May 27, 2023 06:36 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 948. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 49 ya al H'ujuraat, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 50 ya Qaaf. Sura hii iliteremshwa Makka, ina jumla ya aya 45 na maudhui kuu za aya zake ni kuhusu msingi wa Ma'adi, yaani kufufuliwa viumbe na sababu zake, mwisho wa waja wema na wabaya na hatima iliyowapata watu wa kaumu zilizopita. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu kwa aya ya mwanzo na ya pili ya sura hiyo zisemazo:

ق ۚ وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ

Qaaf. Naapa kwa Qur'ani tukufu!

بَلْ عَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ

Bali wanastaajabu kwamba amewajia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!

Sura hii pia kama zilivyo sura nyingine 28 za Qur'ani, imeanza kwa herufi ya mkato, na kufuatiwa kiapo chake na maelezo ya kubainisha utukufu na adhama ya Qur'ani tukufu. Madhumuni yake ni kumaanisha kwamba, kitabu na maneno haya ya Allah yameandikwa kwa kutumia herufi hizi hizi za alfabeti zinazotumiwa na watu wote, lakini hakuna mtu yeyote awezaye kuleta maneno kama hayo na yanayofanana nayo; na huo ndio muujiza wa Qur'ani. Kisha aya zinaendelea kuashiria maneno ya wakanushao Kiyama na kueleza kwamba: wao wanaonyesha kushangazwa na kustaajabishwa kumuona mtu miongoni mwao anadai kuwa yeye ni Mtume na anawatahadharisha juu ya kujiri kwa Kiyama na kusema kwamba, madai ya mtu huyo ni jambo baidi na lisiloingia akilini. Wanasema hayo ilhali yeye si mtu wa mwanzo kubaathiwa na kupewa Utume na kuja na habari ya kujiri kwa Kiyama. Kwa hivyo mastaajabu na mshangao wao hautokani na kutokuwa na uelewa, bali sababu yake ni hulka ya ukaidi na ukanushaji; na kusema kweli hicho ni kisingizio tu wanachotumia ili kuyakataa maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani ni maneno ya Allah yenye adhama, utukufu na sharafu; na mtu yeyote anayetaka awe na adhama na utukufu inapasa ashikamane na Qur'ani na kuhakikisha lolote alifanyalo linaendana na Kitabu hicho. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, sifa maalumu ya Mitume, ya kwamba wao wenyewe walitokana na viumbe binadamu na walikuwa watu kama watu wengine, ni jambo la mantiki na hekima; na kwa hakika ni nukta chanya na inayotilia nguvu Utume wao; lakini wasio na busara na wakanushaji, wanalitumia hilo kama kisingizio cha kutaka kuwadunisha waja hao wateule wa Allah. Halikadhalika, aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, makafiri hawana hoja na sababu ya kimantiki ya kuukana Utume na Ma'adi; na ndio maana ili kuukanusha na kuukadhibisha ukweli wanajifanya kustaajabishwa na kuyachukulia mawili hayo kuwa ni mambo yaliyo baidi kuwepo na yasiyoingia akilini.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tatu hadi ya tano ya sura hii ya Qaaf ambazo zinasema:

‏ أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ۖ ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ

Ati tutakapokufa na tukawa udongo (tutafufuliwa)? Hayo ni marejeo ya mbali kabisa!

قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ ۖ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ

Kwa hakika tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi katika miili yao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi kila kitu.

بَلْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَهُمْ فِي أَمْرٍ مَّرِيجٍ

Lakini waliikadhibisha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogeko.

