Feb 12, 2023 08:06 UTC
  • Mafanikio ya kisayansi ya Iran baada ya mapinduzi ya Kiislamu (1)

Katika makala hii maalum, tutaangazia maendeleo na nafasi ya kisayansi ya Iran katika eneo na dunia kwa ujumla, na katika vipindi vijavyo tutaangazia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja kama vile teknolojia za nano, anga, tiba, seli shina na nyuklia.

Moja ya fakhari za Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuzidi kukua na kuwepo harakati za kiwango cha juu katika nyuga za kisayansi jambo ambalo limethibitishwa mara nyingi na duru za kimataifa. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, sekta ya viwanda Iran ilikuwa tegemezi kwa madola ya kigeni kwa kiwango kikubwa sana na kwa sababu hiyo, viwanda vya nchi vilipata mdororo mkubwa. Idadi kubwa ya bidhaa za kimsingi zilikuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi. Hata hivyo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, hali ilibadilika na viwanda vikaanza kunawiri.

Tukiangazia ustawi wa Iran katika nyuga mbalimbali za kiviwanda, kijeshi na kisayansi pia inatubainikia wazi kwamba mashinikizo ya pande zote za kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya maadui yameshindwa kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu. Kufikiwa kwa teknolojia ya hali ya juu katika nyanja za nano, anga, tiba, seli shina na nyuklia ni miongoni mwa mifano ya maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya Iran, ambayo yote yamefikiwa chini ya vikwazo.

Kasi ya juu ya maendeleo ya kisayansi

Katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nafasi ya Iran katika uzalishaji wa sayansi ya dunia imeongezeka mara 180 zaidi. Utayarishaji wa makala za watafiti wa Iran katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi pia ulishuhudia ukuaji wa mara 55. Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na tovuti ya kimataifa ya "Web of Science": Iran inashika nafasi ya pili kati ya nchi 25 bora duniani zenye kiwango cha ukuaji wa kisayansi cha asilimia 10.4 mwaka 2019. Pia, kwa mujibu wa ripoti ya majarida mawili ya kisayansi yanayoheshimika, New Scientist na Metrix Science, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishika nafasi ya kwanza katika ukuaji wa kisayansi kati ya 1980-2009, ikiwa na kasi ya ukuaji mara 11 ya wastani wa dunia. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa Iran inakwenda kwa kasi zaidi kuliko nchi nyingi duniani katika mwelekeo wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kasi hii ni kiasi kwamba nafasi ya Iran ya uzalishaji wa sayansi ulimwenguni ilitoka asilimia 0.07 mwaka 1998 hadi asilimia 2 mnamo 2020. Hii ina maana kwamba sehemu ya Iran katika uzalishaji wa sayansi duniani imeongezeka zaidi ya maradufu ikilinganishwa na idadi ya watu nchini.

Pia, kwa mujibu wa matokeo yaliyochapishwa na hifadhidata ya "SCimago", kwa mtazamo wa idadi ya nyaraka za kisayansi zilizosajiliwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 1996 iliorodheshwa ya 54 duniani ikiwa na nyaraka 850, lakini mwaka 2020, idadi hii  iliongezeka hadi 74,440.

Miongo minne ya ongezeko la wasomi wa ngazi za juu

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), katikati ya miaka ya 1950, kiwango cha kusoma na kuandika nchini Iran kilikuwa karibu asilimia 30, lakini kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika nchini ilifika karibu asilimia 90 mwaka 2016. Hii ina maana kwamba Iran ilibadilika kutoka nchi isiyojua kusoma na kuandika mwishoni mwa enzi ya ufalme wa kiimla wa Shah na kuwa nchi inayojua kusoma na kuandika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Muda mfupi kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979,kulikuwa na vituo viwili vya mafunzo ya vipaji mahiri nchini, na idadi hii ilifikia vituo 670 mwaka 2012. Kwa upande mwingine, mnamo 1977, kulikuwa na wanafunzi wa vyuo vikuu 170,000 na sasa idadi hiyo ni zaidi ya milioni nne na laki tatu.

Kustawishwa vyuo vikuu na vituo vya wenye vipaji maalumu ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo kutokana na hayo Iran sasa inaongoza katika nyanja nyingi za kisayansi hususan miongoni mwa nchi za eneo hili la Asia Magharibi. Kwa hakika, katika uwanja wa sayansi ya kisasa, wanasayansi wa Iran wameweza kusonga mbele hadi kwenye mipaka mipya ya maarifa ya mwanadamu. Wasomi na wanasayansi wa Iran wamefanya maendeleo na utafiti wao hadi kufikia kiwango ambapo watafiti wengi duniani wanawataja na wako tayari kuungana na Wairani katika miradi ya pamoja ya utafiti. Kabla ya mapinduzi, Iran haikuwa na wanasayansi mashuhuri duniani, lakini mwaka 2016 (2016) kwa mujibu wa mtandao wa kimataifa wa Web of Science, Iran ina zaidi ya wanasayansi 200 ambao ni miongoni mwa wanasayansi bora duniani.

Kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye daima anasisitiza juu ya ulazima wa maendeleo ya kisayansi ya nchi anasema: "Kwa hakika hatukuwa na kitu cha kujivunia katika masuala ya kisayansi. Zamani pengine mwanasayansi angepata mafanikio kama mtu binafsi lakini vyuo vikuu kama taasisi havikuwa na mafanikio makubwa ya kisayansi. Lakini leo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, tumeweza kuchukua hatua na kupata mafanikio makubwa ya kisayansi katika vyuo vikuu na mafanikio hayo yameweza kufikiwa na wahadhiri na pia wanafunzi wenye vipaji.

Jarida la  The Times Higher Education World University Rankings huchapisha orodha ya kila mwaka ya vyuo vikuu bora zaidi duniani. Katika ripoti yake ya mwaka 2021, chapisho hilo liliorodhesha vyuo vikuu 47 vya Iran kati ya vyuo vikuu bora duniani, ambapo idadi hiyo iliongezeka kwa vyuo vikuu 7 ikilinganishwa na mwaka 2020. Iran imepata maendeleo makubwa katika nyanja ya kitaaluma kwa kuorodhesha vyuo vikuu 47 vya Iran kati ya vyuo vikuu 1,527 vya juu katika nchi 93 katika orodha ya 2021. Pia, kwa mujibu wa orodha ya Viwango vya Vyuo Vikuu vya Dunia vya Shanghai (ARWU) mwaka 2020, Iran inashika nafasi ya kwanza kwa idadi ya vyuo vikuu katika eneo hili na miongoni mwa nchi za Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran haikuwa na vyuo vikuu zaidi ya 20.

Kuongezeka kwa makala zilizotajwa sana za Iran

Moja ya vigezo vya kupima ubora wa makala duniani ni faharasa iliyowekwa na hifadhidata ya kisayansi "Clarivate Analytics" au ISI. Mnamo 2007, kulingana na faharisi hii, makala 56 za juu zaidi za ulimwengu zilikuwa za Iran, lakini mnamo 2019, idadi hii ilifikia nakala 473; ambapo imeongezeka karibu mara nane.

Kadhalika, daraja la Iran katika uwanja huu limeongezeka kutoka 38 mwaka 2011 hadi 17 mwaka 2019, jambo ambalo linaonyesha ukuaji wa ubora wa makala za Iran katika orodha ya makala zilizotajwa zaidi duniani.

Mchakato wa maendeleo ya kisayansi nchini Iran katika miongo minne iliyopita umekuwa kiasi kwamba baadhi ya duru za Magharibi zimetoa hata mapendekezo ya kuzuia kuendelea kwa mchakato huu. Kwa mfano, mwaka 2005, jarida maarufu la Nature lilichapisha makala yenye kichwa kinachosema "The Great Parade of Iranians" na ndani yake ilipendekeza kuzuia maendeleo ya kisayansi ya Iran kwa kuwekewa vikwazo au kuvuruga sekta ya elimu ya juu. Katika makala hii, kwa kurejelea maendeleo ya Iran, imeelezwa kuwa: “Ubora wa kisayansi nchini Iran unajengwa upya isipokuwa usitishwe na misukosuko au vikwazo vingine... na Wairani wanajijua wao ni kina nani na wanafahamu vyema ustaarabu wao na historia yao ya kisayansi. " Katika miaka michache iliyopita, nchi hii imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sayansi, hata Ayatollah Khamenei, ambaye anaiongoza Iran kwa busara na hekima amezungumzia mara kadhaa sekta ya sayansi na kuitaka nchi  "kujiamini katika nyanja zote za kisayansi."

Katika sehemu maalum zijazo za mpango wa mafanikio ya kisayansi wa Iran, tutapitia maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu katika nyanja za nano, nyuklia, anga, tiba na seli shina.