May 22, 2023 08:19 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 842 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 17 na 18 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَن يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّـهِ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ ۚ فَبَشِّرْ عِبَادِ

Na wale wanao jiepusha na ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu.

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ

Ambao husikiliza maneno, wakafuata lililo bora yao. Hao ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.

Katika aya hizi tulizosoma, Qur'ani tukufu imetumia tena mbinu ya ulinganishaji. Kama mnavyokumbuka, katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia washirikina, ambao kwa sababu ya taasubi na ukaidi waliokuwa nao, hawakuwa tayari kuikubali haki na kumwamini Allah SW. Kinyume na watu hao, aya tulizosoma zinawazungumzia waja wenye kiu ya kuitambua haki, ambao pale haki inapowabainikia huikubali, wakarejea kwa Mwenyezi Mungu na kupata rehma zake Mola. Hata hivyo imani ya kweli inathibiti kwa kujiepusha na kuabudu kingine chochote kile ghairi ya Allah SW. Yawe ni masanamu ya miti au mawe, matamanio ya ndani ya nafsi ya mtu au kuwatii watawala madhalimu na waovu. Neno tughyan lina maana ya kuvuka kiwango na kupindukia mpaka; na katika misamiati na mafundisho ya Qur'ani, kujiepusha na taghuti maana yake ni kujiweka mbali na kila aina ya shirki ya kuabudu masanamu na matamanio ya nafsi na kutowatii wala kusalimu amri mbele ya watawala madhalimu na madola ya kibeberu na ya utumiaji mabavu. Kisha aya zinaashiria kundi maalumu la waja wa Mwenyezi Mungu, ambao huacha ukaidi usio na msingi na kuweka kando taasubi zisizo na maana, wakawa tayari kusikiliza kauli tofauti, kisha kwa kutumia akili na busara, wakachagua kufuata iliyo bora zaidi miongoni mwao. Hao ni watu wenye kiu ya kujua ukweli. Popote pale wanapokutana na haki huilaki kwa mikono miwili na kuikumbatia kwa ujudi wao wote, wakachota maji ya ukweli kwenye chemchemi yake mpaka kiu zao zikapozeka. Wao sio tu ni watafutaji haki, lakini kati ya mengi ya sawa wanayoyasikia, huchagua na kufuata yaliyo bora zaidi miongoni mwao. Kwa hakika aya hizi zinaashiria sifa ya uhuru wa kufikiri na kuchagua katika masuala mbali mbali, waliyonayo Waislamu. Watu wenye busara, badala ya kusimama dhidi ya maneno ya haki, huyasikiliza waambiwayo, na pale linapowabainikia la haki husalimu amri na kulifuata. Na hiyo ni alama ya ukomavu wa akili na busara. Kwa mujibu wa Qur'ani, hao ni watu walioongolewa na Allah na wenye akili na busara. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sharti la imani ya kweli juu ya Allah ni kujiepusha na kuwatii mataghuti na kujiweka mbali nao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tunapokutana na hoja na kauli tofauti, tunachopaswa kuzingatia ni muhtawa na yaliyomo ndani yake, si watoaji wa kauli hizo wala hadhi na shakhsia zao. Kisha tuchague na kufuata iliyo bora kati ya kauli na hoja hizo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, hakuna mgongano wala mkinzano baina ya akili katika upande mmoja, na wahyi na mafundisho ya dini katika upande mwingine. Vyote hivyo viwili ni hoja za Allah na mwongozo wa kumuelekeza mtu kwenye saada na uokovu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, Uislamu unaunga mkono uhuru wa kufikiri na kuchagua kwa uelewa njia ya maisha, kwa kutegemea akili na mantiki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 19 na 20 ambazo zinasema:

أَفَمَنْ حَقَّ عَلَيْهِ كَلِمَةُ الْعَذَابِ أَفَأَنتَ تُنقِذُ مَن فِي النَّارِ

Je! Yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, je, wewe unaweza kumwokoa aliyemo Motoni?

لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ غُرَفٌ مِّن فَوْقِهَا غُرَفٌ مَّبْنِيَّةٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَعْدَ اللَّـهِ ۖ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ الْمِيعَادَ

Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa zilizo jengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.

