Jan 25, 2023 15:27 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia katika Uislamu (63)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Katika vipindi vyetu viwili vilivyotangulia tulimzungumzia Mirza Shirazi au Mirza Bozorg, mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa Kishia. Tuliona ni kwa namna gani alimu na msomi huyo aliyekuwa akiishi maisha ya kawaida kabisa alivyofanikiwa kuushinda utawala wa Naser al-Din Shah pamoja na mkoloni Muingereza kwa fatuwa yake ya kuharamisha tumbaku ambayo haikuzidi hata mstari mmoja. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 63 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Ali Akbar Fal Asiri, alimu na mwanazuoni mwengine mahiri na mashuhuri wa Kishia ambaye mchango wake una nafasi muhimu mno katika ulimwengu wa Kiislamu. Kuweni pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki ili kutegea sikio yale niliyoakuandalieni kwa leo. Karibuni.

 

Sayyid Ali Akbar Fal Asiri alizaliwa 1256 Hijria katika kijiji cha Asiri kilichoko katika viunga vya mji wa Lamerd. Alipofikisha umri wa miaka 14 taytari alikuwa amemaliza masomo yake ya msingi. Mwaka 1270 Fal Asiri alifunga safari na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Shiraz akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu na kukamilisha maaarifa yake ya dini. Akiwa mjini Shiraz alisoma kwa Sheikh Mahdi Gajouri. Baada ya kufikia daraja ya Ijtihadi alielekea katika mji wa Najaf Iraq kwa minajili ya kupanua zaidi upeo na maarifa yake ya elimu. Akiwa katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf al-Ashraf alisoma masomo yake ya dini kwa Mirza Habibullah Rashti na kisha akaondokea kuwa Mujtahidi mahiri na fakihi mwenye utambuzi wa hali ya juu kuhusiana na masuala ya kijamii na matukio ya kisiasa katika zama zake.

Shaksia wakubwa wa Shiraz Iran na wananchi wa kawaida waliokuwa wakienda kufanya ziyara Najaf al-Ashraf mara kadhaa walimtaka arejee katika mji wa Shiraz ili akawape muongozo watu na kuwafanya wanufaike na elimu na maarifa yake katika masuala mbalimbali sambamba na kuleta ufahamu na welewa miongoni mwao kuhusiana na masuala ya kisiasa na kijamii. Hata hivyo Ayatullah Fal Asir alikuwa akikataa ombi lao hilo, kwani alikuwa ameazimia kubakia milele katika mji wa Najaf na kuishi kando ya Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Hata hivyo, matarajio na matumaini yake ya kuishi milele katika mji wa Najaf hayakutumia kwani alilazimika kukubali ombi la wananchi wa Shiraz baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mwalimu wake yaani Habibullah Rashti na takribani 1277 Hijria akarejea Shiraz. Alianza kujishughulisha na kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) katika mji wa Shiraz sambamba na kuswalisha Swala ya Jamaa katika msikiti wa Jamia uliokuwa ukijulikana kwa jina la Masjid Wakil Shiraz.

Ayatullah Habibullah Rashti

 

Ni katika miaka hiyo hiyo ya awali ya kuwasili kwake huko Shiraz ambapo upenyaji wa Waingereza katika mji huo ulichukua wigo mpana na wananchi siku baada ya siku wakawa wakihisi uwepo mkubwa wa ukoloni katika mji wao. Ayatullah Fal Asiri hakuwa akiweza kuvumilia hali hiyo na kila siku alikuwa akionyesha upinzani wake dhidi ya jambo hilo kwa namna hii au nyingine. Yeye pia kama walivyokuwa Marajii wengine na Maulamaa wa Kiislamu alikuwa akipinga suala la maajinabi kuwa na udhibiti katika ardhi za Kiislamu na alikuwa akilipinga hilo kwa nguvu zake zote.

 

Siku moja Ayatullah Fal Asiri alikuwa akielekea msikitini kwa ajili ya Swala na kusoma Ziyarat Ashura, akamuona mtu Bwana mmoja amevaa nguo za Kimagharibi na anapita katika njia ya watembea kwa miguu kwa jeuri na maringo huku akiwa amepanda farasi. Ayatullah Fal Asiri akawauliza watu aliokuwa ameandamana nao, ni nani mtu yule. Akaambiwa ni balozi mdogo wa Uingereza. Ayatullah Fal Asiri akafunga njia na kumzuia balozi huyo mdogo wa Uingereza na kisha akamtaka ateremke kutoka katika farasi wake na atembee kwa miguu na kila anapomuona Mwislamu amsalimie.

