Jumatano, 18 Januari, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 25 Mfunguo Tisa Jamadithani 1444 Hijria, sawa na tarehe 18 Janauri 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 334 iliyopita alizaliwa mwandishi na mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa, Charles de Montesquieu. Alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. Kitabu maarufu zaidi cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva. Katika kitabu hicho alichunguza aina mbalimbali za serikali zilizojitokeza katika kipindi chote cha historia, ada na sheria za kimaumbile, sheria za kibinadamu na uhusiano baina yao. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni "Persian Letters" (Barua za Kiiran). Alifariki dunia mwaka 1755. ***
Miaka 135 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya Mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatuwa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. ***
Tarehe 18 Januari miaka 108 iliyopita 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Lengo kuu la mkataba huo lilikuwa ni suala la kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean. ***
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa. ***
Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 25 Jamadithani alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu, akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na kujifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa hususan Ayatullahil Udhma Hairi. Ayatullah Muhammad Ali Araki alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum kwa kipindi cha miaka 35 na kulea wanazuoni na wasomi hodari. Mwanazoni huyo mkubwa wa Kiislamu amezikwa katika Haram tukufu ya Maasuma (as) katika mji mtakatifu wa Qum. ***