Apr 28, 2023 03:03 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 27 mwezi Aprili, mwaka 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Shawwal 1444 Hijria sawa na tarehe 27 Aprili mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 658 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokezi wa Hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Baalbek moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus Syria baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhuri baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Bardes ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam.

Siku kama hii ya leo miaka 502 iliyopita, Ferdinand Magellan, baharia wa Kireno aliuawa na wenyeji wa Ufilipino kutokana na kuingilia mambo yao. Alizaliwa mwaka 1470 na kuanzia mwaka 1519 Miladia baharia huyo alianza safari yake kubwa ya baharini akiwa na meli tano. Ferdinand Magellan aligundua lango bahari huko kusini mwa bara la Amerika baada ya kuwasili katika pwani ya Amerika ya Latini. Lango bahari hilo limepewa jina la baharia huyo wa Kireno yaani Lango Bahari la Magellan.

Ferdinand Magellan

Miaka 63 iliyopita katika siku inayofanana na hii ya leo, nchi ya Togo inayopatikana huko katika pwani ya magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Wareno walikuwa watu wa kwanza kuikoloni Togo na nchi hiyo ilijulikana sana kwa jina la "Pwani ya Watumwa"  kwa kuwa nchi za Ulaya  zilikuwa zikiitumia nchi  hiyo kama kituo cha kusafirishia watumwa kuelekea Ulaya. Togo inapakana na nchi za Ghana na Benin na mji mkuu wake ni Lome.

Bendera ya Togo

Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sierra Leone moja ya makoloni makongwe ya Uingereza magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Sierra Leone ilianza kukoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 na nchi hiyo ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya kuuzia watumwa waliokuwa wakipelekwa Ulaya. Uingereza ilianza kuikoloni Sierra Leone mwishoni mwa karne ya 18 hadi mwaka 1961 wakati nchi hiyo ilipopata uhuru. Baada ya uhuru, nchi hiyo ilikumbwa na mapinduzi na uasi mwingi. Kijiografia  Sierra Leone iko Magharibi mwa Afrika ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 71,000 na inapakana na Guinea na Liberia. 

Bendera ya Sierra Leone

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita alifariki dunia Kwame Nkrumah, mwanasiasa mashuhuri wa Kiafrika na mpigania uhuru wa Ghana. Mkrumah alizaliwa mwaka 1909 na baada ya kupata shahada ya uzamivu nchini Marekani alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa. Baadaye Kwame Nkrumah aliasisi chama cha Kitaifa cha Watu wa Ghana na kuanza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Mwaka 1951 alishiriki katika uchaguzi wa Bunge na kuwa Waziri Mkuu. Baada ya Ghana kupata uhuru mwaka 1960 Kwame Nkrumah alikuwa Rais wa nchi hiyo lakini Februari 24 mwaka 1966 aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na wafuasi wa nchi za Magharibi akiwa safarini nchini Uchina. Baadaye alielekea Guinea ambako aliishi hadi kufariki dunia. Kwame Nkrumah anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamapambano mashuhuri wa Afrika waliofanya jitihada kubwa katika kupata uhuru na kujitawala nchi za bara hilo.

Kwame Nkrumah

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Jenerali Abdul Qadir alifanya mapinduzi nchini Afghanistan na baada ya kumuua Daud Khan Rais wa wakati huo wa nchi hiyo, alimuweka madarakani Noor Muhammad Taraki kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Khalq. Baada ya muda Hafizullah Amin alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Muhammad Taraki na yeye kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Hata hivyo mlolongo huo wa mapinduzi uliendelea kwani Hafidhullah Amin alipinduliwa na kisha kuuawa na Babrak Karmal. Katika kipindi cha uongozi wa Babrak, ndipo Afghanistan ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Shirikisho la Umoja wa Sovieti.

Jenerali Abdul Qadir