Mwaka 1303 Hijria, tamaa na kutaka makuu mtawala mpya wa Fars na kuhodhi na kulimbikiza ngano na nafaka kulikofanywa na watu wake wa karibu kulipelekea bei ya mkate kupanda mara kadhaa. Mbali na bei ghali na kufichwa ngano, mkate ukageuka kuwa bidhaa adimu miongoni mwa watu na katika akthari ya nyusiku watu masikini walikuwa wakilala bila ya kupata kitu cha kutia kinywani. Ili kulalamikia hali hiyo, watu wapatao 6,000 walikusanyika katika msikiti wa Wakil. Ayatullah Sayyid Ali Akbar Fal Asiri naye alikuwa pamoja na wananchi katika malalamiko yao hayo na akatuma telegrafu Tehran yalipokuwa makao makuu ya utawala. Akiwawakilisha wananchi, mwanazuoni huyo alitaka kuuzuliwa mtawala na kushughulikiwa hali mbaya ya maisha iliyokuwa ikitawala katika mji wa Shiraz.

Msikiti wa Wakil katika mji wa Shiraz

 

Naser al-Din Shah mfalme wa wakati huo wa Iran badala ya kusikiliza kilio cha wananchi na kushughulikia malalamiko yao alikata shauri kutumia mkono wa chuma dhidi yao. Akampatia jukumu hilo Zelle-e Soltan aliyekuwa mtawala wa Isfahan. Maulamaa wa Isfahan ambao walikuwa na taarifa ya uamuzi huo wa Shah wakiwa na lengo la kuwaunga mkono wananchi wa Shiraz na kuzuia kutokea machafuko, walimkinaisha Zelle-e Soltan ashughulikie tatizo la ughali wa mkate huko Shiraz na badala yake wananchi wahitimishe mkusanyiko na wasitake tena kuuzuliwa mtawala.

Habari hiyo ikamfikia Ayatullah Fal Asir. Mwanazuoni huyo ambaye alikuwa akihofia roho na uhai wa watu, aliwataka watu warejee makwao na kuhitimisha mkusanyiko huo. Wananchi wa Shiraz wakasalimika na baa la kuadimika mkate na kuuzwa kwa bei ya kulanguliwa, na Ayatullah Fal Asiri akabaidishiwa katika mji wa Isafahan. Kutokana na mtawala Zelle-e Soltan kuhofia kuibuka tena uasi wa wananchi wa Shiraz kama atambaidisha mwanazuoni huyo, alitumia ujanja na hila ambapo alilifanya hilo kwa sura ya heshima ya dhahiri. Alimuita kwa heshima na taadhima Ayatullah Fal Asiri huko Isfahan na baadaye akamlazimisha abakie katika mji huo na hatimaye baada ya miaka mingi, mwanazuoni huyo akafanikiwa kurejea tena katika mji wa Shiraz.

 

Katika tukio la mkataba wa kukabidhiwa shirika moja la Uingereza mamlaka ya kuhodhi sekta ya tumbaku, mwanazuoni huyu alikuwa miongoni mwa watu wa awali waliopaza sauti kupinga mkataba huo. Harakati zake za upinzani dhidi ya mkataba huo na kuwashajiisha wananchi wa Shiraz, zilimfanya mtawala wa mji huo atoe amri ya kubaidishiwa Bushehr moja ya miji ya Iran. Hata hivyo maafisa wa utawala hakuwa na uthubutu wa kumtia mbaroni Ayatullah Fal Asiri katikati ya mji au nyumbani kwake. Hivyo walisubiri akiwa ametoka nje ya mji ambapo walimshambulia na kumtia mbaroni na kisha kumvua mavazi yake ya kidini na kisha kumhamishia katika mji wa Bushehr.

Ayatullah Ali Akbar Fal Asiri

 

Alishikiliwa kwa muda katika mji huo ambapo hakuna mtu aliyeruhusiwa kuonana naye. Sayyid Ali Akbar Fal Asiri aliyekuwa kiongozi wa harakati ya wananchi mjini Shiraz alibaidishiwa Basra Iraq. Hata hivyo aliendelea na malengo yake kwani akiwa katika mji huo alikutana na Jamaluddin Asadabadi na akamtaka mwanafunzi huyo mwanapambano na mwenye chuki dhidi ya ukoloni amuandikie barua Mirza Shirazi na ambainishie kile ambacho kinawakabili wananchi wa Iran. Sayyid Jamaluddin Asadabadi ambaye hapo aliwahi kusoma pamoja na Mirza Shirazi na alikuwa akimtambua vyema, alimuandikia barua na ndani yake sanjari na kubainisha matukio ya Iran alimtaka aingilie kati na kuhitimisha kile kinachojri huko Iran. Hatimaye baada ya miaka 63 ya jihadi, harakati na hima mtawalia, Ayatullah Sayyid Ali Akbar Fal Asir aliaga dunia mwezi Rabiul-Awwal 1319 Hijria katika mji wa Shiraz.

Kaburi la Ayatullah Ali Akbar Fal Asiri

 

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena wiki ijayo, katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh