Jumatatu, tarehe Mosi Mei, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 10 Shawwal 1444 Hijria, inayosadifiana na tarehe Mosi Mei, mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1116 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la 'Ibn Muqlah', mwandishi, mchora hati na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji. Alizaliwa mjini Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo kipindi hicho. Akiwa kijana Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Ibn Abbas. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala hao, walipatwa na hasira na hivyo kumtia jela Ibn Muqlah. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi muda punde baadaye. Umashuhuri wake mwingi ulishuhudiwa katika sekta ya uchoraji. Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalat fi Mizaanul-Khat.'

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'. Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, Naser al-Din Shah Qajar, mfalme wanne wa ukoo wa Qajar nchini Iran aliuawa na hivyo kuhitimisha kipindi cha giza cha miaka 50 cha historia ya Iran. Tukio hilo liliandaa uwanja wa kutokea Mapinduzi ya kupigania katiba. Naser al-Din Shah Qajar aliauawa kwa kupigwa risasi na Mirza Reza Kermani mpigania ukombozi. Reza Kerman alikuwa mmoja wa wafuasi wa Sayyid Jamal al-Din Asadabadi. Kipindi kirefu cha utawala wa Naser al-Din Shah Qajar kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu cha historia ya Iran katika zama za utawala wa ukoo wa Qajar.
Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.
Na miaka 18 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo. Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya. Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.