Ukweli Uliopinduliwa na Wamagharibi
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nami katika kipindi chetu cha wiki hii cha Makala ya Wiki. Leo tunachunguza madai ya nchi za Magharibi eti ya kufanya hisani na kujali haki za binadamu, tukiangazia hali ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza katika kipindi cha sasa cha mashambulizi ya kikatili ya Israel yanayofadhiliwa na Marekani na washirika wake dhidi ya watu wa Ghaza.
Moja ya vipengele muhimu vya mashambulizi makali ya Israel dhidi ya Ghaza ni kupindua hali halisi na ukweli wa yanayojiri Ukanda wa Ghaza na kumuweka dhalimu na katili kwenye nafasi ya mhanga na mdhulumiwa katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Katika upande mwingine, Israel inatekeleza sera za kuangamiza kabisa kizazi cha Wapalestina katika sera za vyombo vya habari na misimamo ya maafisa wa kisiasa na kijeshi ya utawala huo ghasibu. Walimwengu kwa ujumla, wanajua vyema kwamba Israel ni utawala wa ubaguzi wa rangi, apartheid; Lakini katika matukio ya sasa huko Gaza, imekwenda mbali zaidi ya hapo na kuwavua watu wa Ghaza Naam, umesikia vizuri, kwani haya ni matamshi yaliyotolewa na waziri wa vita wa Israel aliyesema mbele ya vyombo vya habari vya dunia kwamba: "Israel inapigana na wanyama wanaojidhihirisha kuwa ni binadamu!"
Matamshi haya hayakutolewa kwa jazba na hisia za mihemko ya hali mbaya; bali yanaakisi imani na itikadi ya watawala wa Israel. Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, pia amesema: "Ni wazi kwamba tunamnyima adui yetu maji na umeme." Gideon Levy, mwandishi wa habari wa Kiyahudi wa gazeti la Haaretz, anasema: "Kuwatambua Wapalestina kuwa si binadamu" ni moja ya sababu kuu za kimya kinachoshuhudiwa sasa mbele ya ukatili unaofanyika huko Ghaza.”
Mienendo ya kibaguzi ya Israel dhidi ya Wapalestina na kuwavua sifa ya binadamu wakazi halisi wa Palestina si suala geni. Kwa miaka 75 sasa, Israel imekuwa ikitekeleza sera ya kuangamiza kizazi cha Wapalestina kwa msingi wa nadharia potofu ya "ardhi isiyo na watu kwa ajili ya watu wasio na ardhi" kwa msaada wa madola ya kikoloni. Israel ni dola la watu wanaojiona kuwa "wateule wa Mungu"; na kaumu ambayo sambamba na kujiarifisha kuwa mhanga, inajipa haki ya kufanya chochote, ikiwa ni pamoja na kuvamia na kukalia kwa mavavu ardhi za mataifa mengine, kuwafukuza na kuua wenyeji wa ardhi zinazokaliwa, na wakati huo huo kuwavua sifa ya binadamu. Inasikitisha sana kuona nchi za Magharibi zikisalimu amri mbele ya ubaguzi rasmi wa rangi unaotawala Israeli.
Katika kipindi cha historia ya Umoja wa Mataifa, Marekani imetumia kura ya turufu mara 83, ambapo mara 53 ilikuwa kwa ajili ya kuzuia ukosoaji wa aina yoyote wa uvamizi na ukatili wa Israel. Tumewasikia mara nyingi viongozi wa nchi za Magharibi wakisema kwamba "Israel ina haki ya kujilinda", lakini hatujawahi hata siku moja kusikia wakisema kwamba "Palestina nayo ina haki ya kujilinda". Ukweli ni kwamba, katika sera za kigeni za Marekani na nchi nyingi za Magharibi, Israel ni mwana mdekezwa ambaye inajuzu kukanyaga kanuni na sheria zote kwa ajili ya kumlinda na kumkingia kifua.
Madola ya Magharibi hayajui mpaka katika kulikingia kifua dola bandia la Israel. Daima yamekuwa yakisisitiza tu haki ya utawala wa Kizayuni ya kuwakandamiza Wapalestina huko Ghaza katika kukabiliana na operesheni ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba.
Waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni hawatilii maanani au bora tuseme kwamba, hawataki kujua nini Israel inawafanyia watu wa Ghaza ambalo linawalazimisha kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Wazayuni hususan walowezi maghasibu.
Inatupasa kueleza hapa kuwa, historia ya mzozo wa Palestina na Israeli na kuvamiwa ardhi hiyo haikuanza kwa habari za jioni ya tarehe 7 Oktoba mwaka huu 2023. La hasha. Ni kwa zaidi ya miaka sabini sasa ambapo Wapalestina wamekuwa wakipigania haki ya kuwepo, ambayo inafungamana na utambulisho wao, yaani, ardhi ya mababu zao, historia, lugha na utamaduni wao. Kwa miaka sabini, wameikalia kwa mabavu ardhi ya taifa na kubuni utawala ambao hauzingatii mkataba wowote wa amani, azimio lolote la Umoja wa Mataifa, au kanuni zozote za kibinadamu. Mbali na Palestina, Wazayuni wamevamia ardhi zote zinazoizunguka Palestinana kama ardhi za Misri, Syria, Jordan na Lebanon na kupora kipande cha kila moja ya nchi hizo. Pamoja na hayo, nchi za Magharibi zimekuwa zikiunga mkono utawala huu ghasibu kila uchao na kuwalaumu na kuwatishia wale wanaovamiwa na ardhi zao kuchukuliwa kwa mabavu. Huku ndiko tunakosema, ni kumuweka dhalimu, katili na muuaji kwenye nafasi ya anayeuawa na kudhulumwa.
