Mar 22, 2023 13:42 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (67)

Assalaam Alaykum Wapenzi Wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, bila kusahau athari na vitabu vyao.

 

Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari maisha na historia ya Mulla Muhammad Kadhim Khorasani mashuhuri zaidi kwa jina la Akhund Khorasani, mmoja wa Marajii wakubwa wa Kishia baada ya Mirza Shirazi. Kadhalika tuliashiria harakati zake za kijamii pamoja na harakati zake za uandishi wa vitabu ambapo kitabu chake mashuhuri zaidi ni Kifayat al-Usul. Sehemu ya 67 ya mfululizo huu juma hili, itamuangazia japo kwa mukhtasari alimu na mwanazuoni mwengine mahiri na mashuhuri wa Kishia ambaye ni Ayatullah Shekhe Fadhlullah Kojuri. Tafadhali kuweni pamoja nami hadi mwisho wa kipindi cha leo kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.

 

Fadhlullah Kojuri mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Fadhlullah Nouri alizaliwa 1259 mwafaka na 1843 Miladia katika Wilaya ya Kojur kwenye mji wa Nur ulioko katika mkoa wa Mazandaran Iran.  Baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi alielekea katika mji wa Tehran na baada ya muda akiwa na azma ya kujiendeleza zaidi kielimu alifunga safari na kuelekea katika mji mtakatifu wa Najaf Iraq. Akiwa katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) katika mji wa Najaf, Fadhlullah Nouri alihudhuria darsa na masomo ya walimu mahiri na watajikka katika zama hizo kama Mirza Habibullah Rashti na Sheikh Radhii.

Sheikh Fadhlullah Nouri

 

Baadaye alianza kuhudhuria masomo yaliyokuwa yakifundishwa na Mirza Shirazi mkubwa. Baada ya Mirza Shirazi mkubwa kuhajiri na kuhamia katika mji wa Samarra, Fadhlullah Nouri pia akiwa pamoja na kundi kubwa la wanafunzi wa Mirza Shirazi alihamia katika mji wa Samarra. Kwa kuzingatia kwamba, Sheikh Fadhlullah Nouri alikuwa akiamianiwa sana na Mirza Shirazi wa kwanza, alipewa jukumu la kurejea Tehran na kuongoza harakati za kisiasa na kijamii za Iran. Akijibu takwa hilo, mwaka 1303 Hijria, akiwa katika muongo wa nne wa umri wakke yaani miaka 40, Fadhlullah Nouri aliwasili katika mji wa Tehran.

Akiwa mjini Tehran alijishughulisha na kufundisha masomo ya Hawza sambamba na kuandika na kualifu vitabu. Alifanikiwa kkatuika uwanja huo kulea wanafunzi ambao baadaye waliondokea kuwa na taathira katika jamii ya Kiislamu ya Iran. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Sheikh Abdul-Karim Hairi, alimu mashhuhuri na msomi ambaye alikuja baadaye kuasisi Hawza ya Qum.

Chuo Kikuu cha Kidini ambacho leo ni moja ya vituo muhimu zaidi vya ufundishaji na utoajii wa wanafunzi wa dini katika ulimwengu wa Kishia. Sheikh Fadhlullah Nouri akiwa mwakilishi wa Mirza Shirazi mkubwa alikuwa akiheshimiwa sana na wasomi na wanazuoni mbalimbali wa zama hizo katika ulimwengu wa Kiislamu.

 

Shekhe Fadhlullah Nouri alikuwa amebobea pia katika elimu nyingine kama ambavyo alikuwa na weledi wa hali ya juu katika masuala yanayohusana na jamii. Hali hiyo ilimfanya azingatiwe mno na wanafikra na viongozii wa zama zake kiasi kwamba, Kansela wa wakati huo wa Iran alikuwa na mapenzi na urafiki mkubwa na Sheikh Fadhlullah Nouri.

Moja ya hatua muhimu za alimu huyu ni himaya na uungaji mkono wake kwa harakati ya kupigania katiba iliyojulikana kama Englabe Mashrooteh (Constitutional Revolution).