Kwa kuwa Bwana Mtume SAW alikuwa akitamani sana watu wote waongoke na waokoke, wakiwemo wapotofu na washirikina, kiasi cha kusononeshwa mno na kung'ang'ania kwao njia ya upotofu, aya hizi tulizosoma zinamhutubu mtukufu huyo kwamba: Hivi unadhani utaweza kuwaokoa na moto watu waliohitari kuingia motoni kutokana chaguo batili walilofanya kwa hiari yao wenyewe? Haiwezekani abadani! Wao walioamua kukata njia zote za mawasiliano baina yao na Mola wao, hawana njia yoyote ya kuokoka. Hata Mtume pia hana njia ya kuweza kuwasaidia. Lakini kinyume na kundi la watu hao, wale watu waumini na wamchao Mwenyezi Mungu, watakuwa na utukufu Siku ya Kiyama na wataneemeshwa kwa mabustani na makasri ya peponi. Maisha yao huko peponi hayatakuwa ya tabu, huzuni wala maudhi yoyote, bali watakuwa katika starehe, raha na amani kamili. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jukumu la asili walilopewa Mitume ni kuwaelekeza na kuwaonyesha watu uongofu na njia sahihi ya maisha. Lakini saada na kufuzu kwa wanadamu hakuko mikononi mwa Mitume, bali kunategemea mwenendo na matendo ya watu wenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu mwenye taasubi, inadi na ukaidi hujifungia mwenyewe njia ya kuitambua haki; na kwa kufanya hivyo anajinyima mwenyewe saada na uokovu wa duniani na akhera. Vile vile tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, kama kweli tunamwamini Allah, inatupasa tuamini kwa yakini ahadi zake kuhusu Pepo na Moto na kuchunga amali na matendo tunayofanya.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21 ambayo inasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَلَكَهُ يَنَابِيعَ فِي الْأَرْضِ ثُمَّ يُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَجْعَلُهُ حُطَامًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ

Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano, na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye akili.

Baada ya kufanywa ulinganishaji mdogo tu baina ya mwisho wa waumini na makafiri, aya tuliyosoma inarejea tena kuzungumzia tauhidi na kufufuliwa kwa viumbe, ambapo katika hoja za tauhidi imegusia kuteremshwa kwa mvua kutoka mawinguni. Na sababu ni kwamba maisha ya ardhini yanategemea unyeshaji wa mvua hizo. Laiti kama usingekuwepo mfumo huo, yaani kugeuka mvuke maji ya bahari na kufanyika mawingu; kisha mawingu hayo yakasambaa kuelekea pande tofauti za ardhi na kunyesha katika sura ya theluji na mvua, maeneo mengi ya ardhini yangekuwa makavu yabisi bila ya maji, na maisha yangekuwa magumu au muhali kwa viumbe wa ardhini. Hata wakazi wa pwani za bahari na bahari kuu, nao pia wasingeweza kujidhaminia maji wanayohitajia kwa ajili ya kunywa na kwa kazi zao za kilimo; kwa sababu maji ya bahari yana chumvi na madini mengine chungu nzima, kiasi kwamba haiwezekani kuyabadilisha ladha yake yakanyweka pasi na kutumia mitambo maalumu ya uchujaji yenye gharama kubwa kifedha. Lakini kwa kuwa maji mengi zaidi kati ya hayo huwa yanatumika kwa ajili ya kilimo, hailipi kutumia gharama zote hizo ili kuyafanyia uchujaji. Lakini tatizo hilo la chumvi na madini linatatuliwa kwa namna ya kustaajabisha katika mfumo wa maumbile. Wakati maji ya bahari yanapogeuka mvuke na kuelekea juu angani, madini na takataka zingine za ziada huwa hazigeuki mvuke. Kwa hiyo maji hayo yaliyogeuka mvuke yanayokuwa yamechujwa na kusafishwa huteremka tena chini kwa sura ya mvua na theluji yakiwa ni maji safi na matamu yaliyo tayari kutumika kwa ajili ya kunywa. Hakuna shaka yoyote kuwa hiyo ni tadbiri na upangaji mambo wa Muumba wa ulimwengu ambaye anatumia utaratibu wa kimaumbile kuyafanya maji yawe safi na matamu kwa kuyachuja madini na takataka zingine ili yaweze kutumiwa na wanadamu na viumbe wengine hai. Matone ya maji ya mvua huhifadhiwa kwenye mahodhi ya chini ya ardhi; na madonge ya theluji hukusanyika na kuganda juu ya migongo ya milima, kisha baada ya muda kupita huchimbuka kwa sura ya chemchemi na visima na kutiririka kwa njia ya mito ili yaweze kutumiwa kwa mahitaji mbali mbali. Wakati mwanadamu anapoitafakari neema hii kubwa ya Mwenyezi Mungu, ambayo ni chanzo cha uhai wa mwanadamu, viumbe vingine vyenye uhai pamoja na miti na mimea iliyoko ardhini, ndipo anapoelewa barabara adhama na utukufu wa Mola Muumba wa ulimwengu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, utambuzi wa vitu mbali mbali vya maumbile na kutafakari kwa makini juu ya uumbaji wake ni mojawapo ya njia za kumjua Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo haipasi kughafilika na hilo tukawa tunavipita vitu hivyo bila kujali wala kutafakari. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kutokana na maji na udongo wa aina moja inaota miti na mimea mbali mbali inayotoa maua na matunda ya rangi na ladha tofauti; na hiyo ni moja ya ishara za qudra na adhama ya Mola Muumba. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba miongoni mwa alama za akili na busara ni kwa mtu, mbali na kuwa na utambuzi wa vitu vya maumbile, kufuatilia na kuelewa pia chimbuko na asili ya vitu hivyo na ulimwengu mzima wa maumbile. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 842 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuutafakari uumbaji wake na kuifanya tafakuri hiyo sababu ya kuifikia elimu na imani ya yakini juu yake Yeye Mola. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/