Jumatatu, tarehe 10 Aprili, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 19 Ramadhani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 2023.
Miaka 1404 iliyopita, katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Imam Ali bin Abi Talib (as) ambaye ni mkwe, binamu na mtu wa karibu sana kwa Mtume Muhammad SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya kichwani akiwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri katika Msikiti wa Kufa huko Iraq. Imam Ali alipigwa upanga na mtu aliyejulikana kwa jina la Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali (as) alikufa shahidi siku tatu baadaye. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili mkubwa katika Uislamu baada ya Mtume Muhammad (saw) na anaelezwa katika historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa wa kupigiwa mfano, mwenye imani thabiti, akhlaki njema, elimu na uadilifu usio na kifani. Alipata elimu na kulelewa katika nyumba ya Mtume Muhammad (saw), na alikuwa mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali (as) alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali (as) alikuwa mpole na mwenye upendo. Imam Ali daima alitetea haki na uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima, Imam Ali bin Abi Twalib anasema: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake."

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 Miladia huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25.
Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 Miladia sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon. Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO). Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na 21 Farvardin 1367 Hijria Shamsia, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia mji wa Marivan magharibi mwa Iran na kukilenga kijiji kimoja kwa mabomu ya kemikali. Raia kadhaa waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika jinai hiyo ya utawala wa Saddam Hussein. Jamii ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi zilinyamazia kimya jinai hiyo na badala yake zilitoa misaada zaidi ya silaha za kemikali kwa nchi hiyo.
