Apr 10, 2023 22:47 UTC
  • Jumanne, tarehe 11 Aprili, 2023

Leo ni tarehe 20 Ramadhani 1444 Hijria sawa na 11 Aprili 2023.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka wa 8 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi na kuwafanya waingie kwa wingi katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Makka

Siku kama ya leo miaka 902 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 542 Hijiria, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Kiislamu. Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na ni kwa sababu hiyo ndio maana akaitwa al Alawi, al Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo. Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamasah' na 'Mandhumat Ibn Shajari.' Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad, Iraq na kuzikwa mjini hapo. 

Siku kama ya leo miaka 818 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 626 Hijiria, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na wasomi watajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria ambaye alikuwa mtaalamu mashuhuri wa jiografia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Mu'jamul-Buldan" na Mu'jamul- Udabaa." 

Siku kama ya leo miaka 770 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 674 Hijiria, alifariki dunia Ibn Saai Baghdadi, mtaalamu wa fasihi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Sheikh Tajud-Din Abu Twalib Ali Ibn Anjub Ibn Uthman Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Saai, alizaliwa mwaka 593 huko Baghdad, Iraq. Alijifunza elimu za zama zake kwa walimu mbalimbali. Kwa miaka kadhaa Ibn Saai alisimamia maktaba ya utawala wa wakati huo mjini Baghdad ambayo ilitumiwa kwa ajili ya kutwalii. Baada ya Baghdad kudhibitiwa na silsila ya utawala wa Wamongoli, Ibn Saai Baghdadi aliteuliwa na Nasir al-Din al-Tusi kwa ajili ya kusimamia maktaba mbalimbali za mji huo. Ni katika kipindi hicho ndipo akatokea kuwa mwandishi mkubwa, jambo ambalo lilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Kitabu cha 'al-Khulafaau' ni miongoni mwa athari mashuhuri za Ibn Saai. Vilevile ameandika kitabu cha 'Akhbarul-Udabaa' 'Akhbarul-Hallaj' na 'Akhbaru Qudhaatu Baghdad.' Abin Saai alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa Baghdad. 

Tarehe 11 Aprili miaka 163 iliyopita chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Ferdinand Carre

Miaka 38 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti. 

Enver Hoxha

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran. Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine.