Jul 14, 2023 08:04 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (24)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 24 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 24.

مِنْ کَفَّارَاتِ الذُّنُوبِ الْعِظَامِ إِغَاثَةُ الْمَلْهُوفِ وَ التَّنْفِیسُ عَنِ الْمَکْرُوبِ

Moja ya kafara za madhambi makubwa ni kuwasaidia wanaoteseka na kuwatatulia mambo yao wenye shida.

Mara nyingi sambamba na kupita wakati na umri wetu, na kila tunapoangalia rekodi ya matendo yetu, hukumbwa na wasiwasi kutokana na makosa na madhambi tuliyofanya. Nyoyo zetu muda wote hutaka kufuta mitelezo na makosa yaliyomo kwenye matendo maovu katika maisha yetu. Katika hikma hii ya 24 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatupa suluhisho zuri sana linalofaa na rahisi mno. Anasema:

مِنْ کَفَّارَاتِ الذُّنُوبِ الْعِظَامِ إِغَاثَةُ الْمَلْهُوفِ وَ التَّنْفِیسُ عَنِ الْمَکْرُوبِ

"Moja ya kafara za madhambi makubwa ni kuwasaidia wanaoteseka na kuwatatulia mambo yao wenye shida." Naam, miongoni mwa kafara za madhambi makubwa ni kusikiliza kilio cha masikini na aliyedhulumiwa na kuwafariji wenye huzuni.

Kwa maneno haya ya Imam Ali AS tutaelewa kuwa, kuwasaidia  waliodhulumiwa na kuwatatulia watu matatizo yao ni moja ya njia za kusamehewa mtu madhambi yake. Kama mtu atatenda madhambi ambayo si katika kudhulumu haki za watu, anaweza kupunguza madhambi yake hayo kwa kutumia mafundisho hayo ya Imam Ali AS yaani kufuta madhambi yake kwa kuwatendea mema waja wa Mwenyezi Mungu. Hata Qur'ani Tukufu inalihimiza jambo hilo na bila ya shaka maneno hayo ya Imam Ali AS chimbuko lake ni Qur'ani Tukufu. Katika Aya ya 70 ya Surah Furqan, Mwenyezi Mungu Mtukufu analiashiria suala hilo akisema: "Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema."

Katika hikma hii, Imam Ali AS anatumia neno Malhoof. Malhof lina maana pana inayojumuisha kila mtu aliyedhulumiwa na maskini na mtu mwenye daghadagha na mashaka kama ya ugonjwa, au deni, au maskini, au mfungwa asiye na hatia na vitu kama hivyo. Mtu anayekimbilia kuwasaidia watu kama hao huwa amejiandalia mazingira ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa dhambi alizofanya. Makroob pia ni neno linalotumiwa kwa mtu yeyote mwenye huzuni; Iwe huzuni yake ni kwa sababu ya msiba wa kufiwa na mpendwa wake au huzuni ya ugonjwa au umaskini au kuharibikiwa katika maisha na huzuni nyingine yoyote.

Naam! Kilio cha mnyonge aliyekwama katika makucha ya dhuluma na kilio chake cha mwenye kuomba msaada kinafika mbali. Kuwasaidia wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu matibabu na kujinunulia dawa, kusimamia familia isiyojiweza na inayoshindwa hata kupata mahitaji yake ya kimsingi, kulipa madeni na kuachilia huru wafungwa wa makosa ya kutokusudia, kutoa msaada wa kifedha kwa mwanafunzi ambaye ameacha masomo kwa sababu ya umaskini na hata kumfariji aliyefiwa na mpendwa wake, yote hayo ni mifano ya kutekeleza mafundisho yaliyotiliwa mkazo na Imam Ali AS. Hatimaye, tunaweza kusema katika sentensi moja kwamba kuwasaidia watu katika Uislamu kwa namna yoyote ile ni njia ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu.