May 24, 2023 17:42 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 922 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 6 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَإِذَا حُشِرَ النَّاسُ كَانُوا لَهُمْ أَعْدَاءً وَكَانُوا بِعِبَادَتِهِمْ كَافِرِينَ

Na watu watakapo kusanywa (wale walioabudiwa) watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.

Katika darsa iliyopita na ya mwanzo ya sura hii ilizungumziwa ibada ya washirikina ya kuabudu masanamu, ambapo katika kubainisha jinsi isivyo na faida yoyote, Qur'ani ikawaambia watu hao: kama mtayaomba masanamu hayo mpaka Siku ya Kiyama ili yakutatulieni matatizo yenu au yakufanikishieni mambo yenu, hayatoyasikia maneno yenu wala hayatakuwa na uwezo wa kukufanyieni hayo mnayoyaomba. Baada ya maelezo hayo, aya hii tuliyosoma inasema: lakini mbali na hayo, Siku ya Kiyama, waabudiwa hao watakuja kukupingeni na kutamka dhidi yenu. Tab'an kwa wale waabudiwa wenye akili na utambuzi, kama baadhi ya malaika na watu, ambao walikuwa wakiabudiwa, wao watasimama rasmi na kuwapinga kwa uadui wale waliokuwa wakiwaabudu. Kwa mfano Nabii Isa (AS) na malaika, wao watajibari na kuwakataa waziwazi waliokuwa wakiwaabudu. Na kwa wale waabudiwa wasio na hisi kama masanamu, hayo pia Allah SWT atayawezesha kusema na kudhihirisha chuki zao kwa wale waliowaabudu. Aya hii inatuelimisha kwamba, chochote kiabudiwacho hapa duniani badala ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, badala ya kuwa muombezi wa mtu na kumtakia shufaa, kitageuka kuwa adui kwake na kumshtaki mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya saba na ya nane ambazo zinasema:

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ هَٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ

Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru husema juu ya haki inapo wajia: Huu ni uchawi dhaahiri.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ إِنِ افْتَرَيْتُهُ فَلَا تَمْلِكُونَ لِي مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَا تُفِيضُونَ فِيهِ ۖ كَفَىٰ بِهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۖ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

Au wanasema: Ameizua mwenyewe! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo mnayo ropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ni Mwingi wa Maghufira, Mwenye kurehemu.

Aya hizi zinaashiria baadhi ya tuhuma chafu ambazo washirikina wa Makka walikuwa wakimnasibisha nazo Bwana Mtume SAW na kueleza kwamba: baadhi ya wakati, walikuwa wakimwita Nabii Muhammad SAW mchawi; na Qur'ani ni maneno yatokanayo na sihiri na uchawi wake yeye; na kwamba anazitumia aya za kitabu hicho kuteka na kuwavuta watu. Kwa upande mmoja, washirikina hawakuweza kuukana mvuto wa ajabu iliokuwa nao Qur'ani na jinsi ilivyoziathiri nafsi na kuzivutia mno nyoyo za watu; na kwa upande mwingine, hawakuwa tayari kuiungama kwamba ni haki na ukweli na kuifuata. Kwa hivyo ili kuzipotosha fikra za watu, wakaamua kuivurumizia Qur'ani tuhuma za uchawi. Tab'an kusema hivyo pia, kulikuwa na maana ya kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba, Kitabu hicho cha mbinguni kina taathira ya ajabu na isiyo ya kawaida ndani ya nyoyo za watu. Lakini ukweli ni kwamba sababu hasa ya mvuto wake ni ukweli wa yale yasemwayo na aya zake. Mbali na tuhuma hizo za uchawi, washirikina walikuwa wakati mwingine wakisema: ayatamkayo mtu huyu yanatokana na yeye mwenyewe lakini anayanasibisha na Mwenyezi Mungu na kujitangaza yeye kuwa ni Mtume wake. Bwana Mtume SAW aliwajibu washirikina hao kwa kuwaambia: kama ni kweli hivyo mnavyodai nyinyi, kwamba mimi si Mtume wa Mwenyezi Mungu na haya niyasemayo ni uongo ninaounasibisha na Yeye, basi itapasa Yeye Mola anifedheheshe mimi ili watu wasipotoshwe na maneno yangu. Na litakapojiri hilo hakutakuwa na mtu yeyote atakayeweza kukabiliana na irada ya Mwenyezi Mungu, wala kunilinda na kunitetea mimi mbele Yake. Kwa hakika ni nyinyi, ambao inapasa muihofu adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu mnapingana na Mtume wake na mnawazuilia watu njia ya haki, japokuwa mnajua mimi niko katika haki na wala sihitaji chochote kwenu ili kuthibitisha Utume wangu na ukweli wa ninayoyalingania. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni shahidi wa haya ninayodai na Mjuzi wa juhudi na bidii nizifanyazo katika kufikisha ujumbe wake. Kwa upande mwingine, Yeye Allah SWT anauona uongo, uzushi na uafriti wenu mnaofanya. Na hilo tu linatosha kwangu mimi. Baada ya hayo, ili Allah SWT awaonyeshe washirikina kwamba njia ya wao kurejea haijafungwa na mlango wa toba uko wazi na kwa hivyo waache inadi na upinzani wao na waiamini haki, anasema katika sehemu ya mwisho ya aya tulizosoma ya kwamba: Mwenyezi Mungu ni msamehevu sana na mrehemevu mno kwa waja wake. Anawasamehe wanaotubia na kuwaneemesha kwa rehma zake zisizo na ukomo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ishara za ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW ziko wazi na wadhiha kabisa, lakini tatizo la baadhi ya watu ni kwamba inadi na ukaidi wao ndivyo vinavyowazuia wasiamini na kuifuata haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hata wapinzani pia wanakiri na kuzikubali nguvu za kimiujiza za mvuto wa aya za Qur'ani katika kuziteka nyoyo za watu, lakini wanaishia kudai kwamba, ni sihiri na uchawi. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujihadhari tusije tukanasibisha utashi na itikadi zetu binafsi na dini ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu kufanya hivyo kutakuwa sababu ya kupata hilaki na adhabu kali ya Mola. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, mlango wa toba uko wazi kwa watu wote hata makafiri na wapinzani wa haki; na Mwenyezi Mungu Mola mrehemevu na msamehevu, yuko tayari kuzipokea toba zao.

