Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 63-69 (Darsa ya 905)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 905 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 63 na 64 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَلَمَّا جَاءَ عِيسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ قَالَ قَدْ جِئْتُكُم بِالْحِكْمَةِ وَلِأُبَيِّنَ لَكُم بَعْضَ الَّذِي تَخْتَلِفُونَ فِيهِ ۖ فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ
Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.
إِنَّ اللَّهَ هُوَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia mtazamo potofu wa Wakristo juu ya Nabii Isa (as) wa kumuitakidi kuwa ni mwana wa Mungu na hivyo kumpa utakatifu wa kiungu na kumwabudu. Aya tulizosoma zinaashiria yaliyomo kwenye wito na ujumbe alioufikisha Mtume huyo mteule kwa watu wake na kueleza kwamba: Masih (as), kama walivyokuwa Mitume wengine, naye pia alionyesha miujiza kadhaa ili iwe hoja na ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa unabii wake. Aliwalingania watu kwa hekima, yaani, alizibainisha imani na itikadi za wito wa haki kwa kutumia mantiki sahihi ili watu wote waweze kuzifahamu na kuzikubali na kuepukana na kila aina ya upotofu katika fikra na itikadi. Hikma, tab'an, inajumuisha uga wa amali na matendo pia, ambao ni wa kuzitakasa akhlaqi za watu kwa kujisafisha na kujiweka mbali na hulka chafu na kujipamba kwa tabia na maadili safi na mema. Ni wazi kwamba kuhusiana na tofauti zinazojitokeza pia kati ya watu juu ya mambo mbalimbali, inawezekana kutumia hikma kwa ajili ya kuwasuluhisha na kutoa hukumu sahihi inayoweza kutetewa na kukubalika. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, Nabii Isa (as) aliyapinga na kuyakanusha madai yote ya kumfanya yeye mwabudiwa, alipowaambia watu wake kwamba: hapana shaka Mwenyezi Mungu ni Mola wangu mimi na Mola wenu nyinyi pia. Kwa kauli yake hiyo, Nabii huyo mteule aliwabainishia watu wake kwa uwazi kabisa kuwa, mimi na nyinyi tuko sawa; na Mola wetu pia ni mmoja. Na mimi pia, kama mlivyo nyinyi, ninamhitaji katika hali zangu zote Muumba na wa kunipangia kila jambo. Na Yeye Allah ndiye Mwongozaji wa mambo yangu. Yeye ni Mola Mlezi wa viumbe wote; mwabuduni Yeye tu; hakuna yeyote wa kustahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Na katika kukamilisha ujumbe wake, Nabii Isa (as) akasema: njia sahihi na iliyonyooka ni njia hii ya kudhihirisha uja na kumwabudu Mola Muumba; njia ambayo haijapinda wala kwenda upande hata chembe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wito wa Mitume uliendana na hikma na hoja wadhiha na za wazi kabisa; ili kwa kutumia akili na tafakuri, watu waweze kuufahamu na kuukubali ukweli usio na shaka wa wito huo wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, njia ya kuondoa na kumaliza tofauti za kidini na kijamii ni kurejea kwenye mafundisho yenye thamani ya kipekee ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na kuacha kung'ang'ania utashi wa binafsi na wa kimakundi. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, ujumbe mkuu wa wito wa Nabii Isa (as) ulikuwa ni kuwalingania watu imani ya Tauhidi, ya kumwamini na kumwabudu Mungu mmoja na pekee wa haki. Ibada inamstahikia yule tu aendeshaye na kusimamia mambo yote; na kumuabudu mtu au kitu chochote kile ghairi ya Allah SWT ni kuelekea kwenye dhalala na upotofu. Kwani hakuna mtu yeyote mwenye kustahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, hata kama mtu huyo atakuwa Mtume, ambaye uzawa wake ni wa kimiujiza.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 65 hadi 67 za sura yetu ya Az-Zukhruf ambazo zinasema:
فَاخْتَلَفَ الْأَحْزَابُ مِن بَيْنِهِمْ ۖ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ عَذَابِ يَوْمٍ أَلِيمٍ
Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ
Hawangoji ila Saa iwajie ghafla na wala wao hawatambui?
الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ
Siku hiyo marafiki watakuwa maadui wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu.
