Nov 09, 2023 11:27 UTC
  • Kupambana na Utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mtazamo wa Uislamu

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi chetu cha Makala ya Wiki ambacho leo kinaangazia mtazamo wa dini ya Kiislamu kuhusu kujilinda na kukabiliana na ukandamizaji, uchokozi na uvamizi.

Mashambulio ya kinyama ya mabomu na makombora dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza yameamsha hasira na chuki ya walimwengu dhidi ya utawala huo. Kwa sasa swali hili la msingi linaloulizwa kwa mara nyingine tena ni kwamba: Hadi lini Palestina inapaswa kuwa chini ya utawala wa kibaguzi wa Israel, na watu wake wataendelea kuuawa shahidi, kujeruhiwa, kulazimishwa kuhama makazi yao na kufungwa jela ? Kwa nini jamii ya kimataifa inapuuza kukaliwa kwa mabavu na mauaji ya watu wa Palestina yanayofanywa na  Wazayuni, lakini katika matukio mengine yanayofanana na hayo, inachukua hatua kali na haraka?

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kuikalia kwa mabavu nchi yoyote kunalaaniwa na hakukubaliki, na watu wa nchi hiyo wana haki ya kisheria ya kuanzisha mapambano dhidi ya wavamizi hadi watakapofukuzwa. Operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa", ambayo ilifanywa na wapigania uhuru wa harakati ya Hamas hapo tarehe 7 Oktoba, iliendana na utekelezaji wa haki hii ya kisheria na ya kimantiki. Sasa tunataka kuona nini mtazamo wa dini ya Kiislamu kuhusu suala la kujilinda na kukabiliana na dhulma, uchokozi na uvamizi?

Kimbunga cha Al Aqsa

Tunapotupia jicho kwa haraka mafundisho ya dini ya Kiislamu tunaona kuwa, dini hiyo ya Mwenyezi Mungu imekuja na ujumbe wa amani, udugu na uadilifu. Lakini daima katika historia kumekuwapo watu, vikundi, na serikali au tawala ambazo zimeamua kufuata njia ya ukandamizaji na kuingilia maisha, kunyakua mali na ardhi ya mataifa mengine na kuvuruga kivitendo usalama, amani na utulivu. Katika hali hiyo ya kusikitisha, Uislamu huamua kwa dhati kumshughulikia mchokozi na dhalimu ili kwa kuondosha fitna na uovu wake, wanadamu waweze kuishi pamoja kwa amani.

Katika Uislamu, sio tu ukandamizaji wa watu wengine unaolaaniwa, lakini pia dini hiyo inalaani na kuharamisha kukubali ukandamizaji na kujisalimisha kwa watawala na wavamizi madhalimu. Mwishoni mwa Aya ya 279 ya Surah Al-Baqarah, Mwenyezi Mungu SW anasema kwamba: "Usidhulumu wala kudhulumiwa." Kwa hiyo, mapambano na muqawama wa wananchi wa Palestina ni utekelezaji wa kanuni hii ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu. Naam, usidhulumu wala usikubali kudhulumiwa. Suala hili pia limeelezwa kwa uwazi katika Aya za 39 na 40 Suratul Hajj zinazosema: Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kusawaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu... Katika Aya ya 39, sio tu kwamba Waislamu wanahimizwa kujitetea, bali Mwenyezi Mungu ameahidi pia kuwasaidia. Jambo la kutiliwa maanani hapa ni kwamba, katika Aya inayofuata, Qur’ani inawatambulisha waliodhulumiwa kuwa ni wale waliofukuzwa kutoka katika ardhi yao, jambo ambalo linafanana sana na hali ya sasa ya watu wa Palestina. Mfano bora kabisa wa kutokubali suluhu na mapatano na dhalimu ni mapambano ya Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu kipenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (SAW), dhidi ya ukandamizaji na ufisadi wa Yazid bin Muawiya, khalifa wa utawala dhalimu na kandamizi wa Bani Umayyah. Mtukufu huyo ambaye alimuona Yazid kuwa hastahiki ukhalifa na kuwatawala Waislamu, alikataa kula kiapo cha utiifu kwake, na akaamua kupambana hadi kuuliwa shahidi katika kutetea haki na maadili ya Kiislamu. Akiwa katika medani ya vita, Imamu Hussein (AS) alisema amewekwa baina ya njia mbili, ama kuuliwa au kusalimu amri mbele ya mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kusema kwa sauti kubwa: “Haiwezekani kwetu sisi kunyenyekea na kukubali kudhalilishwa". Kwa njia hii, mtukufu huyo ni ruwaza na kielelezo chema kwa watu huru na wanaopigania haki ulimwenguni katika historia ya mwanadamu.   

