May 05, 2023 22:35 UTC
  • Jumamosi, 6 Mei, 2023

Leo ni Jumamosi 15 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria mwafaka na tarehe 6 Mei 2023.

Katika siku kama ya leo miaka 1441 ilyopita alizaliwa Abu Tufayl A'mir bin Wathilah Kinani ambaye alikuwa miongoni mwa washairi na mahatibu mashuhuri za zama za awali za Uislamu. Abu Tufail alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na alisuhubiana kwa muda mrefu na Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kushiriki katika vita vya Siffin, Jamal na Nahrawan pamoja na mtukufu huyo. Abu Tufail alifaidika sana na elimu na maarifa ya mtukufu huyo. Mashari mengi ya A'mir bin Wathilah yanamsifu Mtume Muhammad (saw).  ***

Abu Tufayl A'mir bin Wathilah Kinani

 

Siku kama ya leo miaka 1192 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim al Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (as). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu katika kizazi cha Mtume walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu Hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika eneo la Rey na wapezi wa Ahlul Bait (as) kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara. ***

Haram ya mtukufu Abdul-Adhim al Hassani katika mji wa Rey

 

Miaka 196 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosafiana na 15 Mfunguo Mosi Shawwal,aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Taqi Razi Najafi Isfahani katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".***

 

Katika siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, alizaliwa huko Czechoslovakia, Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili na raia wa Austria. Akiwa na umri wa miaka minne alihamia mjini Vienna akiwa na wazazi wake. Aidha alipofikisha umri wa miaka saba alijiandikisha katika chuo kidogo cha udaktari ambapo akiwa na miaka 29 alitokea kuwa tabibu aliyebobea kutibu magonjwa ya akili. Baada ya kutibu wagonjwa kadhaa wenye matatizo hayo alipata uzoefu mkubwa suala ambalo lilimsukuma kufanya majaribio kadhaa katika uga huo. Daktari huyo alifanya utafiti na kutwalii matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa ajili hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis. Sigmund Freud alifariki dunia tarehe 23 Septemba 1939 akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo. ***

Sigmund Freud

 

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani, Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa. ***

Alexander Humboldt

 

Tarehe 6 Mei miaka 141 iliyopita mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch ilitangaza habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimefupisha umri wa zaidi ya watu bilioni moja wiki mbili kabla. Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka. Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prf Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxy inayoshabihiana na Quinine. Prf Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika***

Robert Heinrich Koch