Miongo kadhaa iliyopita nchi za Magharibi zilianzisha mazungumzo eti ya amani ili kuhalalisha utawala bandia wa Israel na sera zao za kuunga mkono utawala wa kibaguzi. Hadi sasa, mazungumzo ya Magharibi na Israel na Palestina yamekuwa "mazungumzo ya upanga na shingo"; Ni mazungumzo ya: Vipi tutakata vichwa vyenu na vipi tutakufukuzeni kutoka kwenye nyumba zenu? Wanataka kulifuta na kulinyamazisha kabisa taifa zima. Jeshi la Kizayuni limekuwa miongoni mwa majeshi yenye nguvu katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa msaida wa nchi za Magharibi. Shirika la kijasusi la Israel, MOSSAD, ni mojawapo ya mashirika ya kijasusi yanayoogofya sana duniani. Shirika hilo limeua mamia ya wapigania uhuru wa Kipalestina katika sehemu zote za dunia, na licha ya jinai, uhalifu na uvamizi wawa Israel, Wamagharibi wamebadilisha nafasi ya dhalimu na mdhulumiwa. Wapalestina wamepachikwa jina la “magaidi” na Wazayuni maghasibu na katili wanadhihirishwa kuwa ndio wanaodhulumwa na Wapalestina! Hii ndiyo taswira ambayo Wazayuni waliiwasilisha kwa ulimwengu. Nchi za Ulaya na Marekani pia ziliiunga mkono Israel kwa kuzingatia taswira hiyo eti ya kudhulumiwa Wazayuni, na kuwaweka wapigania uhuru wa Kipalestina katika orodha ya magaidi!
Pamoja na hayo, Lakini si Wazayuni wala waungaji mkono wao wote wa Kimagharibi walioweza kuwasahaulisha walimwengu kadhia ya uhuru wa Palestina licha ya kutumia suhula zote za kisiasa na taasisi za kimataifa ili kuhalalisha utawala bandia wa Israel.
Dhulma ya miaka 70 ya Wazayuni dhidi ya Palestina imeunda miaka 70 ya kudhulumiwa na mapambano ya Wapalestina. Operesheni ya kushtukiza ya harakati ya mapambano ya Hamas ndani kabisa ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kutekwa baadhi ya vituo na miji ya Wazayuni na vilevile kuchukuliwa mateka makumi ya Waisraeli ni ishara nyingine ya uhai wa mapambano ya kupigania uhuru ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Operesheni ya tarehe 7 Oktoba kwa mara nyingine imethibitisha uongo wa ngano ya eti kutoshindwa kwa vyombo vya ujasusi na usalama vya Israeli. Kipigo Kilichoipata Israel katika operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa ya wanamapambano wa Kipalestina na hasara zake kubwa haina kifani katika historia ya uvamizi wa maghasibu Wazayuni.
Wanamapambano wa Kipalestina walifanya operesheni hiyo katika hali ambayo Ghaza imefanywa jela kubwa zaidi ya wazi duniani yenye zaidi ya wafungwa milioni mbili na iko chini ya mzingiro wa pande zote wa jeshi la Israel. Wazayuni hawajatosheka na mzingiro wa Ukanda wa Ghaza na wameua shahidi maelfu ya Wapalestina kwa kuwashambulia kwa mabomu kwa kisingizio cha kuwalenga makamanda wa kambi ya muqawama. Mwaka 2022, Israel iliwaua Wapalestina 220 katika Ukanda wa Ghaza pekee. Sasa na baada ya kupata kipigo kikubwa zaidi kutoka kwa wapigania uhuru wa Ukanda wa Ghaza, Wazayuni wanataka kuwapa adhabu ya pamoja Wapalestina milioni mbili na laki tatu wanaoishi katika Ukanda wa Ghaza.
Ukanda wa Gaza ndio eneo lenye watu wengi zaidi duniani. Ndege za kivita za Kimarekani F-16 zinazomilikiwa na Israel zimedondosha maelfu ya tani za mabomu katika eneo hilo dogo na lenye idadi kubwa ya watu. Lengo la Wazayuni ni kuugeuza Ukanda wa Gaza kuwa ardhi iliyoteketea kwa moto na kuiangamiza harakati ya Hamas. Nchi za Magharibi zinazodai kutetea uhuru na haki za binadamu, zinasimama pamoja na Wazayuni na kuunga mkono mauaji ya maelfu ya raia, wanawake na watoto wa Palestina. Nchi hizo za Magharibi zimeenda mbali zaidi katika kuwaunga mkono Wazayuni, na sasa zimepiga marufuku hata mikusanyiko tu ya kuwaunga mkono watu wa Palestina na kuwawekea vifungo vya jela wale wanaokusanyika kueleza maoni na itikadi zao.
Hata hivyo inatupasa kusema hapa kuwa, zama za kuwadhihirisha Wazayuni kuwa ni wahanga na watu wanaodhulumiwa na kuunga mkono jinai zao bila ya kukabiliwa na jibu la walimwengu, zimepita na kuyoyoma. Sasa, mataifa mbalimbali duniani yamefahamu sura halisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Inatosha kuanganisha kiwango cha uungaji mkono wa walimwengu kwa Wapalestina katika mitaa ya nchi za Ulaya na Marekani na katika mitandao ya kijamii na kulinganisha na kiwango cha uungaji mkono kwa Wazayuni maghasibu. Naam, historia ya miaka 75 ya kukaliwa kwa mabavu Palestina imethibitisha kwamba, ukatili na mauaji haviwezi kulinda amani na usalama wa Israel, na kwamba mauaji ya kimbari hayawezi kuvunja azma na irada madhubuti ya wapigania uhuru.