Alkhamisi, tarehe 20 Aprili 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Ramadhani 1444 Hijria sawa na 20 Aprili mwaka 2023.
Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 221 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) imekuwa ikilengwa na mawahabi. Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi walidumisha mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Ustadh Muhammad Taqi Shariati, mfasiri wa Qur'ani na mwanafikra wa Kiislamu wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alizaliwa mwaka 1286 Hijria Shamsia na baada ya kumaliza masomo yake ya awali alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had hapa Iran na kuanza kusoma masomo ya dini kwa juhudi na hima kubwa. Baada ya muda mfupi alijiunga na harakati za Kiislamu za kueneza utamaduni na maarifa ya Kiislamu. Aidha akiwa mjini humo Ustadh Shariati alianzisha taasisi ya kueneza maarifa halisi ya Uislamu sambamba na kuandaa vikao vya elimu na kufundisha darsa za tafsiri ya Qur'ani.
Miaka 24 iliyopita, katika siku kama ya leo, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari. Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, katika jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo. Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema kuuwa, uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.
Katika siku kama ya leo ya tarehe 20 Aprili miaka 13 iliyopita, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico. Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.