Jumapili, tarehe 14 Mei, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 23 Shawwal 1444 Hijria sawa na tarehe 14 Mei 2023.
Siku kama ya leo miaka 448 iliyopita, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno. Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuidhibiti nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kupigania uhuru wa nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru.
Katika siku kama ya leo miaka 332 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.
Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, chanjo ya kwanza kabisa ya ugonjwa wa ndui ilitolewa nchini Uingereza. Japokuwa hii leo ugonjwa huo umetoweka katika maeneo mengi ya dunia hususan katika nchi zilizoendelea, lakini hadi kufikia karne ya 18, maradhi hayo yalienea sana ndani ya mataifa mengi na kusababisha madhara makubwa. Mwaka 1717 mwanamke mmoja wa Uingereza alianzisha utafiti na uchunguzi mkubwa katika suala hilo, ambapo juhudi zake zilipunguza sana idadi ya waathirika wa maradhi hayo. Hatimaye tarehe 14 Mei mwaka 1796 Dakta Edward Jenner aliifanyia majaribio chanjo ya ndui kupitia mwili wa mtoto mdogo na kutoa majibu mazuri.
Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, nchi ya Paraguay ilijipata uhuru wake. Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kulishudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyeingia madarakani aliongoza kidikteta. Uchaguzi wa kwanza huru wa rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia.
Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, Joseph Reinaud, msomi na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufarasa. Kutokana na kupendelea sana lugha za eneo la Mashariki ya Kati, alianza kujifunza lugha na fasihi ya Kiarabu. Baada ya muda mfupi, Joseph Reinaud alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo kikuu nchini Ufaransa. Aliandika vitabu kuhusiana na historia ya Uislamu ambapo moja ya vitabu hivyo ni 'Fat'hul-Arab' na 'Al-Islamu wal-Muslimin.
Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, Ayatullah Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu, katika hatua ya kukabiliana na ukoloni wa Uingereza, alitoa fatwa ya kuharamisha utumiaji tumbaku nchini Iran. Katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar Uingereza ilikuwa ikiongeza satwa yake nchini Iran kwa kufungua makampuni ya tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini hapa. Fatua hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika fatwa hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.
Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, utawala bandia wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya Wapalestina. Askari wa Uingereza waliikalia kwa mabavu Palestina kufuatia kushindwa utawala wa Othmania wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Miaka mitano baadaye Jumuiya ya Kimataifa iliikabidhi Palestina kwa Uingereza na kuiweka chini ya mamlaka ya mkoloni huyo. Novemba mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio lililotaka kuundwa madola mawili ya Kiarabu na Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.
Na siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, mkataba wa kisiasa na kijeshi wa Warsaw ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw, lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya magharibi waitifaki wa Marekani. Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary.