Duru ya 5 ya Tuzo ya Al -Mustafa
Kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 4 Oktoba, mji wa kihistoria na kiutamaduni wa Isfahan wa hapa Iran, ambao ni mojawapo ya vituo muhimu vya ustaarabu wa Kiislamu, ulikuwa mwenyeji wa duru ya tano ya Tuzo ya Al Mustafa (SAW), ambayo hafla yake imefanyika katika Kasri la Chehelsuton katika mji huo.
Shehere za utoaji tuzo katika duru hii ya tano ya tuzo ya Al Mustafa (SAW) ilifanyika Jumatatu wiki hii tarehe Pili Oktoba huko Isfahan kwa kuhudhuriwa na wasomi watajika 1,000 wa Kiirani na kutoka nchi mbalimbali. Aidha wageni 130 kutoka nchi 30 wakiwemo watunga sera wa nyanja za sayansi na teknolojia, wanasayansi, wafadhili na wanaharakati 15 wa vyombo vya habari kutoka Uturuki, Malaysia, Algeria na Wakurugenzi Watendaji wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) walishiriki kwenye hafla hiyo.
Tuzo ya al Mustafa ni tuzo ya sayansi na teknolojia inayotolewa na Iran kwa wanasayansi bora wa Ulimwengu wa Kiislamu. Wazo la kuunda na kutoa tuzo hiyo ya kielimu ya al Mustafa (SAW) lilitolewa kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa muongo wa mwaka 1390 Hijria Shamsia. Lengo la tuzo hii ni kutambua na kupongeza juhudi za wasomi wa nchi za Kiislamu katika kustawisha sayansi na teknolojia duniani. Tuzo ya Al Mustafa (Rehema na Amani ya Allah iwe juu yake na kizazi chake), ilibuniwa kama Tuzo yenye hadhi ya Kimataifa inayotolewa mara moja kila baada ya miaka miwili, baada ya utafiti wa kisayansi wa tuzo 300 za dunia na kupitia viwango vya tuzo hizo.

Jina la tuzo hii limechukuliwa kutoka katika mojawapo ya lmajina ya Mtume wetu mtukufu (SAW) yaani al Mustafa, lenye maana ya mteule. Mtume Muhammad al Mustafa (SAW) kama lilivyo neno la Mwenyezi Mungu, Qur'ani, alitilia mkazo sana na kuithamini elimu na kutafuta elimu na sayansi. Aya za kwanza zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwenye moyo uliobarikiwa wa Mtume Muhammad al Mustafa (SAW) zilikuwa wito wa kusoma na kupata elimu: "Soma kwa jina la Mola Wako aliyeumba (vitu vyote). Aliyemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma! Na Mola Wako ni Karimu sana. Ambaye amefundisha kupitia kalamu. Amemfundisha mwanaadamu aliyokuwa hayajui. (Aya 1 hadi 5 ya Suratu al Alaq).
Katika Kitabu Kitukufu cha Qur'ani, Mwenyezi Mungu Mwenye hikima siku zote hanawalingania wanaadamu na kuwaita kwenye hoja na kutafakari. Qur'ani inaitaja elimu kuwa ni nuru, na kuutambua ujinga kuwa ni giza. Aidha imeelezwa katika hadithi za Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu kwamba hekima na elimu ni kito kilichopotea cha muumini, na Mtume wa Rehma, Muhammad (SAW) ameitaja elimu na ujinga kuwa ndivyo vigezo vya kumtathimini mtu. Anasema: Watu wenye thamani ya juu zaidi ni wale wenye ujuzi zaidi, na wenye thamani ya chini ni majahili na wenye ujuzi duni zaidi.
Kwa mtazamo wa Uislamu, sayansi kwa maana ya elimu na dini ni kama mbawa mbili za ndege, ambazo kwa pamoja zinaweza kuleta amani na faraja kwa mwanaadamu na jamii ya wanaadamu. Elimu katika asili yake, ni jambo tukufu na la kusifiwa. Elimu inatokana na akili, na akili kwa upande wake ina nafasi ya juu na ya wazi. Kwa hiyo, hakuna elimu yenye manufaa au isiyofaa au ujuzi mzuri na mbaya. Njia ya kutumia elimu na sayansi ndiyo inaweza kuifanya iwe muhimu na yenye manufaa au la. Dini ni mfumo wa maarifa unaofafanua na kuainisha njia na mwelekeo wa elimu na sayansi ili wanaadamu na jamii ya wanaadamu wasihangaike na kutaabika. Katika muktadhaa huo, Dakta Muhammad al Naqib bin Ali al-Attas mwanafalsafa na mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Malaysia anasema: Elimu na sayansi ya Magharibi imepoteza mwelekeo sahihi na kujitenga na Mungu.
Dakta Ali AKbar Salehi, Naibu Mkuu wa Kituo cha Sayansi na Mkuu wa Jopo Kazi la Sayansi linalosimamia Tuzo ya Al Mustafa (SAW) pia anafafanua malengo ya mashindano ya tuzo hii akisema: "Tuzo ya al Mustafa hutunikiwa wasomi ambao wamezalisha elimu yenye manufaa kwa jamii katika nyanja mbalimbali. Msingi wa tuzo hii na sayansi na mwanasayansi mwenyewe. Msomi ambaye ametafuta elimu na kufanya uvumbuzi ambao ulileta ustawi kwa wanaadamu na kuwa na manufaa katika nyanja mbalimbali amefanya harakati katika mipaka ya elimu, akapata teknolojia yenye manuufaa na kuwa na taathira katika utamaduni wa jamii. Msomi huyu lazima awe na sifa nzuri, awe mahiri katika masuala ya ufundi, mawasiliano ya hali juu, na awe na ari na shauku katika nyanja hizo. Kwa kuzingatia kuwa elimu haina mipaka, tuzo ya al Mustafa (Rehema na Amani ya Allah iwe juu yake na kizazi chake) hutolewa katika nyanja nne za sayansi na teknolojia, ikiwa ni pamoja na mawasiliano na habari, sayansi ya kibaolojia na matibabu, sayansi ya nano, na sayansi ya msingi na uhandisi.

Tuzo ya Al Mustafa (SAW) hutolewa mara moja kila baada ya miaka miiwili kwa wasomi bora wa Ulimwengu wa Kiislamu waliofanya vizuri katika nyanja zilizotajwa. Tuzo hiyo inajumuisha zawadi kadhaa ikiwa ni pamoja na kitita cha fedha cha dola laki tano (500,000) za Marekani; na hutolewa kwa washindi wote iwe ni mtu binafsi au timu ya watu kadhaa. Fedha taslimu za tuzo hii hutolewa na Mfuko wa Uwekezaji na Wakfu wa Taasisi ya Al Mustafa, na serikali haihusiki katika kudhamini fedha hizo.
Taasisi ya Al Mustafa inalenga kuandaa mazingira yanayowakutanisha pamoja wamiliki na watumiaji wa teknolojia katika nchi za Kiislamu ambao mbali na kuonyesha matunda na kudhihirisha mahitaji yao, waweze kuwasiliana kuandaa uwanja wa kushiriikiana zaidi. Lengo la Taasisi ya Al Mustafa ni kutambua na kuwaarifisha wasomi wakubwa na waliofanya vizuri katika uga wa sayansi na teknolojia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hili hufanyika kwa njia ya kutathmini miradi mbalimbali ya kisayansi na kiteknolojia na kuwatunuku tuzo wanasayansi na wataalamu bora katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika tuzo hii mtu hawezi kujiteuwa mwenyewe kuwa mgombea, bali taasisi ya masuala ya sayansi yenye itibari na inayofahamika inaweza kuwaarifisha wagombea kwa ajili ya kuwania tuzo hiyo; au kupitia Sekretarieti ya Tuzo ya Al Mustafa ambayo huchunguza mafanikio mahsusi ya kisayansi ya mtu au taasisi husika.
Wagombea wa tuzo ya Al Mustafa huchaguliwa kutoka maeneo mbalimbali duniani. Wasomi Waislamu na wasio Waislamu wenye utaifa wa nchi wanachama wa OIC au wanasayansi ambao wana ushirikiano mkubwa wa kisayansi na nchi za Kiislamu wanaweza kuteuliwa kuwania tuzo hiyo. Kazi zilizochaguliwa zinapasa kuwa katika mipaka ya ujuzi na uvumbuzi na ziwe zenye uhalisia. Uvumbuzi na kutokuwa na mfano ni miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa katika utoaji wa tuzo ya Al Mustafa. Kazi iliyochaguliwa lazima iwe ya vitendo na iwe na athari maalumu katika maisha ya watu na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Hafla ya utoaji Tuzo ya Al Mustafa (SAW) hufanyika sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Umoja na sherehe za Mauliidi na kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), yaani kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal. Katika tuzo ya mwaka huu ya Mustafa baada ya majaji 202 wa kimataifa kupokea maoni na kupitia faili zaidi ya 2600 ya masuala ya sayansi katika nyanja husika; katika uteuzi wa mwisho, watu watatu ambao ni wakazi na wasio wakazi waliteuliwa; na wawili kutoka nchi za Kiislamu wamechaguliwa kuwania tuzo hiyo katika duru hii ya tano.
Katika kundi la wateule wasio wakazi katika duru hii ya tano mwaka (2023), Prof. Ahmed E. Hassan, mwanasayansi wa Misri na Profesa katika Chuo Kikuu cha Queen's Canada, aliyefanya utafiti chini ya anwani "Kuchunguza Hifadhi za Programu (MSR)" katika uwanja wa sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano, pamoja na Prof. Omid C. Farokhzad, kwa pamoja wametunukiwa tuzo ya utafiti kuhusu "ubunifu, ustawi na tathmini ya kimatibabu ya dawa mpya katika uwanja wa sayansi, teknolojia, biolojia tiba.
Katika kipengee cha wateule wanaoishi katika nchi za Kiislamu, Profesa Samia J. Khoury mzaliwa wa Lebanon na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Beirut aliyewasilisha mada ya utafiti kuhusu "njia mpya katika matibabu ya ugonjwa wa MS, sababu za ugonjwa huko na njia za udhibiti, katika uga wa sayansi ya baolojia na tiba, Profesa Murat Uysal, mzaliwa wa Uturuki na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha New York tawi la Abu Dhabi nchini Imarati, ambaye aliwasilisha mada yake chini ya anwani: Mawasiliano ya bila nyaya (wireless) katika uwanja wa habari na mawasiliano", na Profesa Ahmad Fauzi Ismail raia wa Cambodia, mhadhiri na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Malaysia aliyewasilisha mada yake kuhusu ustawi wa teknolojia ya utando (membrane) na matumizi yake katika nyanja za sayansi msingi na masuala ya uhandishi, wote walichaguliwa kuwania tuzo ya Al Mustafa.
Ni vyema kutaja hapa kuwa, mbali na kufanyika hafla kuu ya utoaji tuzo, mambo mengine ya kisayansi pia hufanyika kandokando ya shughuli hiyo. Miongoni mwa mambo hayo ni vikao vya kubadilishana uzoefu katika masuala ya sayansi na teknolojia (Science and Technology Exchange Program) STEP ambavyo hufanyika kwa ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Iran na idadi kadhaa ya wanasayansi watajika katika uwanja huo. Jukumu muhimu la STEP ni kuchunguza changamoto kuu za Ulimwengu wa Kiislamu. Mpango huu unatekelezwa lengo likiwa ni kustawisha mtandao wa mawasiliano baina ya wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kalibu ya matukio ya kimataifa, kuandaa uwanja wa kupanua ushirikiano sambamba na kuendeleza shughuli za kisayansi na kiteknolojia katika nchi za Kiislamu.