Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (72)
Ahlan Wasahlan wapenzi wasikilizaji wa Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Muhammad Hussein Fadhil Toni. Tulisema kuwa, Muhammad Hussein Fadhil Toni alizaliwa usiku wa 25 Muharram 1298 Hijria sawa na tarehe 28 Disemba 1880 Miladia. Alizaliwa katika moja ya maeneo ya Khorasan Kusini kwa jina la Ton ambalo leo hii linajulikana kwa jina la Ferdows. Baba yake ni Mulla Abdul-Adhim ambaye alikuwa mtoa waadhi mashuhuri katika mji huo na alikuwa na umashuhuri huku akipendwa mno na watu wa eneo hilo. Baba huyo alifahamu na kutambua haraka mno kipaji alichokuwa nacho mtoto wake. Kabla ya Muhammad Hussein kufikia umri wa masomo, alimchukua na kumpeleka katika maktaba ya nyumbani. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 72 ya mfululizo hii kitamzungumzia msomi mwingine wa Kishia anayejulikana kwa jina la Hassan Ali Nokhodaki Isfahani. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Hassan Ali Nakhodaki Isfahani alizaliwa 4 Mei 1863 katika mji wa Isfahan Iran.
Baba yake ni Ali-Akbar Meghdadi Isfahani. Mzazi wa Hassan Ali aliishi katika karne ya 13 Hijria na alifahamika mno kwa uchajimungu na kufanya ibada na alikuwa na maingiliano na Maulamaa na wasomi wakubwa wa elimu ya irifani katika mji wa Isfahan katika zama hizo. Ali-Akbar Meghdadi Isfahani alikuwa miongoni mwa muridi na watu waliokuwa na mapenzi na ufuasi mkubwa na Muhammad Swadiq Takht Pooladi. Kila usiku wa Jumatatu na Ijumaa alikuwa akienda kuzuru kaburi lake. Ali-Akbar Meghdadi Isfahani alikuwa na mapenzi maalumu na masharifu na alikuwa akiwahudumia mno watu wanaotokana na kizazi cha Bibi Fatma Zahra (as). Kwa muda mrefu alikuwa akitamani Mwenyezi Muungu amruzuku mtoto wa kiume na hivyo akaamua kutawasali haja yake hiyo kupitia kwa Maasumina (as). Hatimaye Mwenyezi Mungu akamruzuku mtoto wa kiume ambaye aklimpatia jina la Hassan Ali ambaye ndiye tunayemzungumzia katika kipindi chetu cha leo.
Tangu utotoni Hassan-Ali alikuwa pamoja na baba yake kila usiku ambao alikuwa akikesha na kufanya ibada. Alikuwa na miaka saba wakati Muhammad Swadiq Takht Pooladi alipomkubali kuwa mwanafunzi wake. Masomo yaliyokuwa yakifundishwa na mwalimu huyo yalikuwa tofauti kabisa na masomo yaliyokuwa yakifundishwa katika maeneo mengine. Hassan Ali hakuanza na hatua ya kusoma fikihi na usul na mfano wa hayo, bali sambamba na ksoma elimu na maarifa tangu mwanzoni tu alianza hatua ya kulea nafsi na akiwa chini ya usimamizi na uangalizi wa mwalimu wake aliyekuwa amebobea katika irfani alikuwa akijishughulisha na tahajudi na kufanya ibada. Katika kipindi hiki alisoma fasihi ya lugha ya Kiarabu, fikihi, usul, mantiki na falsafa kwa walimu wakubwa wa Isfahan katika zama hizo akiwemo Mirza Jahangir Khan Ghashghaei tuliyemzungumzia katika kipindi chetu kilichopita.
Wakati Hassan-Ali alipofikisha umri wa miaka 11 Muhammad Swadiq Takht Pooladi aliyekuwa mwalimu wake wa Irfan aliaga dunia na ni katika miaka hiyo ambapo alianza kufanya safari katika maeneo mbalimbali. Alifanya safari nyingi katika miji ya Mash'had, Isfahan na Shiraz Iran na vilevile Najaf Iraq na katika safari zote hizi alifanya hima na juhudi za kuongeza elimu na maarifa yake. Hassan Ali alikuwa akiamini kwamba, ujinga katika elimu yoyote ile ni jambo lisilofaa na baada ya kujifunza elimu ya tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Wilaya na hukumu za sheria kuna ulazima pia wa kufanya hima na idili ya kutafuta na kujifunza elimu zingine. Itikadi yake hii ndio iliyomfanya akiwa katika mji wa Shiraz achukue uamuzi wa kujifunza elimu ya tiba na kufanya hima kubwa katika uga huo sambamba na kujifunza siri mbalimbali za mimea amabyo ni dawa kutoka katika kitabu cha Qanoon cha Ibn Sina. Katika kipindi cha mwishoni mwa umri wake, Shekhe Hassan Ali alikuwa akiishi katika kijiji cha Nukhud katika mji wa Mash'had Iran na ni kutokana na sababu hiyo akaondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Hassan-Ali Nokhodaki.
Katika kipindi chote cha kufanya safari kwa ajili ya kwenda kutafuta elimu na kuongeza maarifa, Sheikh Hassan Ali Nokhodaki hakuacha katu suala la kukesha na kufanya ibada usiku, Aidha tangu kuanzia kipindi alichokuwa na umri wa miaka 15 daima alikuwa akifunga saumu miezi mitatu ya Rajab, Shaaban na Ramadhan na kuanzia umri wa miaka 7 na katika kipindi chote cha umri wake alikuwa akikesha kwa ajili ya kufanya ibada na kuomba dua katika usiku wa kuamkia Ijumaa.
Kushikamana kwake na ibada na kumcha Mwenyezi Mungu kulimfanya akawa na karama alizopatiwa na Mola Muumba. Ayatullah Mar'ashi Najafi ameandika kuhusiana na Shekhe Hassan Ali katika kitabu chake cha al-Musalsalat fi al-Ijazat ya kwamba: Yeye alikuwa akitambulika baina ya watu kama mtu ambaye dua yake ni yenye kukubaliwa na watu wengi waliokuwa wamehangaika na kukwama katika haja na matatizo yao yakiwemo maradhi walikuwa wakimrejea ili awaombee dua; alikuwa akiwaomboa dua au alikuwa akiwaaandikia dua ya kusoma na kwa njia hiyo maradhi yao yalikuwa yakkipona na waliokuwa na matatizo Allah alikuwa akiwafungulia faraja katika shida na matatizo yao kupitia dua hizo. Pamoja na hayo yote, lakini Hassan-Ali alikuwa katika kilelele cha tawadhui na unyenyekevu na wala hakuwa na maringo wala majivuno. Alikuwa mfano wa wazi na bayana wa mchaji Mungu ambaye anamzingatia Mwenyezi Mungu tu na mwenye kujitenga kabisa na mambo ya kidunia.
Daima alikuwa akiwanasihi na kuwataka marafiki na watu wake wa karibu wawe ni wenye kuhudumia watu na wakiwa na nia ya kutatuliwa shida na matatizo yao basi watoe sadaka kwa masikini au watie nadhiri.
Sheikh Hassan-Ali alitambuliwa kama alimu na msomi aliyekuwa mahiri katika taaluma ya irfani na aliondokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Maisha yake yalitawaliwa na ibada na kumcha Mwenyezi Mungu na kujiepusha kabisa na mambo ya dunia. Alikuwa ni mtu ambaye daima alikuwa akijitahidi na kuhakikisha kwamba, anaswali Swala yake mwanzo wa wakati huku akiwa ni mwenye kudumisha ada ya kusoma Qur'ani na kutadabari maana yake nyakati za usiku.
Miongoni mwa nasaha zake kwa wengine ni: Mambo mawili ni muhimu; moja ni chakula cha halali na la pili ni kuipa umuhimu ibada ya Swala, ambapo kama mawili haya yatakuwa sahihi basi yaliyobakia pia yatatengemaa.
Aidha alikuwa akiwanasihi watu, kuhuisha nyoyo zao kwa kusema: Ya hayyu ya Qayyuum nyakati za usiku na kutoa sadaka kila siku hata kama kiwango chake kitakuwa ni kidogo.
Hassan-Ali hatimaye aliaga dunia baada ya kutumia sehemu kubwa ya umri wake katika kuhudumia watu. Aliaga dunia mwezi Shaaban 1361 Hijria na kuzikwa katika haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) katika mji wa Mash'had nchini Iran
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umemalizika. Nina wingi wa matumaini kwamba, hamtasita kujiunga name juma lijalo. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh