Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (65)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari maisha na historia ya Muhammad Hassan Ashtiyani au Mirza Ashtiyani alimu na mwanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wake katika Uislamu. Tulisema kuwa, Muhammad Hassan Ashtiyani alizaliwa 1248 Hijria katika eneo la Ashtiyan liililo jirani na mji mtakatifu wa Qom Iran. Aidha tulieleza kwamba,moja ya sifa maalumu ya Mirza Ashtiyani ni uzingatiaji wake wa hali ya juu kuhusiana na masuala ya kijami ya Waislamu. Alikuwa akiamini kuwa, kuleta mageuzi katika jamii na kushughulikia matatizo ya watu ni jukumu la alimu na msomi wa dini na hakusita kutoa gharama ya hali na mali na hata heshima katika njia hii. Sehemu ya 65 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia aalimu na mwanazuoni mwingine mahiri wa Kishia ambaye ni Mirza Muhammad Taqi Shirazi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Muhammad Taqi Shirazi alizaliwa 1256 Hijria katika mji wa Shiraz moja ya miji muhimu na mikubwa ya Iran. Hata hivyo kiasi yeye anatokana na kabila au kaumu ya Zangana katika mji wa Kermanshah moja ya kaumu za Kikurdi nchini Iran. Mirza Shirazi kama ilivyo kwa Maulamaa wengi, baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alifunga safari na kuelekea katika mji wa Najaf, Iraq na akiwa huko alishiriki darsa na masomo ya Mirza Bozorg. Wakati Mirza Bozorg alivyoelekea Samarra, Muhanmmad Taqi Shirazi pia akiwa pamoja na wanafunzi wa Mirza Bozorg alielekea katika mji huo. Kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa mdahalo na masuala mbalimbali ya kielimu aliteuliwa na Mirza Bozorg kufundisha na kuanzia wakati huo akawa na jukumu la kufundisha baadhi ya masomo.
Baada ya kuaga dunia Mirza Bozorg mnamo mwaka 1312 Hijria, jukumu la uongozi na usimamizi wa Hawza na chuo cha kidini katika mji wa Samarra sambamba na kuendeleza fikra na njia ya mwalimu huyo, likawa mikononi mwa Muhammad Taqi Shirazi na alishikilia jukumu hilo zito mpaka mwishoni mwa umri wake huku akifahamika kama alimu na msomi aliyekuwa makini. Moja ya masomo muhimu zaidi ya maktaba na njia ya Mirza Shirazi mkubwa ni mapambano dhidi ya ukoloni na udhalimu. Daima alimu na mwanazuoni huyu alikuwa akisisitiza katika kauli na vitendo vyake kwamba, kuingia na kuwa na udhibiti maajinabi na makafiri kwa ardhi na jamii za Kiislamu ni jambo lisilokubalika. Mirza wa pili pia yaani Muhammad Taqi Shirazi, ambaye alikuwa katika njia, fikra na maktaba hii alifanya hima na juhudi kubwa katika kipindi chote cha umri wake kwa ajili ya kusukuma mbele guurdumu la malengo na harakati hii. Alikuwa akiamini kwamba, lengo lake muhimu ni vita na mapambano dhidi ya uistikbari na ukoloni. Mwaka 1239 Hijria ambapo vikosi vamizi wa Russia vilifanya mauaji dhidi ya wapigania ukombozi nchini Iran, Muhammad Taqi Shirazi alitoa fatuwa ya ulazima wa kuendesha mapambano na kukabiliana na vikosi vamizi. Kwa mtazanmo wake, kudhibiti maajinabi na makafiri jamii za Kiislamu hakukuwa matokeo mengine ghairi ya kuuawa Waislamu jambo ambalo lilidhihirika na kushuhudiwa wazi katika uvamizi wa Warusi nchini Iran. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akaona ni jambo la wajibu kwa Waislamu wote kusimama na kukabiliana na wavamizi kwa njia yoyote ile na wasiruhusu dhahiri ya ukafiri kuchukua nafasi ya nara na shaari za kidini.
Mwaka 1332 Hijria iliyosadifiana na 1914 Miladia, Vita vya Kwanza vya Dunia vilianza na ni kuanzia hapo na kuendelea ambapo Umarjaa wa Mirza Taqi Shirazi ulisadifiana na hujuma na mashambulio ya wazi ya Uingereza na washirika wake dhidi ya ardhi za Kiislamu.
Katika kipindi hiki Mirza Muhammad Taqi Shirazi alifanya hima na juhudi kubwa kwa minajili ya kuleta umoja baina ya Maulamaa wa Najaf na Karbala na vilevile kuleta umoja baina ya matabaka mbalinbali ya wananchi ili kuzuia hujuma na udhibiti wa makafiri dhidi ya ardhi za Kiislamu. Akiwa na nia ya kufikia lengo lake hili alimtuma hata mwanawe katika medani ya vita. Hata hivyo baada ya miaka minne utawala wa Othmania ulishindwa na upande ulioshinda katika vita hivyo yaani Uingereza na waitifaki wake ulilitambua rasmi mamlaka ya Uingereza kwa Iraq pasi na kuzingatia haki na matakwa ya wananchi wa eneo.
Katika kipindi hicho, Mirza Shirazi Mdogo alifanya juhudi za kuwaandikia barua viongozi wa mataifa ya Ulaya na Kiarabu na kuwafikishia walimwengu sauti ya wananchi wa Iraq. Akiwa pamoja na baadhi ya Maulamaa alituma barua kwa watawala wa Saudi Arabia na Syria akiwataka mbali na kuunga mkono haki za wananchi wa Iraq watumie vyombo huru ulimwenguni kufikisha habari ya kukaliwa kwa mabavu Iraq. Akiwa pamoja na Sheikh al-Shariah Isfahani alimuuandikia barua pia Rais wa wakati huo wa Marekani na kutangaza kwamba, takwa la wananchi wa Iraq ni kuundwa dola huru la Kiislamu na kuchaguliwa mfalme ambaye kwanza awe Mwislamu na pili awe anafungamana na kulizingatia Baraza la Taifa la Iraq.
Katika kipindi na miaka ya vita, Waingereza ambao walikuwa wamepata na hasara nyingi za kiuchumi, walikuwa wakitafuta njia ya kuwa na usimamizi kwa ardhi zilizokuwa zimekabiliwa kwa mabavu kwa namna ambayo hilo liwe na gharama kidogo kwao. Katika upande mwingine katika ardhi za Kiislamu kama Iraq, kulikuwa kukiendelea harakati za wananchi zilizokuwa dhidi ya mkoloni Muingereza na Maulamaa hawakuwa wameacha upinzani wao dhidi ya Uingereza. Kudhibiti hali hii lilikuwa jambo gumu mno kwa Uingereza. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana viongozi na watawala wa Uingereza wakachukua uamuzi wa kuitisha uchaguzi ili nchini Iraq atawale mtu ambaye kidhahiri atakuwa amechaguliwa na wananchi lakini katika uhalisia wa mambo awe ni mwenye kufuata na kutekeleza sera na siasa za Uingereza.
Maulamaa wa Kiislamu kutokana na kufahamu vyema ukoloni mkongwe wa Uingereza walipinga vikali kufanyika uchaguzi uliokuwa umeitishwa na Uingereza. Muhammad Taqi Shirazi ambaye katika miaka hiyo alikuwa na jukumu la Umarjaa wa Mashia alitangaza katika fatuwa aliyoitoa ya kwamba, "Hakuna Mwislamu ambaye ana haki ya kumchagua ambaye sio Mwislamu kwa ajili ya kuongoza na kuwa na mamlaka kwa Waislamu".
Sambamba na fatuwa hiyo, mwanawe yaani Muhammad Ridha Shirazi ambaye alikuwa amepewa jukumu na baba yake la kuandaa na kukusanya vikosi vya wananchi wa Iraq, akiwa Karbala alianzishaa jumuiya iliyojulikana kwa jina la "Jumuiya ya Kiislamu” ambapo ndani yake walikuwemo Mulamaa mashuhuri na watajika katika zama hizo. Lengo la kundi hilo lilikuwa ni kukomboa ardhi ya Iraq na kuendesha mapambano dhidi ya Uingereza. Katika kipindi kifupi tu, viongozi wa jumuiya hiyo walitiwa mbaroni na kupelekwa uhamishoni nchini India. Mirza Shirazi akachukua uauuzi wa kuelekea Iran na akiwa huko akatoa fatuwa yya jihadi na kusimama kukabiliana na mkoloni Muingereza. Maulamaa wa Iraq nao kuanzia Najaf, Karbala mpaka Kadhmein wakawa pamoja naye katika uamuzi huo. Baada ya Uingereza kuona hali hiyo katika kipindi cha chini ya miezi minne waliwarejesha Iraq shakhsia na viongozi wa harakati hiyo waliokuwa wamepelekwa uhamishoni nchini India.
Mwaka 1338 Hijria Mirza Muhammad Taqi Shirazi akiwa naumri wa miaka 80 alianza mwenendo mpya wa mapambano. Aliwaita katika kikao cha siri huko Najaf Iraq, idadi kadhaa ya Maulamaa, viongozi wa kikabila na shakhsia wengine. Katika kikao hicho iliamuliwa kuanzishwe hatua mpya za kukabiliana na wavamizi Waingereza.
Hatimaye wanamapinduzi walifanikiwa kuudhibiti mji wa Karbala na kuuondoa katika udhibiti wa Uingereza.
Miezi miwili tu baada ya mafanikio hayo, Mirza Muhammad Taqi Shirazi aliaga dunia katika kifo cha utatanishi. Baadhi wanaamini kuwa, vibaraka wa Uingereza walimpa sumu mwanazuoni huyo na kumuua shahidi. Alimu na mwanamapambano huyo amezikwa katika Haram ya Imam Hussein (as) mjini Karbala Iraq.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki kwa leo umefikia tamati, tukutane tena juma lijalo siku na wakati kama huu katika sehemu nyingine ya kipindi hiki.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.