Aidha alisimama kupambana na ukoloni sambamba na kufanya hima na idili kwa ajili ya kulinda na kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Waislamu.

Katika zama za Mirza Shirazi ilikuwa ada na mazoea kwamba, wakati wa kuwasili wafalme wa mataifa ya Kiislamu, Maulamaa walikuwa wakienda kuonana nao na hilo lilikkuwa likipelekea daraja na nafasi ya wafalme kupata itibari na nguvu zaidi mbele ya macho ya watu. Hata hivyo mwaka 1287 wakati Naser al-Din Shah Qajar, mfalme wa wakati huo wa Iran alipokwenda kufanya ziara katika maeneo matakatifu nchini Iraq, Mirza Shirazi alitumia wasaa na fursa hiyo kwa ajili ya kuvunja na kuondoa ada hiyo. Kinyume na ada ya huko nyuma, Mirza Shirazi hakwenda kuonana na mfalme huyo sehemu alipofikia bali alikutana naye katika Haram ya Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) mjini Najaf na alikataa kupokea zawadi kutoka kwa mtawala huyo. Kitendo hicho kiliporomosha na kusambaratisha haiba na adhama ya Naser al-Din Shah na kuonyesha kwamba, mfalme huyo haheshimiwi wala kuaminiwa na Maulamaa wa Kiislamu.
Mirza Shirazi alikuwa Marjaa wa ulimwengu wote wa Kishia katika zama hizo hivyo halikuwa jambo la ajabu kuletewa mali nyingi kutoka katika maeneo mbalimbalii ya mashariki na magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu katika kalibu ya khumsi na kadhalika. Alifanya kila hima na kwa umakini mkubwa kuhakikisha kwamba, mali hizo ambazo kimsingi ni za hazina ya dola, zinatumikka kwa mujibu wa maagizo na sheria za Kiislamu kama vile kulinda, kuhifadhi na kupanua dini sambamba na kuwasidia kimaisha Waislamu wahitaji. Mirza Shirazi alikuwa akiwasaidia kwa siri wafanyabiashara waliofilisika au watu ambao kwa namna moja au nyingine wamekumbwa na matatizo ya kifedha na kukwama kimaisha. Watu waliokuwa wakipokea misaada hiyo walikuja kumfahamu mtoaji wake baada ya kuaga dunia Mirza Shirazi na kuelewa kwamba, ni kwa namna gani alikuwa akiwafikiria na kuwajali.

Wapenzi wasikiliizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo, hata hivyo kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi kama ambavyo kumalizika muda wa kipindi hiki ndio mwanzo wa pirikapirika za maandalizi ya kipindi kijacho. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ambapo tutaendelea kumzungumzia Mirza Shirazi, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh