May 03, 2023 22:01 UTC
  • Alkhamisi, Mei 04, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria iinayosadifiana na tarehe 4 Mei 2023 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 1017 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Siku kama ya leo miaka 120 alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Twaha, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 83. Familia ya msomi huyo mkubwa inatokana na moja ya maulama mashuhuri wa Kiislamu. Sheikh Twaha alizaliwa mjini Najaf, Iraq na kupata elimu kwa mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo yaani Sheikh Murtadha Answari, Sheikh Twaha alitabahari katika elimu ya fiq’hi, usulu fiq’hi, hadithi na tafsiri ya Qur’ani Tukufu.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Mirza Muhamamad Taqi Shirazi Kiongozi wa Mapinduzi ya Iraq alitoa fatuwa ya jihadi dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya Uingereza kutangaza vita dhidi ya utawala wa Othmania mwaka 1914 na kukaliwa kwa mabavu mji wa Basra, maulamaa wakubwa wa Najaf walitoa hukumu ya kukabiliana na mkoloni huyo. Miaka ya baadaye ilishuhudia kujitokeza makundi yaliyokuwa yakipinga uwepo wa Uingereza nchini Iraq.

Mirza Muhamamad Taqi Shirazi

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Nazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kilifikia ukingoni. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, chama cha Nazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka.

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.

yatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi

Tarehe 4 Mei miaka 53 iliyopita wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent katika jimbo la Uhio nchini Marekani waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Gadi ya Taifa na wengine kadha wakajeruhiwa katika maandamano ya Wamarekani ya kupinga vita vya Vietnam. Kuanza mwaka 1969 Wamarekani hususan vijana walizidusha upinzani na maandamano ya kupinga vita na uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Vietnam. Maandamano hayo yalishadidi baada ya kufichuliwa habari ya mauaji ya mamia ya Wavietnam katika kijiji cha My Lai (My Lai massacre) na vilevile mwaka 1970 baada ya kuchapishwa habari ya kupanuka zaidi vita vya Vietnam na kuingia Cambodia.

Mauaji wanafunzi wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Josip Broz Tito, kiongozi wa Yugoslavia na mmoja wa waasisi wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM alifariki dunia. Wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1915, Tito aliyekuwa akipigana dhidi ya Russia alitiwa mbaroni na baada ya kuachiliwa huru akiwa na Wakomonisti alipigana vita dhidi ya utawala wa Tzar. Kwa muda fulani, Tito alikuwa na nafasi muhimu kkatika Chama cha Kikomonisti cha Yugoslavia na alifungwa jela miaka 6 kwa kosa hilo. Tito aliiongoza Yugoslavia kwa muda wa miaka 35. Josip Broz Tito aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuugua kwa muda mrefu. 

Josip Broz Tito

Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita ndege iliyokuwa imembeba waziri wa mambo ya nchi za nje wa Algeria Bin Yahya ilitunguliwa na ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein wa Iraq baada ya kutembelea Iran. Baada ya tukio hilo mjumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiongoza jumbe kadhaa alikwenda kukagua eneo la tukio hilo. Maafisa wa Iran walitangaza kuwa, nyaraka zilizopatikana zilionyesha kuwa, ndege za kivita za Iraq zilikuwa zikiifuatilia ndege hiyo ya Bin Yahya. Shambulizi la ndege za kivita za Iraq dhidi ya ndege iliyokuwa imembeba waziri wa mambo ya nje wa Algeria liliichafua sana sura ya Iraq katika macho ya walimwengu.

Bin Yahya