Nabii Isa (as) alibaathiwa na kupewa Utume kwa ajili ya kaumu ya Bani Israil. Lakini kundi moja miongoni mwa watu hao walimkadhibisha kwa kumwita muongo na kuukataa ujumbe aliowafikishia. Mkabala na watu hao, kundi jengine katika Bani Israil walifurutu mpaka katika kumkuza na kumtukuza Masih (as). Walimpandisha daraja kutoka ya Utume na kumfikisha kwenye daraja ya Uungu. Walimchukulia Nabii huyo mteule kuwa ni 'mungu' aliyeshuka ardhini kutoka mbinguni, akadhihiri katika umbo la mtu. Baadhi yao walimtaja Nabii Isa kama moja ya madhihirisho matatu ya Uungu. Na hatimaye, imani na itikadi ya Utatu na miungu mitatu ilipata nguvu katika Ulimwengu wa Ukristo; na kama tunavyoshuhudia siku hizi, akthari ya Wakristo wanaamini imani hiyo ya Utatu. Hali hii ya kufurutu kiimani, katika kumshusha au kumpandisha hadhi Nabii Isa (as) ilijiri wakati yeye mwenyewe alikuwa akijitambulisha kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu na akawalingania watu kumwabudu Mola mmoja tu na wa pekee wa haki. Kwa hivyo sehemu inayofuatia ya aya inasema: ole wao wale waliodhulumu na kuikengeuka njia iliyonyooka. Wao wameifanyia dhulma hadhi na daraja ya Utume na watapatwa na adhabu ya Moto Siku ya Kiyama. Hivi wao wanatarajia nini kwa kumnasibishia Mtume wa Mwenyezi Mungu mambo yasiyo sahihi? Wanatarajia kitu kingine ghairi ya kufikiwa ghafla na Kiyama? Naam, mauti na Kiyama vitawashtukiza watu kama hao, pasi na kuwa wamejiandaa na bila kutarajia kuwa kitawafika na kuwanyakua. Kutokana na aya hizi inatubainikia kwamba, tukio zito na lenye mtikisiko wa kipekee la Kiyama lina sifa mbili maalumu: ya kwanza ni kujiri kwake kwa ghafla mno; na ya pili ni kushtukizwa watu na kuwatokezea wakiwa hawajajiandaa wala kujiweka tayari kukabiliana nalo. Kisha aya zinaendelea kuelezea hali ya Siku ya Kiyama na kusema: siku hiyo mahusiano yasiyo na mfungamano na Mwenyezi Mungu yatakatika. Marafiki na jamaa waliokuwa na usuhuba na ukuruba kwenye mambo ya dhulma, madhambi na maovu, watakuwa na uadui baina yao. Kila mmoja atamwona mwenzake kuwa ndiye sababu ya yeye kupotoka na kuhasirika siku hiyo; na atamwambia: wewe ndiye uliyenipotosha, ukanipambia na kunifanya niipende dunia; na ni kwa sababu ya urafiki na kulahikiana na wewe, leo nimefikwa na mwisho huu mbaya. Lakini wale watu ambao walipokuwa duniani, urafiki baina yao na uadui wao na watu ulikuwa ni kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu, hao ndio pekee ambao urafiki wao utaendelea Siku ya Kiyama na wala hautageuka uadui wa kuapizana na kulaaniana. Kwa kuwa urafiki wa wachamungu unafungamana na msingi wa thamani zinazodumu milele, mafungamano yao hayo pia, yanaendelea na kudumu milele. Tab'an matunda makubwa zaidi ya urafiki huo yatadhihirika zaidi Siku ya Kiyama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujiri kwa tukio la Kiyama kutakuwa kwa ghafla na kwa kushtukiza; na hakuna mtu yeyote, hata Mitume, ajuaye wakati wa kutokea kwake. Mwenye ujuzi wa hilo ni Allah SWT peke yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama usuhuba na mafungamano ya duniani hayataendana na malengo ya akhera, Siku ya Kiyama yatakuwa sababu ya uadui baina ya watu. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, urafiki na waumini wa kweli ni endelevu na wa kudumu milele; kinyume na urafiki na watu wengine, ambao hauaminiki na wala hauna dhamana ya kudumu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 68 na 69 ambazo zinasema:
يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ
Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
الَّذِينَ آمَنُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا مُسْلِمِينَ
Ambao waliziamini Ishara zetu na wakawa Waislamu.
Hapa duniani, wachamungu ni watu ambao kiitikadi, wana imani imara na thabiti; na kwa upande wa amali pia wanajisalimisha na kutii kikamilifu amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nyoyo zao haziingiwi na chembe ya shaka juu ya ukweli wa aya za Mola wao, na nafsi zao haziyumbishwi na hawaa na matamanio ya nafsi. Hao ndio watu wanaopewa bishara na Allah SWT kwamba Siku ya Kiyama hamtakuwa na hofu wala wasiwasi wowote; na wala haitakupateni huzuni kwa yaliyopita, wala hamtakuwa na wasiwasi kuhusu hatima na mustakabali wenu. Ni ujumbe ulioje?! Ujumbe utokao moja kwa moja kwa Mola, ambao unafuta kikamilifu ndani ya moyo wa mtu huzuni na majonzi kwa yaliyopita; na hofu na wasiwasi juu ya mustakabali. Naam, hivyo ndivyo ilivyo! Mtu ambaye muda wote anajali kutelekeza jukumu na wajibu wake, hata kama hatafanikiwa kikamilifu, hahisi kuwa ameharibikiwa na wala haingiwi na hofu na tafrani. Anajisalimisha kwa Allah, akiwa na matumaini ya kupata rehma zake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa mja halisi wa Allah na kujisalimisha kwake na kutii maamrisho yake, ndio njia ya kuufikia utulivu wa kweli na kupata kinga ya kuepukana na hofu na mfadhaiko wa matukio ya kutisha ya Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, imani peke yake haitoshi; lazima iambatane na matendo na mtu kujisalimisha na kutii amri za Allah SWT. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 905 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa Waislamu wa kweli tunaomcha Yeye kwa namna hasa inayostahiki; na atuepushe na hofu na huzuni ya siku nzito ya Kiyama. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/