May 12, 2023 22:17 UTC
  • Jumamosi, 13 Mei, 2023

Leo ni Jumamosi 22 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria mwafaka na tarehe 13 Mei 2023 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 293 iliyopita aliaga dunia Muhammad Hussein Khatunabadi aliyekuwa alimu na msomi mkubwa wa Kiirani. Alikuwa hodari katika fiqhi, fasihi na elimu ya Hadithi na alikusanya na kuandika Hadithi nyingi za Mtume (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni Najim al-Thaqib na al Al-wah al-Samawiyyah. ***

Muhammad Hussein Khatunabadi

 

Siku kama ya leo miaka 310 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa. Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa. Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanja tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765. ***

Alexis Cloude Clairaut

 

Miaka 116 iliyopita katika kama ya leo, alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na thamthiliya wa Kiingereza. Maurier alizaliwa katika familia ya wanasanaa na iliyokuwa pia na wanafasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889. ***

Bi Daphne du Maurier

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano yasiyosita ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sheria za mkataba huo, raia wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumhukumu raia wa Marekani aliyekuweko Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa katika nchi yao. ***

Capitulation