Hakika ya Uwahabi (9)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu ambaye ndiye atakayekuwa hakimu wa pekee Siku ya Kiama, Siku ambayo itamtosha kila mtu kujihisabu mwenyewe kuhusiana na matendo aliyotenda na wala hakuna mtendadhambi yeyote atakayekwepa adhabu kali ya Mweyezi Mungu na bila shaka Mwenyezi mungu hatamdhulumu mtu yeyote. Siku hiyo itakuwa ni siku ya adhabu ya kudhalilisha kwa wanafiki.
Salamu ziwe juu ya wale wote ambao licha ya kuzungukwa na ulimwengu uliojaa mawimbi na tufani kali ya uongo na upotofu lakini wameamua kulinda na kuziangaza nyumba za nyoyo zao kwa hakika iliyo wazi.
Tulisema katika vipindi viwili vilivyopita kwamba kisingizio kinachotumiwa na Mawahabi kwa ajili ya kuharibu makaburi ya Mitume na Maimamu watoharifu (as) ni kwamba wanachukulia tawassul kuwa jambo lililoharamishwa na kudhani kwamba watu walioaga dunia ni wafu wasiokuwa na athari yoyote humu duniani. Tulisema kuwa fikra hiyo potofu inapingwa na wanazuoni wa madhehebu zote za Shia na Suni na kwamba haiendani na mafundisho ya Aya za Qur'ani Tukufu wala sira na nyendo za maisha ya Mtume Mtukufu (saw). Sasa swali letu hapa ni kwamba, je, kama fikra na itikadi hizo hazitokani na dini wala sira ya Mtume (saw) ni vipi watu wanaodai kuwa ni Waislamu wanakuwa na itikadi potovu kama hizo? Ikiwa itikadi na matendo yanayotokana na fikra hizo hayana misingi yoyote katika dini tukufu ya Uislamu basi yanatokana na nini?
Ili kujibu maswali haya ya msingi, ni muhimu tupanue upeo wa mitazamo yetu na tuchunguze kwa makini historia ya Mawahabi au kwa ibara nyingine Masalafi wa leo.
***************
Kile ambacho kimesajiliwa katika nyaraka za historia ni kwamba zaidi ya Waislamu elfu saba waliuawa kinyama na kwa umati kwa ajili ya kubuniwa utawala wa Kiwahabi wenye misimamo mikali ya kufurutu ada katika ardhi ya Hijaz ambayo ni Saudia ya leo. Baada ya utawala huo kudhibiti ardhi hiyo tukufu, ulivamia na kuharibu maeneo mengi matakatifu ya viongozi wa Uislamu. Mawahabi walibomoa na kuharibu kila kitu ambacho Waislamu walikuwa wakitabaruku nacho kwa kadiri kuwa waliharibu asilimia 90 ya athari na maeneo matakatifu ya Waislamu katika ardhi ya Hijaz. Waliharibu makaburi ya Jannat al-Mu'alla katika mji mtakatifu wa Makka ambako alizikwa Bibi Khadija, mke mpendwa wa Mtume Mtukufu (saw), Abu Talib, Ami yake pamoja na babu yake miongoni mwa watukufu wengine na makaburi ya Baqee mjini Madina Munawwara ambako kuna makaburi ya Maimau wanne watoharifu (as). Kama hilo halikutosha waliendelea na njama yao hiyo haribifu ya kubomoa na kufuta kabisa makaburi ya Mashahidi wa Vita vya Badr na Uhud, nyumba alikozaliwa Mtume (saw), nyumba ya Bibi Khadija (as) na nyumba ya Imam Ali na Bibi Fatwimah (as). Hiyo ni sehemu ndogo tu ya uharibifu uliofanywa na watawala wa Kiwahabi katika kufutilia mbali historia tajiri ya Waislamu katika ardhi ya Wahyi ya Hijaz.
Mawahabi hata walichoma moto maktaba ya kihistoria na kimataifa huko Saudia mbayo ilikuwa moja ya maktaba zenye thamani kubwa ya kihistoria. Maktaba hiyo ilijumuisha vitabu adimu zaidi ya 60,000 ambapo 40,000 kati yavyo vilikuwa vimeandikwa kwa maandishi yaliyorejea nyuma hadi zama za kabla ya Uislamu.
Hatua za uharibifu mkubwa ulioanzishwa na Mawahabi huko Hijaz katika zama hizo hii leo zinadumishwa na kukamilishwa na wafuasi wao wa Daesh katika maeneo mengi ya Waislamu. Wameharibu pakubwa athari za kihistoria kama vile mji wa kihistoria wa Namroud, jumba la makumbusho ya kale la Mosul nchini Iraq na maeneo mengine ya kihistoria na kiustaarabu kama vile mji wa kihistoria wa Tadmur (Palmyra) na Hekalu la Bel huko Syria na hasa katika miji ya Halab, Edlib, Dar'a' na Hamaa. Masalafi au tuseme Matakfiri hao ama waliiba au kuharibu kabisa athari za kale na kihistoria katika miji hiyo.
******************
Jambo la kushangaza ni kuwa mkabala wa uharibifu huo wote uliofanyika kwa kisingizio cha kuvunja masanamu ambapo athari nyingi za Kiislamu na kale zilibomolewa, kuna baadhi ya maeneo na majengo ya kihistoria yaliyoachwa bila kuguswa na Mawahabi kwa sababu yanahusiana na historia yao moja kwa moja. Mawahabi si tu wameyaacha maeneo na majengo hayo ya kale bali wamekuwa wakiyakarabati na kuyasajili kimataifa kama athari za kale za Wasaudi. Moja ya maneo hayo ni Khaibar, ngome ambayo inahusiana na Mayahudi wa Madina ambao licha ya kutia saini mkataba na Mtume Mtukufu (saw) mwanzoni mwa Uislamu, lakini walimfanyia hiana na usaliti. Eneo hilo hutembelewa sana na Mayahudi kila mwaka. Kuna maeneo mengine mengi ya Mayahudi mjini Madina ambayo yameachwa bila kughuswa na Mawahabi hadi leo hii. Moja ya maeneo hayo ni ngome na kasri la Ka'b bin Ashraf, mmoja wa Mayahudi waliokuwa na chuki kubwa dhidi ya Mtume Mtukufu (saw), na ambaye daima alikuwa akiwaudhi Waislamu kutokana na mashairi na vitendo vyake vya kuwakera. Mbali na athari hizo za Mayahudi, Mawahabi hata wangali wanahifadhi vitu vilivyoachwa nyuma na wafalme wao katika majumba ya maonyesho ya vitu vya kale. Wamehifadhi viatu vya Abdul Aziz, mmoja wa wafalme wa ukoo wa Aal Saud, katika kalibu ya kioo ili visifutike katika historia.
Waraka mwingine ambao unathibitisha undumakuwili na chuki ya Mawahabi dhidi ya Mtume (saw) na Watu wa Nyumba yake tukufu (as) kwa kudai kuwa ni haramu kuzuru makaburi na haram zao ni picha iliyochapishwa katika gazeti moja la Marekani. Katika muongo wa 50 Miladia, wakati wa kutiwa saini mikataba ya kistratijia kati ya Marekani na Saudi Arabia, moja ya magazeti ya Marekani yalichapisha picha ambayo ilionyesha picha ya wafalme watano wa Saudia wakiwa pembeni ya kaburi la George Washington, rais wa kwanza wa Marekani. Sio tu walizuru kaburi hilo bali walibeba na kuweka juu yake shada kubwa la maua kama ishara ya kutoa heshima zao kwa kiongozi huyo wa zamani wa Marekani. Katika picha hiyo Mfalme Abdul Aziz anaonekana pembeni mwa kaburi hilo akiwa na watoto wake wanne wa kiumme, Saud, Faisal, Khalid na Fahd ambao wote walikuwa wafalme wa Saudia katika vipindi tofauti vya maisha yao baada yake.
**************
Maswali yetu sisi kwa Mawahabi, tukiwa watu wanaotumia akili salama na watafuta haki ni kama ifuatavyo: Je, ni vipi kuzuru kaburi la Mtume Mtukufu (saw) na ya watu wengine wema wa nyumba yake itakuwa ni shirki ilihali wao kuzuru kaburi la rais wa zamani wa Marekani na kutoa heshima mbele yake hakuna tatizo lolote la kisheria?
Ikiwa kulinda athari za ustaarabu na historia ya Waislamu au tamaduni za mataifa mengine ni bida' na haramu basi ni kwa nini athari za Mayahudi zimeondolewa kwenye mkondo huo?
Ikiwa juhudi za kulinda na kuhifadhi nyumba na vitu vingine vilivyoachwa nyuma na Mtume Mtukufu (saw) ni jambo baya na linalokemewa, basi ni kwa nini mnahifadhi viatu vya wafalme wenu kwenye majumba ya vitu vya kale?
Huenda tukapata majibu ya maswali haya kwenye hutoba iliyotolewa na Ernest Bevin. Bevin ambaye alihudumu miaka 6 ya mwisho ya umri wake kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, alisema katika hotuba yake kwenye Congress ya nchi hiyo kuwa ukoo wa Aal Saudi ulikuwa ukishirikiana na Marekani katika kusukuma mbele malengo ya Mayahudi na kutekeleza siasa ambazo ziko dhidi ya Waarabu na Waislamu.
Isitoshe, Yitzhak Ben-Zvi, rais wa pili wa utawala haramu wa Israel, ameandika kitabu kuhusu Uyahudi na kusema kwamba kuna baadhi ya makundi ya kidini katika nchi za Kiislamu ambayo yanajiona kuwa miongoni mwa Mayahudi ambapo sasa yanatekeleza tamaduni za dini ya Kiyahudi. Ben-Zvi amewataja wazi wazi Mawahabi kuwa miongoni mwa makundi hayo na kuandika; Wao ni Waislamu kidhahiri tu, lakini kwa matendo na faraghani, wanahuisha shaari na nembo za dini ya Mayahudi.
**************
Katika Qur'an Tukufu, Mwenyezi Mungu amewatambulisha wanafiki na kusema kuwa ni wale wanaoshajiisha ufisadi, wanazuia watu kufanya mambo mema, na wamemsahau Mwenyezi Mungu katika maisha yao yote, ni wavunja sheria na wapotovu, lakini pamoja na sifa zote hizi mbaya, wanadai kumwamini Mungu na kwamba imani yao katika misingi ya Uislamu ni thabiti na imara kuliko watu wengine. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 16 ya Surat al-Mujaadalah:
Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.
Aya hii inaeleza hali ya wanafiki, ambao licha ya kutokuamini kwao dini, lakini wanaapa kuwa wao ni waumini halisi wa dini ya Mwenyezi Mungu, na hivyo kutumia kisingizio hicho kuhujumu shaari na nembo zote za dini na kuwazuia watu kuwa waumini. Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu amewaahidi watu kama hao adhabu ya kuwafedhehesha, na Yeye ndiye mkweli zaidi wa wanaotoa ahadi.
Huku tukiwa na matumaini ya kutimizwa ahadi hii ya kweli, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aalykum Warahmatullahi Wabarakatuh.