Mar 02, 2023 10:46 UTC
  •  Mafanikio ya kisayansi ya Iran baada ya mapinduzi (3)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza makala hii maalumu. Miongoni mwa mifano mingine ya maendeleo ya kisayansi yaliyopatikana nchini Iran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, ni katika nyanja ya nano, tiba na sayansi zinazohusiana nayo, zikiwemo seli shina.

Tathmini kuhusu maendeleo ya kimatibabu nchini Iran inaonyesha kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 ulikuwa na nafasi kubwa katika maendeleo ya pande zote ya Iran katika kategoria mbalimbali za sayansi ya matibabu. Kulinganisha Iran kabla na baada ya mapinduzi katika uwanja wa masuala ya matibabu na kueleza mabadiliko makubwa na ya kimsingi na maendeleo makubwa yaliyotokea katika uwanja huu katika miaka 44 iliyopita kunaweza kufichua mambo muhimu ya maendeleo hayo. Kwa hakika, moja ya sekta mbazo zimeshuhudia mabadiliko makubwa sana ni za  afya.
Kuongeza umri wa kuishi watu, kupanua mitandao na miundombinu ya mfumo wa afya, kupunguza vifo vya akina mama na watoto, kuongeza idadi ya madaktari,  kuongeza vyuo vikuu vya sayansi ya tiba nchini, kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya na matibabu, maendeleo ya dawa na ugunduzi na uzalishaji wa dawa mpya, maendeleo katika uwanja wa utaalamu wa upasuaji na kuvumbua mbinu mpya za matibabu, kutokomeza baadhi ya magonjwa na uzingatiaji maalumu kwa uhandisi wa matibabu ni miongoni mwa maendeleo ya nchi hii katika nyanja ya afya ya umma baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Pia, elimu ya matibabu nchini Iran imepata maendeleo makubwa, hasa katika maeneo kama vile seli za shina, ukarabati wa jeraha la uti wa mgongo, uzalishaji wa madawa ya magonjwa maalum na sasa Iran ni kati ya nchi zilizo mstari wa kwanza katika sekta hizo.

Maendeleo ya taasisi za matibabu na hospitali

Mnamo 1978, kulikuwa na taasisi za matibabu 558 zilizo na vitanda 57,927 nchini, ambayo ilikuwa takwimu isiyofaa kulingana na idadi ya watu nchini. Wakati huo huo, katika muongo wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu, huduma ya afya ya msingi (PHC) imehusishwa na uboreshaji wa huduma  katika kiwango cha asilimia 100 kwa wakazi wa mijini na zaidi ya asilimia 94 kwa wakazi wa vijijini kote nchini. Wakati huo huo, mfumo wa mtandao wa matibabu ya afya umeundwa kama mfano wa kimataifa ambapo kuna zaidi ya zahanati na klinikki 23,000. Wakati mnamo 1978, ni  asilimia 37 tu ya miji ya nchi ilikuwa na hospitali, takwimu hii sasa imefikia zaidi ya asilimia 94.

Kukua kwa idadi ya madaktari na wataalamu wa afya

Mnamo 1976, ikiwa na idadi ya watu milioni 33, Iran ilihitaji na ilitegemea sana madaktari wa kigeni  lakini sasa, ikiwa na idadi ya watu zaidi ya mara mbili ya wakati huo, zaidi ya madaktari elfu 80 na wataalam wanafanya kazi nchini. Hali kadhalika idadi kubwa ya wagonjwa husafiri kutoka maeneo mbali mbali duniani kupata matibabu nchini Iran na huduma zote hutolewa na madaktari wa Iran.
Kuboresha vifaa vya matibabu

Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, kulikuwa na takriban makampuni 50 ya utengenezaji wa vifaa vya tiba nchini, ambayo yote yaliagiza malighafi kutoka nje ya nchi. Makampuni hayo yalikuwa na uwezo wa kukidhi asilimia 3 tu ya mahitaji ya nchi katika uga huo. Sasa nchini Iran kuna zaidi ya makampuni 500 ambayo yanategeneza vifaa vya matibabu. Kulingana na takwimu, leo zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji ya hospitali 910 kote Iran hukidhiwa na makampuni ya ndani ya nchi.
Hivi sasa, vitengo vya utengenezaji vifaa vya matibabu nchini vinazalisha na kusambaza zaidi ya aina elfu 8 za vifaa vya matibabu katika viwango tofauti katika soko la ndani na nje.

Iran ni miongoni mwa nchi 10 bora katika uwanja wa seli shina

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uga wa utafiti wa seli shina. Iran ni kati ya nchi 10 bora duniani na katika nafasi ya kwanza katika kanda katika uga wa seli shina.

Kimsingi seli shina ni mojawapo ya nyanja mpya za afya ulimwenguni na juhudi nyingi zimefanywa kuboresha sekta hii. Sambamba na juhudi za kimataifa, wanaharakati wa mfumo ikolojia wa teknolojia na uvumbuzi nchini Iran pia wameashiria maendeleo mapya katika uwanja huu. Mnamo 2003, watafiti wa Irani walipata mafanikio ya kwanza katikak uga wa seli  shina za kwanza na mafanikio hayo yalisajiliwa katika Jumuiya ya Kimataifa ya Seli Shina. Wakati huo, Iran ilikuwa nchi ya sita kupata maarifa hayo. Kwa mujibu wa taarifa za tovuti ya kimataifa ya seli shina, Iran ni nchi ambayo pamoja na kusonga katika uwanja wa seli shina na kufikia hatua ya utafiti wa kimatibabu katika uwanja huo, imeweza pia kusajili ubunifu wake na miradi ya majaribio ya kimatibabu katika uwanja huo.
Ahmadreza Bahrami, Mkuu wa Kongamano la 3 la Kimataifa la Seli Shina na Tiba  amesema kuhusiana na hadhi ya Iran katika uga wa sayansi hii ya kisasa duniani: Iran inajulikana kuwa mji mkuu wa seli shina miongoni mwa nchi za Asia.

Aidha Iran sasa ni nchi ya tatu ambayo ina teknolojia ya kutibu ugonjwa wa leukemia kwa "tiba ya jeni."
Kwa mara ya kwanza nchini, watafiti wa Iran wamefanikiwa kutibu saratani ya damu kwa kutumia njia ya "gene therapy."

Tiba ya kwanza yenye mafanikio ya jeni nchini Iran kwa kutumia mbinu ya CAR_T Cell ilifanywa mwaka huu katika Kituo cha Matibabu cha Watoto kinachohusishwa na Chuo Kikuu cha Tehran cha Sayansi ya Tiba.

Tiba ya saratani ya seli ya T tayari ipo na hatua ya chanjo ya saratani imekuwa moja ya ugunduzi wa kufurahisha zaidi katika ugonjwa wa saratani.

Mfano maarufu ni ule wa CAR-T - dawa ya jeni iliyoundwa kushinikiza seli ya T kushambulia ama kuharibu seli za saratani mwilini

Watafiti wanasema kwamba seli aina ya T inaweza kufanikisha tiba ya saratani duniani.

Wagonjwa wa saratani ya damu ambao upandikizaji haukufanya kazi wana nafasi ya asilimia ya kupona kwa matibabu ya jeni.
Hadi sasa, ni makampuni mawili tu ya kimataifa yaliyokuwa na ukiritimba wa matibabu ya saratani kwa kutumia jeni, hivyo mafanikio ya wanasayansi wa Iran katika kutumia njia hii ya matibabu yanazingatiwa kuwa moja ya mafanikio muhimu katika uga wa tiba na kinga katika miaka ya hivi karibuni.
Maendeleo katika uwanja wa nano.

Nano ni teknolojia ya kisasa inayohusu matumizi ya vitu vidogo sana na miundo yake inapimwa kuwa kati ya nanomita 1 hadi 100. Asili ya Nano ni nanomita ambayo ni kipimo cha sehemu ya bilioni moja ya mita. Hii inamaanisha vitu ambavyo ni vikubwa kuliko atomu na vidogo mara 1000 kuliko upana wa unywele.

Teknolojia ya nano nchini Iran imestawi sana, na hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambulika duniani kama miongoni mwa nchi zilizostawi sana katika uga wa teknolojia ya nano.

Mafanikio yenye thamani katika uwanja wa nano na leza ni miongoni mwa kazi nyingine za maendeleo ya sayansi na teknolojia ya Iran katika miaka ya hivi karibuni.

Sayansi ya nano imeunda mabadiliko makubwa duniani na ina matumizi mapana katika nyanja za uzalishaji wa dawa, utambuzi wa magonjwa, uondoaji wa sumu kwenye maji na kuongeza tija katika kilimo na utakaso wa hewa.

Hivi sasa Iran inauza bidhaa zake za nano katika nchi muhimu za dunia zikiwemo za Afrika.

Tags