May 27, 2023 05:24 UTC
  • Sura ya Fat-h, aya ya 10-13 (Darsa ya 939)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 939 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya Al Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 ya sura hiyo ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّهَ يَدُ اللَّهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا

Hakika wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hakika anaivunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa

Katika darsa kadhaa zilizopita tulizungumzia Sulhu ya Hudaibiyah iliyofikiwa baina ya Bwana Mtume SAW na washirikina wa Makka. Kabla ya kusainiwa mkataba wa suluhu hiyo, Bwana Mtume SAW alimtuma mmoja wa masahaba zake kwa washirikina wa Kikureishi ili akawape taarifa kwamba Waislamu wamekusudia kwenda kuzuru Nyumba ya Allah ya Al-Kaaba na hawana nia yoyote ya kuanzisha ugomvi na mapigano. Washirikina walimkamata na kumweka kizuizini kwa muda mjumbe huyo aliyetumwa Makka na Bwana Mtume, jambo ambao liliibua tetesi na kueneza uvumi miongoni mwa Waislamu kwamba mjumbe huyo wa Mtume ameuliwa. Kufuatia hali hiyo, Bwana Mtume SAW aliwakusanya masahaba zake na kuchukua baia' na ahadi kwao ya kwamba kama habari ya kuuliwa mjumbe wake ni ya kweli, badala ya kurudi Madina wataingia vitani kubariziana na washirikina. Wakati habari ya baia' na kiapo hicho cha utiifu cha masahaba kwa Bwana Mtume ilipowafikia washirikina, walimwachia huru mjumbe wa Mtume, na badala ya kupigana vita na Waislamu, wakaridhia kufanya suluhu nao. Na kwa sababu hiyo, kadhia ya mkono wa baia' waliotoa Waislamu kumpa Bwana Mtume Muhammad SAW imekuwa na nafasi muhimu katika historia ya Uislamu, kiasi kwamba katika aya nyingine za Qur'ani, Allah SWT ameeleza alivyofurahishwa na kuwaridhia Waislamu kutokana na ahadi hiyo ya utiifu waliyotangaza kwa Mtume wake. Katika aya hii tuliyosoma pia, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: kutoa mkono wa baia' kwa Mtume, ni sawa na kutoa baia' hiyo kwa yeye Allah SWT. Na kama inavyokuwa katika baia', ambapo watu wawili huwekeana mkono juu ya mkono mwingine; vivyo hivyo Waislamu waliombai' Mtume ni kama kwamba wamewekeana mikono yao na mkono wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambao uko juu kabisa ya mikono yote. Na ni wazi kwamba mtu anayewekeana ahadi na Mwenyezi Mungu ya kuinusuru dini yake, inatarajiwa kuwa hataivunja ahadi hiyo. Na bila shaka kama atafanya hivyo, atakuwa ameidhuru imani yake na kuitia hasarani nafsi yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, sharti mojawapo la kumwamini kikweli Mwenyezi Mungu ni kuinusuru dini yake na kuendelea kuwa na utiifu na uaminifu kwa viongozi wa dini katika kukabiliana na njama na hila za maadui. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mkono wa rehma za Allah unawafikia watu wanaotoa msaada wa kuinusuru dini yake na kuendelea kuwa thabiti katika njia hiyo. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kwamba, kuheshimu ahadi na mkataba ni katika alama za kushikamana na dini, na kuvunja ahadi na makubaliano huwa kwa hakika ni sawa na mtu kuivunja nafsi yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 11 ambayo inasema:

سَيَقُولُ لَكَ الْمُخَلَّفُونَ مِنَ الْأَعْرَابِ شَغَلَتْنَا أَمْوَالُنَا وَأَهْلُونَا فَاسْتَغْفِرْ لَنَا ۚ يَقُولُونَ بِأَلْسِنَتِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ ۚ قُلْ فَمَن يَمْلِكُ لَكُم مِّنَ اللَّهِ شَيْئًا إِنْ أَرَادَ بِكُمْ ضَرًّا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ نَفْعًا ۚ بَلْ كَانَ اللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرً

Watakuambia mabedui walio baki nyuma: Zimetushughulisha mali zetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha. Wanasema kwa ndimi zao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Sema: Ni nani awezaye kukusaidieni chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka Yeye kukudhuruni au akitaka kukunufaisheni? Bali Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

