Apr 06, 2023 22:48 UTC
  • Ijumaa, tarehe 7 Aprili, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 16 Ramadhani 1444 Hijria sawa na Aprili 7 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 717 iliyopita, alifariki dunia Ibn Zamlakani, mtaalamu wa sharia za Kiislamu, hadithi na fasihi mkubwa wa mjini Damascus, Syria. Ibn Zamlakani alisoma elimu mbalimbali kutoka kwa maulama wakubwa wa zama zake huku akiipa umuhimu mkubwa elimu ya dini na hadithi. Miaka 20 baadaye Ibn Zamlakani alifikia daraja ya kutoa fatwa katika masuala ya dini. Alijishughulisha pia na shughuli za ukadhi na ukufunzi katika shule tofauti za mji wa Damascus. Moja ya athari za Ibn Zamlakani ni pamoja na kitabu cha 'Burhanul-Kaashif an I'jaazil-Qur'an.'

Siku kama ya leo miaka 599 iliyopita alifariki dunia Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Maqrizi alizaliwa mjini Cairo, Misri na baadaye kusoma elimu ya Kiislamu katika miji tofauti ya nchi hiyo kama ambavyo pia alikuwa na uhodari katika elimu mbalimbali za Kiislamu. Kwa muda fulani alifanya kazi ya ukadhi mjini Cairo. Alipendelea sana historia huku akiandika vitabu tofauti katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi ni pamoja na kitabu cha 'as-Suluuk Lima'arifatil-Muluuk' ambacho kinazungumzia historia.

Katika siku kama ya leo miaka 302 iliyopita, Peter the Great mfalme wa wakati huo wa Russia aliivamia Sweden. Ruussia na Sweden zikishirikiana na Poland na Denmark kuanzia mwaka 1700 zilikuwa katika vita vya kaskazini. Wakati jeshi la Russia linaishambulia Sweden nchi hiyo ilikuwa imefikia mapatano na nchi nyingine zilizokuwa pamoja vitani na ilikuwa na mpango wa kupatana na Russia pia. Hata hivyo Peter the Great ambaye alikuwa na nia ya kupanua mamlaka yake, akiwa na jeshi lililojizatiti aliishambulia Sweden na baada ya kuishinda akaitwisha nchi hiyo mkataba wa amani.   

Peter the Great

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, alizaliwa mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bibi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika fani ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu.Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu". 

Bibi Annemarie Schimmel

Miaka 76 iliyopita mwafaka na leo, aliaga dunia msomi na mvumbuzi maarufu wa Kimarekani Henry Ford akiwa na umri wa miaka 84. Ford alizaliwa mwaka 1863 katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Greenfield nchini Marekani. Akiwa bado barobaro Henry Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa na alipokuwa kijana alifanya kazi ya umakanika. Henry Ford anatambuliwa kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari. 

Henry Ford

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya baraza la kwanza la dunia la afya na kuandika hati ya kwanza ya mkutano wa kimataifa wa afya. Baraza hilo pia lilichukua uamuzi kwamba tangu mwaka 1950 tarehe 7 Aprili itakuwa Siku ya Kimataifa ya Afya. Tangu mwaka huo tarehe 7 Aprili kila mwaka imekuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya.