Jumatano, tarehe 3 Mei, mwaka 2023
Leo ni Jumatano tarehe 12 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria sawa na Mei 3 mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1060 iliyopita, yaani sawa na tarehe 12 Shawwal mwaka 384 Hijiria, alifariki dunia Ibrahim Bin Hilal Sabi, mtaalamu wa fasihi na malenga maarufu wa karne ya nne Hijiria. Sabi alizaliwa mjini Baghdad, Iraq ambapo alitokea kuwa na uhodari maalumu katika fani ya mashairi na fasihi. Mwandishi huyo mashuhuri, alitabahari pia katika uga wa elimu za hisabati, nujumu na uhandisi. Kuna athari kadhaa kutoka kwa Ibrahim Bin Hilal Sabi, baadhi zikiwa ni 'Risala katika Elimu ya Pembe Tatu' na 'Risalah katika Elimu ya Nujumu.'

Siku kama ya leo miaka 594 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.
Siku kama ya leo miaka 554 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."
Katika siku kama ya leo miaka 529 iliyopita, sawa na tarehe 3 Mei 1494 Miladia, Christopher Columbus, baharia wa Uhispania aligundua nchi ya Jamaica, huko Amerika ya Kati katika safari yake ya pili ya uvumbuzi ndani ya bara la Amerika. Licha ya tabia ya upendo na maridhiano ya wakazi asilia wa Jamaica na nchi nyingine zilizogunduliwa, lakini Christopher Columbus na watu wengine waliotumwa na Uhispania, waliwafanyia ukatili wenyeji hao wakazi. Kwa utaratibu huo Jamaica ambayo kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia na kwa kuwa na dhahabu nyingi zilizokuwa zikikodolewa macho na Uhispania, ilikoloniwa kuanzia mwaka 1509 Miladia hadi muda unaokaribia karne mbili. Baada ya Uhispiania nchi hiyo pia ilikoloniwa na Uingereza ambapo katika kipindi hicho akthari ya wakazi wake asilia walifukuzwa au kuuawa. Hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake mwaka 1962 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 508 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormuz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormuz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, ikiwemo Bahrain ambayo wakati huo ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Siku kama ya leo miaka 414 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, Iran Bahaud-Din Muhammad Bin Hussein Amili, maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, alimu maarufu wa Waislamu wa elimu ya sheria, mataalamu wa nyota na hisabati. Sheikh Bahai alizaliwa mjini Baalbek, Lebanon mwaka 952 Hijiria katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa viongozi na masheikh wakubwa wa zama hizo. Kwa kuwa na maandalizi ya kielimu msomi huyo aliweza ndani ya kipindi kifupi kufikia daraja la ualimu, huku akibobea pia katika elimu za fiqhi, tafsiri ya Qur'an, hadithi, hisabati, nyota, fasihi na historia. Kuna vitabu kadhaa vya thamani vinavyonasibishwa na msomi huyo ambavyo wataalamu wa historia wameviorodhesha na kufikia 100. Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na 'Jamiu Abbasi' 'Kashkuul' 'Hablul-Matin' 'Tashriihul-Aflaak' na 'Khulaswatul-Hisaab.'
Siku kama ya leo miaka 216 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein (Treaty of Finckenstein) kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India.
Leo ni Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Maadhimisho haya yanalenga kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuwaenzi wadau wa sekta hiyo ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wakitekeleza wajibu na majukumu yao.
Siku hiyo iliainishwa kutokana na pendekezo lililotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Hii leo uhuru wa vyombo vya habari unabinywa na kukandamizwa na baadhi ya tawala za kidikteta na kimabavu zisizopenda kuona ukweli ukiwafikia watu. Katika upande mwingine uhuru wa vyombo vya habari unatumiwa vibaya na baadhi ya nchi hususan za Magharibi kutangaza kila kitu, makala, picha na filamu chafu na zinazokiuka maadili ya kibinadamu. Mwenendo huo umekwenda mbali zaidi kiasi cha kutumiwa uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuvunjia heshima matukufu ya kidini ya mabilioni ya watu kote duniani.