Yeye pamoja na Akhund Khorasani tuliyemzungumzia katika kipindi chetu kilichopita pamoja na Maulamaa wengine wa Najaf waliwashajiisha watu waungane na harakati hiyo, jambo ambalo liliandaa uwanja na mazingira ya kupatikana ushindi.

Harakati ya kupiigania katiba haikuishia kwa Sheikh Fadhlullah Nouri na wakazi wa Tehran tu, bali ilijumuisha Iran nzima. Maulamaa na wananchi waliokuwa wameshikamana na dini wote kwa pamoja walikuwa wakiitaka na kuitetea harakati hiyo. Hata hivyo baadhi ya propaganda ziliwafanya baadhi ya watu wenye ufahamu mdogo kupingana na Maulamaa. Sheikh Nouri akkiwa na lengo la kuwekak wazi mambo akiwa pamoja na wafuasi wake walifanya mgomo wa kukketi kattika haram ya Hadhrat Abdul-Adhim Hassani katika mji wa Rey. Alitangaza wazi na bayana kwamba, hapingi mapinduzi ya katiba na kubanwa utawala wa Kifalme, lakini  anaona ni jambo la dharuura kuweko magezuio ya mambo, kutekelezwa uadilifu, kuweko sheria ya lazima ambayo katika nchi ya Kiislamu sheria hiyo inapaswa kuwa ni ya dini au kwa uchache iwe inaafiki hukumu za Kiislamu na sio kwamba, sheria hiyo ipuuze Uislamu na yenyewe iwe ni udikteta mpya.

Mapinduzi ya katiba

 

Hatua za Sheikh Fadhlullah Nouri za kuweka wazi mambo zilipelekea wapigania katiba kutokuwa na chaguo isipokuwa kukubaliana na hilo na wakatangaza kwamba, neno la mashrooteh halipingani na dini na hukumu za kisheria. Kwa tangazo hilo Sheikh Fadhlullah Nouri na wafuasi wake wakahitimisha mgomo wao wa kuketi.

Hata hivyo wapigania katiba kivitendo walifuata njia na mkondo uleule wa hapo kabla. Mara hii wakafanya njama za kupunguza nguvu na nafasi ya Sheikh Fadhlullah Nouri baina ya watu. Ni kwa muktadha huo, wakaja na telegrafu bandia kutoka kwa Maulamaa wa Najaf iliyokuwa ikitangaza kwamba, Sheikh Nouri amepoteza hadhi ya ijtihadi kutokana na kukwamisha masuala ya Waislamu. Licha ya kuwa katika zama hizo Shekh Nouri hakuwa akiendesha harakati dhidi ya wapigania katiba, lakini propaganda hizo ziliwafanya baadhi ya wanaharakati hao wafanye njama za kumuua Sheikh Nouri, ingawa njama hizo zilifeli.

Kaburi la shahidi Sheikh Fadhlullah Nouri

 

Baada ya kuaga dunia Mozaffar ad-Din Shah, Muhammad Ali Shah akisaidiwa na vikosi vya usalama alivunja Bunge la Taifa la Ushairi na hivyo akawa amesambaratisha mapinduzi ya katiba. Hata hivyo haukupita muda wapigania katiba wakafanikiwa tena kuudhibiti mji wa Tehran.

Viongozi wa ukombozi wa Tehran wakaunda Bunge na kuliita Bunge la Juu. Wakamchagua mtoto wa Muhammad Ali Shah yaani Ahmad Shah kuwa mfalme na kugawana baina yao nyadhifa mbalimbali serikalini na kwa mara ya kwanza wakataka kulipiza kisasi waliopinga harakati hiyo. Muhammad Ali Shah akakimbilia katika ubalozi wa Russia na kuomba hifadhi na wapinzani wengine wa harakati ya kupigania katiba kila mmoja alishika roho yake mkononi na kukimbia. Hata hivyo Sheikh Fadhlullah Nouri alibakia nyumbani kwake mjini Tehran na hakuwa tayari kuwa chini ya bendera ya ukafiri ili kuokoa roho na maisha yake.

Hatimaye nyumba yake ilivamiwa na akatiwa mbaroni. Akashhikiliwa kwa siku kadhaa katika kituo cha polisi na baadaye akanyongwa.

Naam, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh