May 24, 2023 17:02 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 914 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 44 ya ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 51 hadi 55 ambazo zinasema:

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ

Hakika wachamngu watakuwa katika mahala pa amani. 

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ

Katika mabustani na chemchem. 

يَلْبَسُونَ مِن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَقَابِلِينَ

Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, 

كَذَٰلِكَ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ

Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza Mahurilaini.

يَدْعُونَ فِيهَا بِكُلِّ فَاكِهَةٍ آمِنِينَ

Humo watataka (na watapata) kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.

Katika darsa iliyopita tulizungumza machache kuhusu hali watakayokuwa nayo huko Motoni madhalimu na wafanya madhambi. Mkabala wake, aya tulizosoma zinabainisha hali za wachamungu Peponi na kueleza kwamba: makazi yao wao yatakuwa ya amani kamili. Ni amani ya kuepushwa na kila aina ya ghamu, huzuni, machungu, misiba na mateso. Kwa hakika hiyo hisia tu ya kuwa katika amani na usalama, yenyewe ni neema kubwa kabisa ya Mwenyezi Mungu, ambayo hata hapa duniani pia anapomneemesha nayo yeyote katika waja wake, huishi kwa raha na utulivu. Mahali watakoishi watu wa Peponi kutakuwa na anuai za mabustani zipitayo kando yake chemchem na maporomoko ya maji ya namna kwa namna, vitu ambavyo vitawachangamsha na kuwaburudisha mno, kiasi kwamba wingi na utofauti wa vitu hivyo utawafanya watu hao wa peponi wasichoke wala kuishiwa na hamu ya neema hizo watakazojaaliwa. Hapa duniani, nguo za hariri ni maarufu na zinasifika kwa uzuri, ulaini na unyororo wake. Allah SWT ameahidi kuwapatia nguo na mavazi hayo watu wa peponi huko akhera. Na bila shaka rangi, mapambo, usanifu na nakshi zake zitakuwa za sura na namna tofauti kiasi cha kubakisha muda wote uzuri, upya na mvuto wake. Nyoyo za watu wa Peponi zitazoeana na kuungana pamoja. Wataketi na kujumuika pamoja huku hali ya furaha, upendo na umaanawi wa namna ya kipekee ukitawala baina yao, wakielekeana kwa pamoja pasi na yeyote miongoni mwao kujikweza na kujiona bora mbele ya mwenzake. Na kwa kuzingatia kwamba huko akhera pia watu watajaaliwa kuwa na matamanio na ghariza za kimwili, Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaozesha watu wa peponi wake wenye jamali na uzuri wa kipekee, ambao sisi tunaoishi duniani hatuwezi katu kuuwaza wala kuufikiria namna ulivyo. Kwa kuwa waja hao wema waliyapeusha macho yao hapa duniani kuangalia wasio maharimu zao na wakazilinda tupu zao na machafu, Mwenyezi Mungu atawafidia huko akhera malipo hayo bora kabisa ya kuwaozesha mahurul-aini. Kwa kuzingatia kuwa matakwa na mahitaji mengine ya kimwili ya mwanadamu ni kula na kunywa, kila watakachotamani waja wema watakuta wameandaliwa huko peponi. Kutakuweko na matunda ya aina kwa aina; na si ya kungojea msimu wake maalumu ufike, bali yatakuwepo muda wote mitini, tayari kwa ajili ya kuchumwa na kuliwa. Matunda hayo yenye rangi za kila aina na ladha na utamu wa kila namna, yatakuwepo muda wote na wala mtu hatopata tabu au usumbufu wowote wa kuyachuma. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, utulivu na amani kamili ni moja ya neema muhimu zaidi za Allah zilizoashiriwa kuwepo huko peponi kabla ya neema nyinginezo. Huko hakutakuwepo na hofu ya kufikwa na hatari au dhara yoyote, wala wasiwasi wa kuchelea kufikwa na mauti na kuzipoteza mtu neema alizojaaliwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na taqwa na uchamungu kwa kujiepusha na kujiweka mbali na mambo ya haramu na yasiyofaa ndiko kutakakomfikisha mtu kwenye pepo tukufu ya Mwenyezi Mungu. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, yale ambayo mtu alikatazwa kuyafanya hapa duniani kutokana na madhara yaliyonayo na yeye akajizuilia na kujiepusha nayo, atakwenda kufidiwa kwa malipo bora peponi huko akhera. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, watu wa peponi watajumuika pamoja kirafiki na wataliwazika na kuburudika kwa vikao na maongezi watakayofanya baina yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 56 na 57 ambazo zinasema:

لَا يَذُوقُونَ فِيهَا الْمَوْتَ إِلَّا الْمَوْتَةَ الْأُولَىٰ ۖ وَوَقَاهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ

Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu.

فَضْلًا مِّن رَّبِّكَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

(Hayo yote) ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Moja ya madukuduku makubwa zaidi na ya muda wote aliyonayo mwanadamu hapa duniani ni suala la mauti. Mauti ni sababu ya mtu kutengana na jamaa na marafiki zake na kila akipendacho. Lakini Allah SWT ameahidi kuwa watu wa peponi hawatokufa tena na watabaki hai milele. Kubaki hai milele huko kwa watu wa peponi kumetajwa katika aya kadhaa za Qur’ani tukufu kwa maneno “Khaalidiina Fiihaa”, yaani watabaki humo milele. Na si tu watu wa peponi hawatafikwa na mauti ya kuwafanya watenganishwe na pepo yao, lakini pia hawatahamishwa katu peponi na kupelekwa motoni. Yamkini baadhi ya watu kutokana na madhambi yao, kwanza wataingizwa motoni, lakini baada ya kusafishwa nyoyo na roho zao taka na kutu za madhambi watapelekwa peponi, lakini haitatokea kinyume chake kwa watu wa peponi. Alaa kulli haal, watu watakaoingizwa peponi watakuwa wamerehemewa na Allah kwa ukarimu wake na kuwaepusha na adhabu ya moto. Kwa hiyo hawatakuwa na wasiwasi wa kufikwa na adhabu yoyote. Aya tulizosoma zinaashiria nukta moja muhimu kwa kusema: neema zote hizo zitatokana na fadhila na rehma za Mwenyezi Mungu. Sababu ni kwamba ilivyo hasa na kwa amali haba na zenye ukomo wazifanyazo waja, hawastahiki kulipwa na Allah SWT neema zote hizo za milele na zisizo na ukomo. Lakini kwa rehma na ukarimu wake, Mola Raufu na Mrehemevu atawapa waja wake waliomcha na wema neema hizo ambazo haziwezi kutasawirika na kufikirika na watu wa dunia hii. Alaa kulli haal, kupata malipo yote hayo ni kufuzu kukubwa mno kwa watu wa peponi ambako hakupatikani isipokuwa kwa rehma za Allah SWT. Miongoni mwa tunayojielimisha kutokana na aya hizi ni kwamba, yeyote atakayeingia peponi, hatatoka, bali atabaki humo milele. Allah atujaalie kuwa katika hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kila yule ambaye hapa duniani aliyadhibiti matamanio ya nafsi yake na kujiepusha na madhambi, Allah SWT atamhifadhi na kumlinda na adhabu ya Moto. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, mema tuyafanyayo hapa duniani ni machache na yana kikomo na wala hayawezi kulinganishwa na neema adhimu za Mwenyezi Mungu katika pepo yake ya milele. Kwa hiyo Pepo na neema watakazopata ndani yake waja wema zitatokana na rehma na fadhila za Allah na si wao kuwa na haki ya kuyapata hayo kwa Mola.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 58 na 59 za sura yetu hii ya Ad-Dukhan ambazo zinasema:

فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Basi tumeifanya nyepesi hii (Qur'ani) kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.

فَارْتَقِبْ إِنَّهُم مُّرْتَقِبُونَ

Basi ngoja tu, hakika wao (pia), wanangoja.

Aya hizi ambazo ndizo za mwisho za Suratu-Dukhan, zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba, lengo la kuteremshwa wahyi ni kuzindua na kukumbusha ili wale walioghafilika wazinduke na kuzichunga nafsi zao. Kinyume na vilivyo vitabu vya kielimu na kitaalamu, ambavyo watu wengi wa kawaida hawawezi kunufaika navyo, Qur’ani tukufu, licha ya kuwa na muhtawa wa kina na maana pana, lakini imetumia pia lugha nyepesi na ya uwazi, ambayo inaweza kueleweka na kufahamika na watu wa matabaka yote. Nukta na maelezo yake ni yenye mafunzo, ubainishaji wake mambo uko wazi na wadhiha, na hoja zake ni imara na makini. Kwa hivyo aya zake hupenya ndani ya nyoyo zenye utayarifu na kuziamsha. Lakini kwa watu ambao wameshajipangia kukanusha, kupinga, kukaidi na kufanya inadi, vyovyote vile watakavyosomewa aya hizo hawatakumbuka wala kuzinduka. Na sababu ni kwamba hawataki kuikubali haki. Ni sawa na mtu aliyejifanya tu kuwa amelala, ambaye hata akiitwa kwa sauti yoyote ile haitikii wala hatikisiki. Hao makafiri na wakanushaji wamekaa wakidhani kwamba, wewe na dini uliyokuja nayo utashindwa; basi na wewe pia subiri ithibiti ahadi ya Mola wako ya ushindi wa dini yake ya haki dhidi ya makafiri na wafanya inadi na kushindwa shirki na ukafiri wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mafundisho ya Qur’ani inapasa yabainishwe kwa kutumia lugha nyepesi inayoweza kufahamika na watu wote, kwa sababu lengo lake ni kuwaongoza wanadamu wote, si kundi maalumu au jamii fulani tu ya watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amekamilisha dhima yake kwa watu kwa kuteremsha vitabu vya mbinguni na kuwatuma Mitume. Kwa hiyo kama mtu ataamua kuikataa haki kwa makusudi, akae kungojea adhabu ya Mwenyezi Mungu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 914 ya Qur’ani imefikia tamati. Na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura hii ya 44 ya Ad-Dukhan. In shaa Allah tuwe tumeaidhika, kuelimika na kufaidika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka na atujaalie kuwa miongoni mwa atakaowarehemu kwa kuwaingiza katika Pepo yake ya milele huko akhera, amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/