Kukumbuka siku ya kufariki dunia Bibi Maasuma SA
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyofariki dunia Bibi Faatima al Maasuma 'Alayha Salam', mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (SAW).
Mtume Mtukufu (SAW), Maimamu Watoharifu (AS) pamoja na watoto wao watukufu wana daraja na utukufu mkubwa miongoni mwa viumbe vyote.Mwenyezi Mungu SW amewafanya kuwa viigizo vya kweli kati ya wanaadamu. Kadiri ufahamu na maarifa kuhusiana na watukufu hao yanavyozidi kuongezeka, ndivyo mtu anavyohisi mapenzi na mahaba zaidi kwa watukufu hao moyoni mwake. Hakuna shaka kuwa, mapenzi ya kweli hupatikana kutokana na kuwafahamu na kuwajua vyema watu wao watukufu. Moja ya njia za kuweza kuwafahamu mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kutwalii na kutafakari sira na mwenendo wa maisha yao, na pia kukumbuka nafasi ya kimaanawi na fadhila zao za kiakhlaki. Njia hiyo ya ufahamu mbali na kuwa kiasili huleta athari muhimu ya kujenga na kuzidisha mapenzi nyoyoni, pia humfanya mtu afuete mafunzo yao na kuiga mifano yao. Hii ni kwa sababu, hakuna mtu anayeweza kupata malezi sahihi, saada na kufikia ukamilifu, isipokuwa atakapokuwa tayari kufuata njia na kuiga watu ambao wamepata daraja ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa watukufu hao ni Bibi Fatima al Maasuma (A.S) binti wa Imam Mussa bin Jaafar (A.S), ambaye hii leo ni siku ya kukumbuka kifo chake. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na haswa wapenzi wa Mtume Mtufuku (SAW) na watu wa nyumba yake tukufu kwa mnasaba wa kufariki dunia mjukuu huyo mtukufu wa Mtume.
Kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu, kuwa mwanaume au mwanamke sio kigezo cha kuwa mbora au kuwa mtukufu zaidi, kwani mafunzo ya Uislamu yanamlenga mwanadamu na wala sio jinsia ya mtu. Kama ambavyo wanaume kama Mitume na Maimamu watoharifu (A.S) walivyokuwa mifano bora kwa wengine, wanawake watukufu pia kama vile Bibi Asya mke wa Firaun, Bibi Maryam, Bibi Khadija, Bibi Fatimatul Zahra, Zainabul Qubra na Fatima al Maasuma (A.S) vilevile wanahesabiwa kuwa vigezo na mifano bora kwa wanawake wote duniani. Kwa msingi huo, kutwalii historia ya maisha, sira ya kivitendo na yaliyobainishwa kuhusiana na mienendo ya watukufu hao walioteuliwa na Mwenyezi Mungu, ni mfano unaofaa kwa ajili ya kufikia saada, ukamilifu na maisha bora ya mwanadamu. Pia kuwafahamu vyema watu hao huwa ni mwanga wa uongofu katika maisha ya watu wote. Ni wazi kuwa mche utakaomea katika bustani ya Uimamu na kupata nishati kwa kustafidi na nuru hiyo ya fadhila, kila muda unavyopita ndivyo unavyozidi kubadilika na matawi yake huchanua na kupendeza, kutokana na shajara njema ya familia ya Mtume Mtukufu. Bibi Fatima al Maasuma (A.S) ni binti anayetoka katika familia hiyo, ambaye alizaliwa mjini Madina tarehe Mosi Dhil Qaadah mwaka 173 Hijiria. Bibi huyo alilelewa na kuishi katika nyumba aliyokuwa pia akiishi baba yake Imam Mussa Khadhim (A.S) na kaka yake Imam Ridha (A.S). Bibi Fatima al-Maasuma 'Alayha Salaam' alikulia katika malezi ya ucha-Mungu na katika chemchemi ya maarifa, hekima, elimu na zuhdi na kupata utakasifu mkubwa wa mwili na roho. Akiwa bado mdogo, alikumbwa na msiba mkubwa wa kuuawa shahidi baba yake kipenzi kwenye jela ya Haroun katika mji wa Baghdad. Hivyo kuanzia wakati huo akawa chini ya usimamizi na ulezi wa kaka yake Imam Ali bin Mussa ar Ridha (A.S).
Hakuna shaka kuwa chanzo kikuu cha saada na ukamilifu wa mwanadamu na kumkurubia Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kuwa na imani thabiti juu ya dhati iliyotakasika ya Mwenyezi Mungu na kufuata vyema na ipasavyo maamrisho yake. Mwenyezi Mungu ametuambia kuwa maisha mazuri ni matokeo ya imani na amali njema, na katika Suratul Nahl amemuahidi kila mwanamume au mwanamke atakayetenda amali njema, maisha mazuri. Bibi Fatima al Maasuma (A.S) ni miongoni mwa wanawake, ambaye imeelezwa kuwa aliwazidi wengine katika kufuata mwendo huo. Mtaalamu mashuhuri wa hadithi marhum Haji Sheikh Abbas Qumi anaandika kuhusiana na watoto wa kike wa Imam Mussa Kadhim (A.S) kuwa: 'Kwa mujibu wa yale yaliyotufikia, wabora kati yao ni Bibi Jalilah Muadhama na Fatima binti wa Imam Mussa al Kadhim (A.S) maarufu kama Bibi Maasuma.' Bibi huyo mwenye fadhila alikuwa na utukufu mkubwa, na Maimamu Watoharifu walikuwa wakimtaja kwa utukufu na fadhila, kiasi kwamba hata kabla ya kuzaliwa kwake, baba yake mtukufu alikuwa tayari amelisikia jina lake kutoka kwa baadhi ya Maimamu, na tayari utukufu na nafasi yake adhimu ilikuwa imeshazungumziwa. Miongoni mwa fadhila za bibi huyu Mtukufu ni 'uwezo wa kutoa shifaa.' Imenukuliwa kutoka kwa Imam Jaafar Swadiq (A.S) kwamba: ' Mwanamke kutoka katika watoto wangu atafariki dunia katika mji wa Qum, ambaye jina lake ni Fatima binti Mussa. Kutokana na shifaa yake wafuasi wangu wataingia peponi.'
