Sura ya Fat-h, aya ya 5-9 (Darsa ya 938)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 938 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya Al Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya tano ya sura hiyo ambayo inasema:
لِّيُدْخِلَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَيُكَفِّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عِندَ اللَّهِ فَوْزًا عَظِيمًا
Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika Bustani zipitazo mito chini (ya miti) yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia Sulhu ya Hudaibiya iliyofikiwa baina ya Bwana Mtume Muhammad SAW na washirikina wa Makka, ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliitaja kuwa ni bishara ya ushindi wa Waislamu katika siku za usoni na kuwapoza na kuwapa utulivu wale waliokuwa wamekereka na kutiwa wasiwasi na yaliyotokea. Aya hii tuliyosoma inasema: wale ambao wanamtii Mtume wa Allah na wako pamoja naye katika kila hali, -mbali na kupata utulivu wa hapa duniani-, Allah SWT amewadhaminia akhera yao pia, kwa kuwasamehe makosa yao na kuwaandalia makazi katika Pepo ya milele na neema zake zisizomalizika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, japokuwa wanawake hawashiriki moja kwa moja katika baadhi ya mambo mazito na magumu kama kwenye medani za vita na Jihadi, lakini kama watakuwa pamoja kiroho na kifikra na waume zao na watoto wao wapiganaji; na wakawa radhi nao na kuwaunga mkono kwa kushiriki kwao kwenye medani za vita na Jihadi, basi na wao pia watakuwa na fungu katika malipo ya thawabu watakayopewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, maana ya kuamini, si kwamba mtu muumini hawezi kuteleza wala kufanya kosa au dhambi yoyote. Lakini kutokana na waumini kufanya mambo mengi mema na ya kheri, Allah SWT huyafumbia macho makosa machache wanayofanya kwa kuteleza, akawasamehe na kuwarehemu kwa rehma zake. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, saada ya kweli na kufuzu kukubwa kabisa kwa mja, ni kupata fanaka ya dunia na ya akhera pia; kwa sababu kuna makafiri wengi ambao wameneemeshwa mno kwa neema za mali na vitu vya kimaada hapa duniani.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya sita na ya saba ya sura yetu ya al Fat-h ambazo zinasema:
وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ الظَّانِّينَ بِاللَّهِ ظَنَّ السَّوْءِ ۚ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ ۖ وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ وَلَعَنَهُمْ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا
Na awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanao mdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio mabaya kabisa.
وَلِلَّهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا
Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Wakati Bwana Mtume SAW na masahaba zake walipoondoka Madina kuelekea Makka, wanafiki, ambao hawakudhani kama Allah SWT atawapa Waislamu auni na msaada wake, walikuwa wakisema: Waislamu hawatarudi Madina salama; ama watauliwa au watakamatwa mateka na washirikina. Na wao washirikina wa Makka walikuwa kweli wamejipanga kukabiliana na Waislamu, lakini hatari hiyo ikawaondokea Waislamu kwa tadbiri na hekima ya Bwana Mtume na kusainiwa mkataba wa Sulhu ya Hudaibiya baina ya mtukufu huyo na washirikina. Katika kuielezea hali hiyo, aya tulizosoma zinasema, wanafiki wa Madina na washirikina wa Makka ambao walikuwa wakiwawazia mabaya Waislamu, wao ndio watakaopatwa na hatima mbaya, kwa kughadhibikiwa na kufikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu duniani na akhera. Wale ambao wameelekeza matumaini yao kwa Allah SWT, wakajitosa kwenye medani kwa kutegemea uwezo na hekima ya Mola watarehemewa kwa auni, uraufu na msaada wake na mwishowe watapata ushindi. Lakini wale ambao woga na hofu zinawakalisha majumbani mwao na wanawahofisha na wenzao juu ya nguvu na uwezo mkubwa wa jeshi la maadui na hivyo kudhoofisha ari ya Waislamu na kuwavunja moyo, mwishowe watafikwa na hatima mbaya. Kwa hakika watu wa aina hiyo wanajiharibia dunia na akhera yao. Nukta moja yenye kutoa mguso hapa ni kwamba, katika aya hizi, waumini wanawake wametajwa pamoja na waumini wanaume, na wanawake washirikiana na wanafiki wametajwa pamoja na wenzao wanaume wenye sifa hizo, ili kutanabahisha juu ya nafasi na mchango muhimu wa wanawake katika masuala ya kijamii na kisiasa na taathira yao kwa wanaume. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na dhana mbaya juu ya ahadi za Mwenyezi Mungu ni katika sifa wanazokuwa nazo wanafiki na washirikina; hawawi nayo sifa hiyo waumini wa kweli ambao wana imani kamili ya kuthibiti ahadi alizowapa Mola wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanafiki na washirikina huungana na kuwa kitu kimoja kifikra katika uafriti, ushetani na upotofu wao. Na ndio maana katika aya hizi, hatima ya wanafiki imeunganishwa na ya washirikina, japokuwa watu wenye unafiki huwa wanaishi pamoja na waumini; na kidhahiri, wanaonekana na wanahisabika kuwa ni Waislamu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wanawake wana hali sawa na wanaume katika kupambika na sifa njema au hulka chafu; na kama walivyo wanaume, wana taathira na mchango kamili kwa hatima na majaaliwa yao wenyewe na ya jamii zao. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, vitu vyote na kila kilichoko katika ulimwengu wa maumbile viko chini ya mamlaka na uendeshaji wa Allah Azza wa Jalla, na yeyote yule atakayetaka kukabiliana na Allah hatakuwa na hatima nyingine isipokuwa kufeli na kushindwa.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nane na ya tisa ambazo zinasema:
إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا
Hakika tumekutuma wewe uwe Shahidi, na Mbashiri, na Mwonyaji,
لِّتُؤْمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتُعَزِّرُوهُ وَتُوَقِّرُوهُ وَتُسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا
Ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mumsaidie, na mumtukuze, na mumsabihi (Mwenyezi Mungu) asubuhi na jioni.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kwa kubainisha hadhi na nafasi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa watu kwa kusema: yeye ni mwenye kuyashuhudia na kuyaona yale yanayojiri katika jamii na hakuna chochote kinachofichika kwake japokuwa yamkini asiyaeleze na kuyafichua yale anayoyajua. Yeye Bwana Mtume SAW anawalingania watu kufanya mema na ya kheri na kujiepusha na maovu na mabaya na kuwapa bishara juu ya kufanya amali njema na maonyo na indhari juu ya kutenda mabaya. Kwa hivyo linalotarajiwa kwa waumini ni kuyakubali maneno yake; na kuwa naye bega kwa bega katika matendo pia na kuienzi hadhi na nafasi yake katika jamii ili wanafiki wa ndani na maadui wa nje wasijusuru wala kuthubutu kumdhuru kwa namna yoyote ile. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tuwe tunaweka mlingano katika utoaji bishara na maonyo tunapowalingania na kuwafunza watu uongofu, ili wasije wakaingiwa na ghururi za kuwa na matumaini kamili ya kufuzu au wakavunjika moyo na kukata tamaa moja kwa moja ya kupata rehma za Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, watu wenye masuulia na uongozi katika kufanya tablighi na kufikisha wito wa dini katika jamii, wanatakiwa wawe ruwaza na mfano wa kuigwa na watu wengine kwa tabia na matendo yao; na wao wenyewe wawe na uwelewa na taarifa za yanayojiri ndani ya jamii. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, sharti mojawapo la kumwamini Allah ni kulinda na kutetea heshima ya dini yake na ya Mtume wake. Inapasa Waislamu wamuenzi Bwana Mtume Muhammad SAW na kuitukuza hadhi na nafasi yake katika jamii. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, pamoja na kushughulika na harakati za kijamii na masuala mengine ya kimaisha, mtu muumini huwa anamdhukuru na kumkumbuka Allah asubuhi na jioni na akiwa ndani ya Sala na nje yake; na kwa njia hiyo, kuimarisha zaidi mawasiliano yake na Mola wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 938 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu mapenzi ya kweli ya Mtume wetu na amjaalie Siku ya Kiyama yeye na Aali zake, waje wawe waombezi wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/