Jumamosi, 29 Aprili, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria mwafaka na tarehe 29 Aprili 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 341 iliyopita, Peter the Great alichukua madaraka ya nchi huko Russia akiwa na umri wa miaka 10. Peter alikuwa ndugu wa Feodor katika kizazi cha tatu cha Tzar katika ukoo wa Romanov. Baada ya kuchukua madaraka Peter alivuliwa uongozi na dada yake na kubaidishwa katika kijiji kimoja karibu na mji wa Moscow. Baada ya muda Peter aliandaa jeshi kubwa na kwenda kupambana na dada yake. Katika vita hivyo Peter alishinda na kutawala nchi hiyo kwa mara nyingine. Kadhalika Peter alifanya marekebisho makubwa ndani ya Russia. Peter the Great alifariki dunia mwaka 1725. ***
Katika siku kama ya leo miaka 169 iliyopita, alizaliwa Henri Poincaré, mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi. ***
Miaka 120 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lilichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mijadala yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge. ***
Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Uislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi Waislamu wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kama Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliotawala kwa kipindi cha miaka 623 nchini humo. ***
Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya Waitifaki yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi Waitifaki wa Ulaya vilifanya shambulizi la pamoja dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Benito Musolini. ***
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, alifariki dunia Ludwig Wittgenstein, mwanafalsafa mashuhuri wa Austria. Alizaliwa mwaka 1889 Miladia mjini Vienna, mji mkuu wa nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo ya msingi aliendelea na masomo nchini Uingereza katika fani ya uhandisi. Kukutana kwake na Bertrand Russell, mwanafalsafa mkubwa wa Uingereza kulimvutia sana Ludwig Wittgenstein na kumfanya ajiunge na fani hiyo. Baada ya kusoma kitabu cha Russell alidai kwamba masuala yote ya falsafa yametatuliwa, hata hivyo baada ya miaka kadhaa alitambua kosa lake na mwaka 1929 alifikia daraja ya PHD katika falsafa na kufanikiwa kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Cambridge. Ameacha athari kadhaa katika fani hiyo na moja ya athari hizo ni kitabu cha 'Tafiti za Kifalsafa'.
Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Ordibehesht mwaka 1378 Hijria Shamsia, wawakilishi wa duru ya kwanza ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji nchini Iran walianza kazi zao na siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la Siku ya Mabaraza. Kwa kuzingatia kwamba, katika Uislamu suala la mashauriano na kuwa na fikra moja lina umuhimu mno, katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, Mabaraza yana nafasi muhimu na ni dhihirisho la urada ya wananchi katika mfumo wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi. Katika sheria hiii Mabaraza mbalimbali huchaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuongoza masuala tofauti ya nchi ambapo Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Wanazuoni Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ni miongoni mwa mabaraza hayo. ***