Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (62)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilianza kumzungumzia Sayyid Muhammad Hassan mashuhuri kwa jina la Mirza Shirazi mmoja wa wanazuoni na wanamapambano wakubwa na mashuhuri katika ulimwengu wa Kishia na katika historia ya mapambano ya Iran.
Tuliashiria kwa mukhtasaari na kutupia jicho sehemu ndogo tu ya historia ya maisha yake. Kipindi chetu cha juma hili kitaendelea na maudhui hii, tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili muweze kutegea sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Moja ya hatua muhimu ya kisiasa iliyochukuliwa na Mirza Shirazi ni fatuwa yake ya kihistoria ya kuharamisha tumbaku ambayo ilipelekea kuibuka harakati na vuguvugu kubwa la wananchi nchini Iran. Harakati ya tumbaku inahesabiwa kuwa moja ya matukio muhimu sana katika matukio ya historia ya leo ya Iran. Katika zama hizo Waingereza walifanya njama ya kuhodhi uchumi wa Iran kwa kuchukua mamlaka kamili ya uzalishaji na ununuzi wa tumbaku nchini Iran.
Mfalme wa wakati huo wa Iran, Nasser Din Shah aliazimia kumkabidhi Gerald Talbot, mmoja wa washauri na watu wa karibu wa Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza ulimaji, usambazaji na uuzaji wa tumbaku ya Iran. Mkataba huo ulikuwa wa miaka hamsini. Hii ni katika hali ambayo, katika zama hizo tumbaku ilikuwa moja ya bidhaa muhimu kabisa za kilimo nchini Iran na mkataba huo ungehatarisha uchumi wa Iran pamoja na maisha ya akthari ya Wairani.
Wananchi wa miji ya Shiraz, Isfahan, Tabriz na Tehran wakiongozwa na viongozi wa dini, walijitokeza na kupinga vikali mkataba huo. Utawala wa kifalme wa wakati huo ukitumia mkono wa chuma ulikandamiza maandamano na upinzani wa wananchi na kuwatia mbaroni na kisha kuwabaidisha viongozi wote wa harakati hiyo ya wananchi.
Sayyid Ali Akbar Fal Asiri aliyekuwa kiongozi wa harakati ya wananchi mjini Shirazi alibaidishiwa Basra Iraq. Hata hivyo aliendelea na malengo yake kwani akiwa katika mji huo alikutana na Jamaluddin Asadabadi na akamtaka mwanafunzi huyo mwanapambano na mwenye chuki dhidi ya ukoloni amuandikie barua Mirza Shirazi na ambainishie kile ambacho kinawakabili wananchi wa Iran. Sayyid Jamaluddin Asadabadi ambaye hapo aliwahi kusoma pamoja na Mirza Shirazi na alikuwa akimtambua vyema, alimuandikia barua na ndani yake sanjari na kubainisha matukio ya Iran alimtaka aingilie kati na kuhitimisha kile kinachojri huko Iran.
Hatimaye tarehe Mosi Mfunguo tatu Dhul-Hija 1308 Hijria, Naser al-Din Shah alipokea telegrafu kutoka kwa Mirza Shirazi ambayo ilisisitiza kwamba, mkataba huo wa Tumbaku unakinzana na Qur'ani na fauka ya hayo utapelekea kusambaratika uhuru na mamlaka ya serikali ya kujiamulia mambo na kupotea nidhamu ya mamlaka.
Naser al-Din Shah Qajar ambaye alikuwa akifahamu vyema ushawishi wa maneno ya Mirza Shirazi kwa jamii pamoja na nafasi yake ya kijamii na kidini, alimtaka mwakilishi wa Iran mjini Baghdad ambainishie Mirza Shirazi kuhusiana na mkataba huo ili amkinaishe. Hata hivyo Mirza Shirazi hakukinaika na yale aliyoelezwa na akaonya kwamba, kama serikali haiwezi kufanya hilo basi yeye atachukua jukumu hilo.
Naser al-Din Shah na baraza lake la mawaziri walikuwa wakidhani kwamba, Mirza Shirazi ni mujtahidi kama Mamujitahidi wengine na hivyo walikuwa wakiamini kwamba, vitisho vyake vitaishia katika maneno tu na hakuna wakati ambao vitafikia katika hatua ya vitendo.
Hatimaye mwaka 1308 Hijria, Mirza Shirazi alitoa fatuwa ya kuharamisha matumizi ya tumbaku kwa namna yoyote ile.
Mirza Shirazi alisema katika fautwa yake hiyo:
Bismillahi Rahman Rahim
"Hii leo kutumia tumbaku kwa namna yoyote ile ni sawa na kupigana na Imam wa Zama (atfs).
Kufuatia fatuwa hiyo ambayo maneno yake hayakuwa yakizidi hata mstari mmoja, wananchi wote Waislamu wa Iran, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, wasomi, wafanyabiashara, wananchi wa kawaida na hata wasiokuwa Waislamu waliitii fatwa hiyo kwa kutotumia tumbaku kwa njia yoyote ile na hivyo wakawa wamesimama dhidi ya mkoloni Muingereza na kuanzisha harakati ya pamoja dhidi ya mkataba wa tumbaku au mkataba wa Talbot.
Wananchi walijitokeza kwa wingi wakavunja na kuharibiharibu kikamilifu vifaa vya shisha, na wakulima wengi wakachoma moto bidhaa yao ya tumbaku. Harakati hiyo ikapiga hodi na kuingia ndani ya ufalme. Anis al-Dawla, mke wa mtawala Naser al-Din Shah ambaye katika zama hizo alikuwa kama ndio malkia wa Iran alitoa amri ya kukusanywa shisha zote ndani ya ikulu ya mfalme. Wakati Naser al-Din Shah Qajar alipotaka kujua sababu ya hilo, Anis al-Dawla alimjibu kwa kusema: Watu ambao jana walinihalalisha mimi kwako, ndio hao hao ambao leo wameharamisha tumbaku.
Kuanzia hapo hata Shah Qajar mwenyewe hakuwa akithubutu kuwataka wafanyakazi wake wamletee shisha, kwani alikuwa akifahamu kuwa, ombi lake hilo halitatekelezwa.
Baada ya fatuwa hiyo ya kihistora na iliyokuwa na taathira kubwa, Shah na baaraza lake la mawaziri walifanya juhudi kubwa ili kuwakinaisha Maulamaa wa Tehran na wa miji mingine ili wawe pamoja nao, lakini hakuna aliyekuwa tayari kupingana na fatuwa ya Mirza Shirazi. Hatimaye baada ya siku 50 tangu kutiwa saini mkataba huo wa tumbaku ambao ulikuwa ukimpa mamlaka Gerald Talbot ya kuhodhi kikamilifu sekta hiyo, ulivunjwa na kwa mara nyingine tena mikono ya ukoloni kwa utajiri wa Iran ikawa imekatwa. Hivi ndivyo, Mirza Shirazi aliyekuwa akiishi maisha ya kawaida kabisa huko Samarra Iraq, alivyofanikiwa kuushinda utawala wa Naser al-Din Shah Qajar kwa andiko la sentensi moja.
Historia inaeleza kuwa, Mirza Shirazi alilia sana baada ya kufutwa mkataba huo wa tumbaku na alipoulizwa sababu ya hilo alisema: Kilio, ghamu na huzuni yangu inatokana na kuwa, maadui wa Uislamu kuanzia leo wamefahamu nguvu ya Uislamu iko wapi na kuanzia leo wataanza kuandaa mbinu na mikakati ya kuishinda.
Hatimaye Mirza Shirazi, alimu, Marjaa mkubwaa na mwanazuoni mahiri wa Kiislamu aliaga dunia huko Samarra Iraq 24 Shaaban 1312 Hijria akiwa na umri wa miaka 82 na kuacha nyuma historia yake iliyojaa ibra, mafunzo, hima, idili, kusimama kidete na kupigania Uislamu. Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.