Wakati Waislamu walipokuwa wanaondoka Madina kuelekea Makka, Bwana Mtume SAW aliwaagiza Waislamu wengine wa makabila ya kibedui yaliyokuwa yakiishi kwenye viunga vya mji wa Madina wajiunge na wenzao hao; lakini baadhi ya makundi ya watu wa makabila hayo yalikhalifu agizo hilo la kuandamana na Bwana Mtume kwa sababu ya woga na hofu ya kwenda kubariziana na washirikina wa Makka. Wakati Waislamu waliporudi Madina, ili kutetea hatua yao ya kuhalifu agizo walilopewa, wale watu ambao walikwepa kujiunga na msafara wa Bwana Mtume, walimwendea mtukufu huyo na kumwambia, mashughuliko ya maisha ndiyo yaliyowafanya wasitoke pamoja naye. Lakini aya za Qur'ani zikateremshwa na kuwafedhehesha watu hao, kwamba yale wanayoyatamka kwa ndimi zao ni tofauti na yaliyomo nyoyoni mwao. Kisha aya ikaendelea kutilia mkazo nukta moja muhimu, nayo ni kwamba, kukimbia Jihadi hakumdhaminii mtu kuishi milele. Kwani si ajabu kuwaona watu wengi wanakwenda kupigana Jihadi na wanarudi makwao salama usalimini, na wengine wengi wanaobaki makwao wanafikwa na mauti wakiwa ndani ya nyumba zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, moja ya mambo yenye taathira hasi kutokana na kukaidi kutekeleza majukumu ya kijamii, ni watu kuwa dhaifu kidini na kushuka kiwango cha maarifa na utamaduni wao. Kwa sababu hiyo, viongozi wanaowaza na kufikiria mustakabali, inapasa waizingatie nukta hiyo katika upitishaji maamuzi juu ya masuala muhimu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuikumbatia dunia na kuwa na utegemezi nayo wa kinafsi kupindukia huwafanya baadhi ya watu wakwepe kujitokeza kwenye medani za vita na Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba, dua na uombezi wa Mtume wa Allah kwa walioteleza na kufanya makosa, vinakubaliwa na Yeye Mola. Halidhalika aya hii inatutanabahisha kuwa, tuna wajibu na ulazima wa kuihami dini ya Mwenyezi Mungu na viongozi wa dini hata kama tutapata hasara na kufikwa na madhara katika njia hiyo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 12 na 13 za sura yetu ya Fat-h ambazo zinasema:

بَلْ ظَنَنتُمْ أَن لَّن يَنقَلِبَ الرَّسُولُ وَالْمُؤْمِنُونَ إِلَىٰ أَهْلِيهِمْ أَبَدًا وَزُيِّنَ ذَٰلِكَ فِي قُلُوبِكُمْ وَظَنَنتُمْ ظَنَّ السَّوْءِ وَكُنتُمْ قَوْمًا بُورًا

 Lakini mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mlidhania dhana mbaya, na mmekuwa watu wanao angamia. 

وَمَن لَّمْ يُؤْمِن بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ فَإِنَّا أَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ سَعِيرًا

Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa hakika Sisi tumewaandalia makafiri Moto mkali.

Katika mwendelezo wa maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia, aya hizi zinataja chanzo cha baadhi ya watu kukaidi kuandamana na Bwana Mtume SAW na Waislamu wenzao na kueleza kwamba, sababu hasa ya watu waliokataa kutoka, haikuwa kutingwa na kushughulishwa na masuala ya kifedha na ya maisha yao ya kifamilia, bali ni mtazamo potofu uliotokana na dhana mbaya waliyokuwa nayo nafsini mwao kwa ahadi za Mwenyezi Mungu. Watu hao walikuwa wakidhani kwamba, Waislamu hawatorudi salama katika safari hiyo, na ndio maana hawakuandamana nao. Wao walifikiri Mwenyezi Mungu atamwacha mkono Mtume wake katika safari hiyo mbele ya maadui zake; na kwa hiyo hakukuwa na sababu yoyote ya wao kuhatarisha maisha yao. Na ni dhana hiyo potofu ndiyo iliyowakosesha kuandamana na Mtume, wakakosa kumbai' tena mtukufu huyo na kuwa sababu ya wao kuharibikiwa. Sababu ni kwamba, kitendo chao hicho ni alama ya imani dhaifu; bali si hasha kukawa ni kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake ambako kutawafanya wale waliokhalifu ahadi na baia' yao wafikwe na adhabu kali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusichukue uamuzi kuhusiana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na viongozi wa dini kwa kutegemea dhana na mahesabu ya kilimwengu tu; bali tuchukue hatua kwa kutawakali kwake Yeye Mola pasi na kuhofu kitu chochote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwadhania dhana mbaya waja wa Mwenyezi Mungu ni katika madhambi makubwa, seuze kuwa na dhana mbaya juu yake Yeye Allah SWT na ahadi zake. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, baadhi ya wakati, dhana mbaya na fikra potofu humuathiri mtu mpaka zikamfanya aasi na kuhalifu amri za Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, kuwa na mapenzi kupindukia kwa ahli na familia kusiwe sababu ya kumzuia mtu kutekeleza majukumu yake ya kidini, kwani kufanya hivyo kutamfanya ahasirike na mwishowe kuangamia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 939 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atuguhufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/