Sura ya Fuss’ilat, aya ya 19-23 (Darsa ya 877)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 877 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 na 20 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ
Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao watazuiliwa (wasubiri waunganishwe na wenzao).
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia adhabu zilizowapata madhalimu na wahalifu wa amri za Mwenyezi Mungu hapa duniani. Aya hizi tulizosoma zinazungumzia adhabu itakayowafika watu hao akhera kwa kueleza kwamba, watu wanaowapinga Mitume wa Mwenyezi Mungu na mafundisho yao na wakachukua hatua dhidi yao, hao kwa hakika ni maadui wa Mwenyezi Mungu; na wameamua kukabiliana na Yeye Mola. Kwa hivyo Siku ya Kiyama wataongozwa kwenda kutiwa motoni mithili ya wahalifu waliopangwa kwenye safu moja kwa ajili ya kupelekwa gerezani. Ni wazi kwamba wakati mtu mwovu na mhalifu atakapouona moto atataka kujitoa hatiani kwa kukana na kulalamika. Qur’ani tukufu inasema: Wakati huo viungo vya miili ya watu waovu yakiwemo masikio, macho pamoja na ngozi zao zitatamkishwa na kutoa ushahidi dhidi yao; ushahidi ambao haitayumkinika kuukana kwa njia yoyote ile; kwa sababu mashahidi hao ni viungo vya mwili wa mtu mwenyewe. Walikuwa pamoja naye kila mahali huku wakishuhudia kila kitu, kwa hivyo viungo hivyo vitatoa ushahidi dhidi yake. Ushahidi huo wa Siku ya Kiyama unaonyesha kuwa, yote ayasemayo na ayatendayo mtu hapa duniani yanarekodiwa na kuhifadhiwa na nafsi yake mwenyewe na athari zake zinasalia kwenye mwili na viungo vyake. Ukweli ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya aibu kubwa; ni siku ambayo mwili mzima wa mwanadamu utatamkishwa; na siri zake zote zitafichuka. Waovu na wafanya madhambi watapatwa na hofu kubwa na mshtuko wa ajabu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, shirki na ukafiri vina viwango, kikiwemo cha mtu kufika hadi, badala ya kumkanusha tu Mwenyezi Mungu akaanzisha uadui pia na Muumba huyo wa ulimwengu. Kutokana na inadi na uadui wake dhidi ya haki, mtu kama huyo hula njama na kuchukua hatua dhidi ya Kitabu cha Allah na mafundisho ya Mitume wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutoa ushahidi viungo vya mwili kunamaanisha kwamba, viungo hivyo vinaelewa yote yafanywayo na mwanadamu hapa duniani na vitakwenda kuyaeleza Siku ya Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21, 22 na 23 za sura yetu ya Fuss'ilat ambazo zinasema:
وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ
Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda.
وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ
Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa waliopata hasara.
Baada ya viungo vya mwili kutoa ushahidi dhidi ya waovu, watu hao wataaibika na kufedheheka sana na kuamua kuvifokea viungo vyao kwa kuviuliza, kwa nini mnatoa ushahidi dhidi yetu? Kwani nyinyi si mikono, miguu, macho, masikio na ngozi zetu? Hatukupitisha miaka na miaka pamoja nanyi na tukakutunzeni na kukuenzini? Inakuwaje basi, leo mnasema maneno kama haya dhidi yetu? Jibu vitakalotoa viungo litakuwa zito na la wazi, pale vitakaposema: Sisi hatusemi kwa matashi yetu, bali Mwenyezi Mungu, Mola aliyekuumbeni akakuleteni duniani, kisha akakufufueni baada ya kukufisheni, na akakisemesha kila kitu, ndiye aliyetutamkisha sisi pia kwa irada yake. Wakati mlipokuwa mkiambiwa duniani kwamba Mungu yuko, Naye ni mjuzi wa mnayoyafanya, na wala hakuna kinachofichika kwake Yeye, hamkuwa mkiamini. Mlikuwa mnadhani Mwenyezi Mungu hayajui mengi ya mliyokuwa mkiyafanya. Hamkufikiria kama hata sisi pia tunashuhudia maneno na matendo yenu na iko siku tutakuja kutamka na kutoa ushahidi dhidi yenu. Kwa sababu hiyo mlikuwa mkifanya madhambi mbali na macho ya watu bila kujua kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe anazijua siri zenu, za ya dhahiri na batini na anaowatuma pia wako na nyinyi kila mahala, na wanayaona mnayoyafanya. Ukweli ni kwamba sisi viungo vya mwili tulikuwa mashahidi na waangalizi wa amali zenu. Vyovyote itakavyokuwa, imani potofu mliyokuwa nayo juu ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyokufanyeni leo mharibikiwe na mhasirike. Inafaa tuashirie pia hapa kuwa, usemaji hauvihusu viungo vya mwili pekee, kwani Siku ya Kiyama si viungo vya mwanadamu tu vitakavyosema, kwa sababu ndani ya Qur’ani tukufu umeashiriwa pia usemaji wa mbingu na ardhi pamoja na moto wa Jahanamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, hakika hasa ya mwanadamu ni roho yake; na mwili ni wenzo aliokabidhiwa na kuwekwa kwenye mamlaka yake. Kwa hiyo Siku ya Kiyama viungo vya mwili huo vitaweza kutoa ushahidi dhidi ya hakika hiyo ya mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mashahidi wa Siku ya Kiyama wataripoti na kutoa ushahidi wao kwa umakini na usahihi kwa namna ambayo hautaweza kukanushika. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, vitu vyote vilivyotuzunguka pamoja na viungo vya miili yetu, ambavyo kidhahiri vinaonekana viko kimya na havina sauti, siku Allah atakapotaka ,vitakuja kusema na kutoa ushahidi kwa viliyoyashuhudia. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, watu waovu wanapata uthubutu na ujasiri wa kufanya madhambi kwa sababu wanaghafilika kuwa viungo vya miili yao ni mashahidi wa yale wayafanyayo. Ukweli ni kwamba ikiwa mwanadamu atajitambua kuwa katika muda wote na popote pale anapokuweko, huwa anaonekana na Mwenyezi Mungu, ambaye kwake Yeye hakuna tofauti yoyote kati ya vinavyoonekana na vilivyofichikana, katu hatofanya dhambi na kumwasi Mola wake. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, imani potovu na isiyo sahihi anayokuwa nayo mtu kuhusu Allah SWT ndio chanzo cha kiumbe huyo kuporomoka, kuangamia na kuhasirika. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 877 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/