Mar 12, 2023 07:43 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 13

Wakati mwingine wahalifu husema uwongo mkubwa ili kuepuka kuangamia, "Daima kuna nguvu ya kuaminika katika uwongo mkubwa." Hii ni moja ya kauli mashuhuri za Adolf Hitler.

Bismillahir Rahmanir Raheem. Kwa jina la MwenyeziMungu mjuzi wa siri zote. Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Wakati mwingine wahalifu husema uwongo mkubwa ili kuepuka kuangamia, "Daima kuna nguvu ya kuaminika katika uwongo mkubwa." Hii ni moja ya kauli mashuhuri za Adolf Hitler. Yeye, na bila shaka idadi kubwa ya wanasiasa wengine wanaamini kwamba, uwongo unapaswa kusemwa kwa kiasi kikubwa kidiri kwamba si tu umfanye mtu asithubutu kuukana, bali hata asifikirie kabisa kuwa jambo kama hilo ni uwongo.

**********************

Ilikuwa katikati ya Vita vya Kwanza vya Dunia ambapo mkataba ulitiwa saini kati ya Uingereza na serikali ya Kiwahhabi ya Saudi Arabia. Mfalme Abd al-Aziz aliandika chini ya mkataba huo maneno yafuatayo: "Mimi, Mfalme Abd al-Aziz bin Abd al-Rahman Afsal Saud, ninakiri mara elfu moja kwamba kwa maoni yangu ... hakuna tatizo katika kuikabidhi Palestina kwa Mayahudi" ..... takriban miaka 24 baadaye na kabla ya kunza Vita vya Pili vya Dunia; Churchill, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza, alimwambia Weisman, Mkuu wa Jumuiya ya Wazayuni Duniani: Ninataka ujue kwamba nimekuandalia mpango ambao hautatekelezwa hadi mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Nimeamua kuwa Ibn Saud atakuwa kiongozi na mtawala wa watawala wa Mashariki ya Kati, bila shaka, kwa sharti kwamba akubaliane na wewe kwanza. Wakati mpango huo utakapokamilika, itakulazimu  uchukue kutoka kwake kila kitu unachotaka na kinachoweza kupatikana. Bila shaka, tutakusaidia katika kazi hii, lakini ni muhimu kwako kulificha jambo hili na nitalijadili na Roosevelt (Rais wa Marekani)..."

Churchill (kulia), Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia/ Weizmann, Mkuu wa Jumuiya ya Wazayuni Duniani

Vita vya Pili vya Dunia vilidumu kwa miaka sita... Katika vita hivyo, raia milioni 40 na wanajeshi milioni 20 kutoka nchi mbalimbali walipoteza maisha, miji mingi iliharibiwa, watu wengi wakachukuliwa mateka au kujeruhiwa na familia nyingi zikasambaratika. Moja ya matokeo muhimu ya vita hivyo vya umwagaji damu kwa manufaa ya Waingereza, ilikuwa ni kudhibiti kwao Palestina. Waliweka vikosi vyao vya kijeshi na kisiasa huko Palestina kwa muda wa miaka miwili na hivyo kuandaa mazingira ya kuhamia huko maelfu ya Mayahudi. Mwishoni mwa 1947, Umoja wa Mataifa, ambao ulikuwa bado mchanga wakati huo, ulipitisha azimio lililoigawa Palestina katika sehemu tatu za Mayahudi, Waarabu na kimataifa. Azimio hilo lilikwenda kinyume na sheria zilizokubalika katika Umoja wa Mataifa, lakini pamoja na hayo Marekani ilitumia ushawishi wake kwa nchi za Amerika ya Latini kuliidhinisha na kuzilazimisha kukubaliana nalo. Bila shaka, Umoja wa Kisovyeti pia ulishirikiana na nchi hizo kuhusu suala hilo. Uamuzi huo haukuwafurahisha walio wengi huko Palestina, yaani Waislamu. Licha ya pingamizi zote hizo za kisheria na baada ya kufumbiwa macho haki za watu na serikali za Kiislamu, miezi michache baadaye, utawala wa Kizayuni ulitangaza kuasisiwa kwake na hivyo kuamsha hasira za Waislamu.

****************

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia hadi kukaliwa kwa mabavu Palestina, Waarabu walioishi katika nchi ndogo ambazo zote zilitawaliwa na madola ya Magharibi walishuhudia ukandamizaji wa wakoloni na unyonge wa kupindukia dhidi yao. Udhalilishaji na ukatili huo uliibua hasira kubwa miongoni mwao... na kukaliwa kwa mabavu Palestina kuliwasha moto wa ghadhabu katika ulimwengu wa Kiislamu. Waislamu walikerwa sana na hatua hiyo na wote wakaingiwa na hamasa kubwa ya kutaka kuikomboa Palestina. Hamasa hiyo ndiyo iliyafanya majeshi ya Waarabu kuingia Palestina siku moja tu baada ya kuasisiwa utawala haramu wa Israel. Majeshi hayo yalipata ushindi fulani mwanzoni mwa kuingia kwao Palestina, lakini yakashindwa muda mfupi baadaye kwa sababu kadhaa. Sababu hizo zinapaswa kuchunguzwa na kutafutwa katika katika miaka ya kabla ya kuanza vita hivyo.

Anthony Eden, Waziri Mkuu wa Uingereza baada ya Vita vya Pili vya Dunia

Takriban miaka mitatu kabla ya kuanza vita vya Waarabu na Wazayuni, Robert Anthony Eden, Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, alitoa pendekezo la kushangaza... kuanzishwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League)... Unadhani ni kwa nini Uingereza ilitoa pendekezo la kuasisiwa jumuiya ya umoja na mshikamano, kidhahiri kwa manufaa ya watu ambao siku zote ilikuwa ikipigana vita nao?!!!

*************

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ilipaswa kuwa jumuiya ya kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiarabu. Ilitakiwa kuimarisha umoja wa Waarabu kwa namna ambayo ingerudisha heshima yao, kuhuisha haki zao zilizoporwa na kufuatilia mustakbali wao mwema ambao ungewarejeshea matumaini. Lakini baada ya kupita miaka mingi tangu kuanzishwa jumuiya hiyo, wachambuzi wengi wa Kiarabu wanaamini kuwa taasisi hiyo sio tu kwamba haijakuwa na faida yoyote kwa Waarabu, bali mara nyingi imekuwa ikienda kinyume na maslahi yao na kuwadhuru moja kwa moja. Ali Al-Khayat, mmoja wa wachambuzi wa Kiarabu anasema: “Tangu kuasisiwa kwake, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu haijaweza kufikia hatua na mipango ambayo watu wanatarajia kutoka kwake. Hivi sasa watu wanaitazama kwa jicho la shaka na wala hawaiamini hata kidogo." Kwa mtazamo wake wachambuzi wengine wengi wa Kiarabu, wanaamini kuwa kwa miaka mingi Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeshindwa kufikia malengo yake. Ariel Sharon, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni pia alisema katika moja ya hotuba zake kwamba: "Maidhinisho na maazimio ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hayana umuhimu wowote na hata hayana thamani ya karatasi zinazoandikwa humo."

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa sababu ya kushindwa huko inatokana na kujidhalilisha na kujisalimisha baadhi ya nchi za Kiarabu kwa Marekani na Uingereza. Serikali hizo vibaraka, sio tu katika suala la Palestina bali pia katika masuala ya hivi karibuni zaidi kama vile mgogoro wa Syria na Iraq, haziruhusu kuchukuliwa misimamo yenye nguvu na ya wazi dhidi ya wavamizi na wachokozi. Nchi tajiri kama vile Saudi Arabia zinajiona kuwa mabwana wa jumuiya hiyo kutokana tu na kuwa ndizo zinazodhamini matumizi na gharama zake za kifedha na hivyo humlazimisha katibu mkuu wa jumuiya hiyo kuchukua misimamo mikali dhidi ya baadhi ya serikali za Kiarabu na kuunga mkono makundi hasimu ya kigaidi dhidi ya serikali hizo. Kwa maneno mengine ni kuwa siasa mbovu za nchi hizo tajiri za Kiarabu zimeifanya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuwa adui wa mmoja wa wanachama wake.

Mfalme Faisal, Mwanamfalme wa Saudi Arabia akiwa na Weizmann, Mkuu wa Jumuiya ya Wazayuni Duniani

Kwa utendaji kama huo, na bila shaka kwa kukumbuka maneno ya Churchill kwa Weizmann na pia kwa kutilia maanani kukiri Abdul Aziz bin Saud mara elfu moja kuhusu nafasi ya Waingereza katika eneo la Mashariki ya Kati, inabainika wazi kwamba kubuniwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa pendekezo la Uingereza ni moja ya uwongo mkubwa ambao watenda-jinai huutumia kuepuka maangamizi. Ni wazi kuwa wakati huo waongo hawakutumia uwongo huo kuepuka maangamizi tu bali ulikuwa mwanzo wa wao kuanzisha njama nyingine kubwa dhidi ya Umma wa Kiislamu. Ni wazi kuwa huko nyuma walikuwa wamewahi kutekeleza njama hiyo kwa mbinu tofauti lakini wakashindwa kufikia malengo waliyokusudia lakini mara hii walikuwa wamepata fursa mpya ya kuitekeleza bila kukabiliwa na vikwazo vikubwa. Njama hiyo mbovu haikuwa na lengo jingine ghairi ya kuibua ugomvi na mgawanyiko kati ya Waislamu, mara hii ikiwa ni kwa anwani ya Waarabu na wasio Waarabu. Nam, hizi ndizo siasa za Uingereza na Marekani, yaani za kufanya kila kitu na kundi lijiharibu lenyewe kutokea ndani. Huyachukua mateka mataifa kwa kisingizio cha kuyaletea uhuru, kupora utajiri wao kwa jina la kuyaletea maendeleo, kutenda jinai kwa jina la kutetea haki za binadamu na kuyagawanya kwa kisingizio cha kuyaletea umoja.

***************

Mfalme Faisal, mmoja wa wanawafalme wa Saudia, anaandika katika kumbukumbu zake: "Sisi na Mayahudi ni binamu, kwa hiyo...... tunataka kuishi nao kwa amani na usalama." Ili kuunda na kudumisha amani na usalama huo kati yao na binamu zao, Mawahabi wa Saudia wamekiuka kivitendo itikadi na malengo yote ya Uislamu na kufanya jinai kubwa dhidi ya Umma wa Kiislamu. Hawajawahi kupigana vita au kushiriki katika mvutano wowote wa moja kwa na utawala wa Kizayuni, bali wamekuwa wakitumia kila fursa inayojitokeza kwa shabaha ya kuanzisha uhusiano wa kirafiki kati ya Waarabu na Mayahudi. Natija ya juhudi hizo ni makubaliano kadhaa eti ya amani ambayo yametiwa saini kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni, moja ya makubaliano ya hivi karibuni zaidi ikiwa ni Makubaliano ya Ibrahim. Makubaliano ambayo yamepelekea nchi za Misri na Jordan, zikifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain, kutambua rasmi uwepo wa utawala haramu wa Kiyahudi na kuanzisha nao uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia.

Kutoka kushoto kwenda kulia: Waziri wa mambo ya nje wa Bahrain, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, rais wa Marekani na waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu/White House - Makubaliano ya Ibrahim - Septemba 2020

Amani na urafiki, usalama na utulivu ni mambo mazuri na ya kuvutia sana, lakini hayapasi kutufanya tusahau ukatili, mauaji na uporaji, ubakaji na mauaji ya kizazi yanayofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya Waislamu wa Palestina kwa ushirikiano wa nchi za Magharibi na vibaraka wao wa Kiarabu na hasa mawahabi wa Saudi Arabia. Haiwezekani kuwakumbatia wahusika wa jinai hizo na kutoa wito wa kuwepo amani na urafiki na watenda-jinai hao. Ni fisi waliovaa ngozi ya kondoo ambao wanaweza kufanya usaliti na jinai nyingine kubwa wakati wowote. Ni wezi ambao wamejipenyeza ndani ya msafara na hawawezi wala hawapaswi kuaminika. Kufanya amani na urafiki na wahalifu kama hao yenyewe ni dhulma ya wazi ambayo lazima ipigwe vita.... Huu ni mfano mwingine wa kukifanya kitu kijiangamize chenyewe kutokea ndani. Mara hii njama inayofanywa ni ya kutumia jina la amani na urafiki, kwa ajili ya kuketisha dhuluma, uchokozi, mauaji na uporaji kwenye kiti cha enzi, na hilo halina maana nyingine isipokuwa  kutokomeza amani, usalama na utulivu.

Sehemu ya matini ya mapatano ya Ibrahimu