Ifuatayo sasa ni aya ya tisa ya sura yetu ya Al Ah'qaaf ambayo inasema:

قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

Sema, mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyo fanywa mimi wala nyinyi. Sifuati ila yaliyofunuliwa kwangu (kwa Wahyi), wala mimi si chochote ila ni mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.

Katika aya hii ya tisa, Bwana Mtume Muhammad SAW anatakiwa avijibu visingizio vinavyotolewa na washirikina wa Makka kwa kuwaambia: mimi siko tofauti na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu; na kama walivyokuwa Mitume wengineo, mimi pia ni binadamu kama nyinyi. Mimi si Mtume wa mwanzo kuwalingania watu Tauhidi. Kabla yangu mimi, walikuja Mitume wengi, ambao wote walikuwa wanadamu, waliokuwa wakivaa nguo na wakila chakula. Tofauti pekee iliyopo baina yangu mimi na nyinyi ni kwamba, Mwenyezi Mungu ananiteremshia wahyi na kuniamuru nikuonyeni na kukupeni indhari juu ya mwisho mbaya utakaotokana na matendo maovu mnayofanya. Elimu ya ghaibu pia niliyonayo haitokani na mimi mwenyewe; mimi ninayajua baadhi ya mambo ya ghaibu ambayo Yeye Allah mwenyewe ananifunza. Sijui mimi, nini atanifanya Mola wangu, kama ambavyo sifahamu pia atakufanyeni nini nyinyi. Kwa hiyo msinitarajie kufanya utabiri na uaguzi kuhusu mustakabali wangu mwenyewe au wenu nyinyi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, lengo la Mitume katika zama zote za historia lilikuwa moja. Kila Mtume alisadikisha na kuendeleza yaliyoletwa na mwenzake aliyemtangulia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa viongozi wa jamii inapasa wawe wakweli katika wanayowaeleza watu na wala wasidai kujinasibisha na mambo wasiyo na uwezo wala mamlaka nayo au kuahidi wasiyoweza kutekeleza. Vilevile aya hii inatuonyesha kwamba Mitume walikuwa wakiwaonea uchungu na kuwatakia kheri watu wao na kuwaonya kila mara juu ya mambo yatakayowafanya waharabikiwe hapa duniani na huko akhera.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 10 ambayo inasema:

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّهِ وَكَفَرْتُم بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na akashuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.   

Kama ilivyoelezwa katika tafsiri za Qur'ani, Abdullah bin Salam, alikuwa mmoja wa maulamaa maarufu wa Kiyahudi aliyekuwa akiishi katika ardhi ya Hijaz. Myahudi huyo alisilimu na akatangaza kuwa Bwana Mtume SAW ndiye Nabii ambaye kudhihiri kwake kumetabiriwa na kuahidiwa ndani ya Taurati na Injili. Lakini wakubwa wengi wa Kiyahudi walimkataa mwanazuoni huyo, wakamvurumizia tuhuma na uzushi. Wao hawakuwa tayari kuuamini Utume wa Nabii Muhammad SAW. Na hapana shaka chanzo cha kukufuru kwao kilikuwa ni ghururi na kiburi walichokuwa nacho. Miongoni wa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika kujadiliana na wapinzani, badala ya kuwa na taasubi na ukereketwa juu ya itikadi yetu na kutaka kuonyesha kuwa ni haki mutlaki na isiyo na shaka, tuwaambie, chunguzeni na pimeni nyinyi wenyewe; kama mtaona maneno yetu ni haki basi yakubalini; lakini mjue pia kuwa kama mtaifahamu haki na mkaikataa, mwisho mbaya unakungojeeni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, chimbuko la ukafiri ni inadi na kutakabari mbele ya haki; si mghafala na ujinga wa mtu. Aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba, kusimama ili kuupinga ukweli wa wahyi na Qur'ani ni kuifanyia dhulma kubwa jamii ya wanadamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 922 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/