Katika maelezo tuliyotoa kwenye aya zilizotangulia tulieleza kwamba, wanaokanusha kufufuliwa viumbe hawana hoja ya kuonyesha kuwa kujiri kwa hilo ni muhali. Aya hizi zinaashiria suali walilokuwa wakiuliza watu hao kila mara na kwa mshangao la kwamba: itawezekanaje kwa viungo vya miili yetu vinavyosagika sagika na kugeuka udongo baada ya sisi wenyewe kufa, viwe na uhai tena na kuturejesha tena kwenye maisha yetu ya awali? Qur'ani tukufu ikawajibu watu hao kwa kuwaambia: Mwenyezi Mungu anajua baada ya kifo ni mabadiliko gani yanatokea katika viungo vya mwili wa mtu; kwa hivyo Siku ya Kiyama atavirejesha tena vyote hivyo katika hali zao za awali. Hayo yote yametunzwa na kuhifadhiwa kwake Yeye Allah SWT. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Bila shaka, miongoni mwa hao wakanushaji, wako walioifahamu haki, lakini wakaamua kuikanusha. Kwa maneno mengine ni kwamba, ukafiri wa watu hao haujatokana na ujinga na kutokuwa na uelewa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kati ya mbinu za kuvutia zinazotumiwa na Qur'ani kulingana na kinachojadiliwa, huwa kwanza ni kuleta maneno ya wapinzani na wakanushaji, kisha ndipo inapoyatolea majibu madai yao kwa hoja na mantiki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa uumbaji umesimama na unaendeshwa kwa elimu na ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; na kila kitu kinafanyika kwa nidhamu, makadirio na hisabu maalumu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, chanzo cha mwanadamu kumahanika na kutafirika ni kukadhibisha haki na kuikufuru; kama ambavyo chanzo cha umakinifu na utulivu ni kumkumbuka na kumtaja Allah na kuikubali haki. Na kwa sababu hiyo, ndio maana watu wasio na imani thabiti na madhubuti huwa daima katika hali ya kumahanika, kutafirika na kutangatanga.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya sita hadi ya nane ambazo zinasema:

أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ

Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao, tumezijengaje na tumezipambaje na wala hazina nyufa?

وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ

Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.

تَبْصِرَةً وَذِكْرَىٰ لِكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ

(Yawe haya) ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja muelekevu. 

Ukanushaji wa Ma'adi, yaani kufufuliwa viumbe unatokana na shaka katika elimu na ujuzi wa Allah, au nguvu na uwezo wake Mola. Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia upana na ukubwa wa elimu na ujuzi wa Mwenyezi Mungu usio na ukomo, aya hizi tulizosoma zinabainisha uwezo mutlaki wa Mola kwa kueleza kwamba: kama mtainua vichwa vyenu juu na kulitazama jua na mwezi, nyota na sayari zisizohesabika mtabaini na kuuelewa uwezo wa Mola Muumba na hamtahoji na kuuliza tena, vipi Mwenyezi Mungu atawafufua waliokufa? Na kama mtatupia jicho mazingira yaliyokuzungukeni mtaiona milima na mabonde, misitu na nyika na anuai za miti na mimea, ambayo nyinyi wanadamu hamjachangia kuwepo kwake kwa namna yoyote ile, bali vyote hivyo vimetokana na qudra na uwezo wa Allah SWT. Yote hayo ni sababu na njia za ukumbusho na mazingatio ya kumtambua Muumba, tab’an kwa mtu anayetaka kumjua Mola wake na kujikurubisha kwake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ardhi na mbingu na ulimwengu wote wa uumbaji ni darasa la somo la kumjua Mwenyezi Mungu, lakini somo hilo linamnufaisha yule aliye na kiu na azma ya kuitambua asili na chanzo cha ulimwengu pamoja na hatima na mwisho wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuna nidhamu na kanuni maalumu inayotawala katika sayari na maumbo ya angani. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, uimara, uzuri, jamali, nidhamu na mpangilio ni sifa maalumu za uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, kiasi kwamba hakuna dosari, kasoro wala ila yoyote inayoshuhudiwa katika mfumo wa uumbaji wake Mola. Huu wenyewe ni ushahidi na uthibitisho wa ujuzi na uwezo usio na kikomo wa Muumba wa ulimwengu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa uotaji wa mimea yenye uhai kwenye ardhi ya udongo ulio mfu ni mfano mmojawapo wa qudra na uwezo wa Allah SWT wa kuwafufua waliokufa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 948 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuzidishie elimu na ujuzi wa kumtambua Yeye Mola wetu utakaozifanya imara na thabiti zaidi imani zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/