Mashambulizi ya kinyama ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza 

Wanachofanya hivi sasa Hamas na makundi mengine ya kupigania uhuru ya Kiislamu ni kufuata kauli mbiu na mbinu hiyo hiyo ya Imam Hussein, ambayo mara hii imetumika dhidi ya maghasibu wasio na ubinadamu hata kidogo wa Israel. Utawala bandia wa Israel umekuwa ukiikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina kwa miaka 75 kwa usaidizi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza, na ufanya jinai zote za kutisha dhidi ya Wapalestina. Makundi ya Wapalestina yaliyokuwa yakitafuta himaya na uungwaji mkono wa kimataifa na Kiarabu katika kipindi hicho chote, yalitambua kwamba hakuna matumaini yoyote kutoka upande huo na kwamba yanapaswa kuzidisha nguvu zao za kijeshi kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na uungaji mkono wa wananchi, na kupambana na jeshi la Wazayuni maghasibu. Kwa sababu, katika Aya ya 4 ya Suratu Swaf, Mwenyezi Mungu anawataka Waislamu wajiandae na kujizatiti kadiri inavyowezekana kwa ajili ya kukabiliana na maadui zao. Kwa utaratibu huo, makundi hayo ya muqawama, hususan Hamas, yalijiimarisha ipasavyo kijeshi licha ya kuwa chini ya mzingiro wa pande zote wa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kuanza kujibu mashambulizi ya kikatili ya utawala huo.

Wanamuqawama wa harakati ya Hamas ya Palestina 

Wapenzi wasikilizaji, Qur'ani Tukufu na hadithi za Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake zimehimiza sana suala la Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kumtia adabu dhalimu kutokana na umuhimu wake mkubwa katika kurejesha amani na utulivu wa jamii. Kwa mfano tu Aya ya 4 ya Suratu Swaf inasema: Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaopigana katika Njia Yake kwa safu, kama kwamba wao ni jengo liliojengwa kwa risasi (na kukamatana). Vilevile imenukuliwa kutoka kwa Mtume wetu, Muhammad (SAW) kwamba amesema: Juu ya kila jema kuna jema bora zaidi mpaka mtu auliwe katika njia ya Mwenyezi Mungu; Na akiuliwa katika njia hiyo hakuna jema zaidi juu yake.

Vilevile khalifa na wasii wake, Imam Ali bin Abi Twalib anasema: Jihadi ni moja kati ya milango ya Pepo, ambao Mwenyezi Mungu ameufungua kwa ajili ya mawalii wake makhsusi...”

((((Kwa mujibu wa mtazamo huo wa Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema kuhusiana na kadhia ya Palestina kwamba: "Suluhisho pekee la suala la Palestina ni muqawama na mapambano." ))))))

Hivi sasa Mujahidina wa Palestina wanapigania uhuru na ukombozi wa ardhi yao iliyokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, na kwa hiyo wanayo haki ya kuipigana hadi itakaporejeshwa kikamilifu. Nukta nyingine muhimu ni kwamba, kwa kuzingatia Aya ya 75 ya Suratu Nisaa, Waislamu wengine pia wana wajibu wa kuwasaidia Wapalestina kila inapowezekana katika njia ya kuondokana na uovu na shari ya utawala wa Kizayuni. Katika Aya hiyo Mwenyezi Mungu anawakemea Waislamu akisema: Na mna nini nyinyi hampigani katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa, katika wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie kiongozi kutoka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana wapiganaji wa muqawama wa Kiislamu huko Lebanon, Iraq, Syria na Yemen, wakiwa katika hali ya umoja na mshikamano, wanawasaidia ndugu zao wa Ghaza ili kulishinda jeshi vamizi na linaloua watoto la Israel; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawaunga mkono na kuwasaidia kikamilifu. (((((Katika muktadha huo pia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhuullah Khomeini (RA), aliitaja Israel kuwa ni donda la saratani katika eneo la Magharibi mwa Asia, na kusema: "Sisi tunawaunga mkono watu wanaodhulumiwa. Yeyote anayeonewa popote alipo, tunamuunga mkono, na Wapalestina wanadhulumiwa. Israel inawadhulumu na ndio maana tunawaunga mkono."))))

 

Tags