Fadhila nyingine ya Bibi Fatima al Maasum (A.S), ni uwezo wake wa kubainisha hadithi, na kutokana na kipaji hicho alijulikana kwa jina la 'Muhadditha.' Jina la Fatima binti Mussa bin Jaafar pia linaonekana katika silsila ya sanadi za baadhi ya wapokezi wa hadithi, na maulamaa wa Kisuni na Kishia wanazielezea riwaya zake kuwa ni sahihi na zenye kukubalika. Miongoni mwa hadithi hizo ambazo mapokezi yake yanaenda hadi kwa Bibi Fatimatul Zahra (A.S) na Mtume Mtukufu (SAW) ni 'Hadith ya Ghadir' na 'Hadithi ya Manzila', hadithi ambazo zinaelezea utukufu wa Imam Ali (A.S). Bibi Fatima al Maasuma (A.S) alikuwa akimpenda sana kaka yake Imam Ridha (A.S). Mapenzi na upendo huo haukutokana tu na uhusiano wa kinasaba kati ya kaka na dada, bali ufahamu wa bibi huyo mtukufu juu ya nafasi ya wilaya na uongozi katika Uislamu. Mapenzi hayo yalisababisha bibi huyo kufunga safari ambayo ilikuwa na nafasi muhimu katika maisha yake.
Safari ya Imam Ridha ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marwa nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Kiabbasi, na mtukufu huyo alielekea katika mji wa Khorasan nchini Iran pia bila kufuatana na mtu yoyote wa familia yake au watu wa nyumbani kwake. Mwaka mmoja baada ya kuhijiri kaka yake, Bibi Fatima al Maasuma huku akifuatana na baadhi ya kaka zake na watoto wa kaka zake alianza safari ya kuelekea Khorasan kwa ajili ya kumuona kaka yake huyo na muhimu zaidi kutekeleza jukumu la kutetea nafasi ya wilaya na uongozi. Msafara wake ulipokelewa na kulakiwa na watu wengi katika kila mji waliopita. Bibi huyo mtukufu pia alifikisha ujumbe wa kudhulumiwa na kuachwa pekee kaka yake kwa waumini na Waislamu wa sehemu alizopitia, kama alivyofanya Bibi Zeynab (A.S), na kuonyesha upinzani wake na wa Watu wa Nyumba ya Mtume (A.S) dhidi ya utawala uliokuwa umejaa hila wa Bani Abbas. Kwa ajili hiyo, msafara wa bibi huyo mtukufu ulipofika katika mji wa Save, baadhi ya watu waliokuwa wakiwapinga Ahlul Bait waliokuwa wakiungwa mkono na vibaraka wa utawala huo waliuzuia msafara huo, na kupigana na waliofutana na bibi huyo suala ambalo lilisababisha karibu wanaume wote wa msafara huo kuuwawa shahidi. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya Bibi Fatima al Maasum pia alipewa sumu na waovu hao. Alaa Kulli hal Bibi Fatima al Maasuma aliugua, labda kutokana na majonzi na huzuni kubwa iliyotokana na tukio hilo au kutokana na athari ya sumu aliyopewa, na kwa kuwa hakuweza tena kuendelea na safari yake kuelekea Khorasan, aliamua kwenda katika mji wa Qom. Alisema: 'Nipelekeni katika mji wa Qum, kwani nilimsikia baba yangu akisema kwamba, mji wa Qum ni kituo cha wafuasi wetu.'
Wakuu wa mji wa Qum walipofahamu kuhusu ujio wake waliharakisha kwenda kumlaki. Mussa bin Khazraj mmoja wa wazee wa mji huo aliwatanguliwa watu wote kwenda kumlaki bibi huyo mtukufu. Tarehe 23 Rabiul Awwal mwaka 201 Hijiria Bibi Fatima al Maasuma aliwasili katika mji mtukufu wa Qum. Aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubishwa kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW).
Mwishowe katika siku kama ya leo yaani tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake Imam Ridha (A.S), Bibi Fatima al Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Watu wa Qum na wapenzi wa Ahlul Bait waliuzika mwili wa bibi huyo mtukufu katika eneo ambalo wakati huo lilikuwa nje ya mji lililojulikana kama 'Bustani ya Babol'. Baada ya kuzikwa Mussa bin Khazarj Saibani aliweka juu ya kaburi la mtukufu huyo mikeka mingi. Hali hiyo ilibaki hivyo hadi mwaka 256 Hijiria ambapo Bibi Zeynab binti wa Imam Jawad (A.S) alijenga kuba la kwanza juu ya kaburi la shangazi yake huyo mtukufu, na kwa utaratibu huo eneo hilo alikozikwa mtukufu huyo wa Kiislamu, likawa kivutio cha nyoyo za wapenzi na maashiqi wa Ahlul Bait (A.S) na wafuasi wa Maimam Watoharifu. Kutokana na baraka ya eneo hilo, hadi hii leo mji wa Qum ni moja ya vituo vikubwa vya elimu ya Ahlul Bait na dini tukufu ya Uislamu. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na haswa wapenzi wa Mtume Mtufuku (SAW) na Watu wa Nyumba yake tukufu kwa mnasaba wa kufariki dunia mjukuu huyo wa Mtume.
Wasalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.