Jumatano, 31 Mei, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 11 Mfunguo Pili Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 31 Mei 2023.
Siku kama ya leo miaka 1494 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuhamia mji wa Byzantine, ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake na uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, ndipo dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi na wafuasi wake wakaruhusiwa kuabudu kwa uhuru.

Siku kama ya leo miaka 1296 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume (as). Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu.

Siku kama ya leo miaka 1108 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhulqaad 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na faqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alikulia katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na akapata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kielimu za Sheikh Mufid ilikuwa midahalo yake na wanazuoni wa faqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu vingi vya thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usulul Fiqh.

Siku kama ya leo, miaka 191 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1832 miladia aliuawa Évariste Galois, mtaalamu mwenye kipawa cha hesabati wa Ufaransa. Évariste Galois alizaliwa katika mji wa Bourg-la-Reine karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Hadi kufikia umri wa miaka 12, Galois hakuwa na mwalimu mwengine zaidi ya mama yake. Kuanzia rika la uchipukizi alianza kusoma vitabu vya kiwango cha juu mno vya hesabati na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha ukweli wa hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Katika siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi ziliingia mikononi mwa wazungu wachache. Lakini hatimaye baada ya mapambano makali ya waafrika kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, mnamo mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhatimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 2010, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia msafara wa meli zilizosheheni misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Ghaza waliozingirwa na utawala huo. Shambulio hilo liliua watu 9 na kujeruhi wengine zaidi ya 50. Msafara huo uliokuwa na wanaharakati 663 kutoka nchi 37 duniani, ulikuwa umebeba shehena ya misaada ya dawa na chakula kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza wanaokabiliwa na mzingiro wa kidhulma wa Wazayuni. Shambulio hilo la kinyama lililaaniwa vikali na mataifa mbalimbali duniani, na hatimaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likatoa azimio la kufanyika uchunguzi wa haraka na usiopendelea upande wowote kwa lengo la kubaini na kuwekwa wazi wahusika wa jinai hizo.

Na leo Mei 31 ni siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku. Historia ya tumbaku inarudi kwenye matumizi ya mmea wa tumbaku na wenyeji wa Amerika katika zama za kale. Mwaka 1492, Christopher Columbus na wenzake walifika kwenye kisiwa kilichoko kati ya Amerika ya Kaskazini na Kusini, na kuwaona wenyeji wakiweka majani ya ajabu ya mimea juu ya moto na kuvuta moshi wake kwenye mapafu yao. Christopher Columbus alidhani kwamba alikuwa amegundua kitu cha ajabu au uchawi, na aliporudi kwao, alichukua baadhi ya majani na mbegu za mmea huo hadi Uhispania, na kwa njia hii, tumbaku ikaingia Ulaya. Watu wa Ulaya waliupa mmea huo jila la tobacco. Zawadi hiyo ya kikoloni, iliyoambatana na mtazamo kwamba inatibu maumivu, imeathiri karibu jamii zote za dunia ya leo, na waraibu wake wanaiona kuwa ni muhimu zaidi kuliko hata chakula cha usiku!
Nchi kubwa zinazozalisha sigara za Magharibi, licha ya kujaribu kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo katika nchi zao, zinasafirisha sehemu kubwa ya uzalishaji wao wa sigara katika nchi zinazoendelea na maskini, na kuzidisha matumizi ya sigara na tumbaku katika nchi hizo kwa mbinu mbalimbali za utangazaji na propaganda.
Siku hii imepewa jina la siku ya Mapambano Dhidi ya Tumbaku Duniani ili kuanzisha harakati ya kimataifa ya kupambana na hatari hii kubwa kwa afya ya binadamu. Takwimu zinaonyesha kuwa, uvutaji sigara huua mamilioni ya watu kila mwaka.
