Mauaji ya Gaza na madai ya ubinadamu ya Wamagharibi
Karibuni wasikilizaji na wafuatiliaji wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran katika Makala yetu ya Wiki hii ambayo itatupia jicho mauaji yanayofanyika Ukanda wa Gaza na madai ya Wamagharibi ya kutetea ubinadamu.
Mauaji ya watoto na wanawake wa Gaza yanayofanywa na wachinjaji wa Kizayuni yamedhihirisha upande wa pili wa madai ya kutetea ubinadamu ya Wamagharibi. Pamoja na kuwa akthari ya vyombo vikubwa vya habari vya nchi za Magharibi vinasimulia mashambulizi ya kikatili dhidi ya Gaza kwa kutegemea mtazamo wa utawala wa kibaguzi na unaouwa watoto wa Israel lakini watu waliowengi katika nchi za Magharibi wanajua vyema dhulma na ukandamizaji wanaofanyiwa Wapalestina kwa miongo kadhaa sasa. Tangu kuanza mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, miji mikubwa barani Ulaya imeshuhudia maandamano makubwa ya kuipinga Israel na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina wa Ukanda wa Gaza. London, Edinburgh, Paris, Berlin, Brussels na miji mingine mingi ya Ulaya na Marekani pia imeshuhudia maandamano ya wananchi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel. Maandamano ya London yalihudhuriwa na watu wengi zaidi ikilinganishwa na miji mingine ya Ulaya. Maandamano hayo yalifanyika katika hali ambayo, Rishi Sunak, Waziri Mkuu wa Uingereza, alitangaza kuwa hakufurahishwa na hatua ya Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo ya kutoa kibali cha kufanyika maandamano hayo.
Wakati huo huo, msimamo wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wa kuunga mkono utawala wa haramu wa Israel unaoendelea kuuwa watoto, uliibua changamoto kwa Waziri Mkuu, Rishi Sunak, na miito ya kumtaka ajiuzulu. Suella Braverman Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Uingereza alidai kuwa washiriki katika maandamano hayo wanataka kuangamizwa Israel na akayataja maandamano ya waungaji mkono wa Palestina kuwa "maandamano ya chuki". Braverman pia aliwataja washiriki katika maandamano hayo kuwa genge la wahuni, licha ya kwamba yalifanyika kwa amani pasina ghasia zozote. Kwa mujibu wa taratibu za serikali ya Uingereza, kabla ya kutoa hotuba yoyote, kuchapisha taarifa au kuitisha mkutano na vyombo vya habari na kutekeleza ubunifu wowote mpya wa kisiasa, mawaziri wa serikali kwanza wanapasa kupata idhini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Downing Street.
Rishi Sunak, Waziri Mkuu wa Uingereza, amelazimika kumuuzulu Suella Braverman baada ya matamshi ya yake ya kuunga mkono mashambulizi ya kikatili ya Israel na mauaji ya halaiki huko Gaza, na kitendo chake cha kuwaita wanaopinga jinai na uhalifu wa Israel kuwa ni wahuni. Tukio hili linatajwa kuwa ni la nadra kushuhudiwa nchini Uingereza. Uingereza ni baba wa kambo wa utawala bandia wa Israel. Utawala huo usingeundwa bila ya uungaji mkono na himaya ya Uingereza kwa takwa la Wazayuni la kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuasisi utawala bandia wa Israel.
Wasikilizaji wapendwa, jinai zinazofanywa huko Gaza zinapaswa kukomeshwa kwa njia yoyote ile. Kwa sasa utawala bandia wa Israel umegonga mwamba mbele ya fikra za waliowengi duniani. Sera za kujidhihirisha kuwa mdhulumiwa na kwamba Wayahudi ni wahanga, na vilevile kutambuliwa upinzani wowote dhidi ya jinai za Israel kuwa ni chuki dhidi ya Wayahudi hazina tena mnunuzi. Katika siku za mwanzo za mashambulizi makubwa ya Israel huko Gaza serikali za nchi za Ulaya zilitangaza kuwa uungaji mkono wowote kwa mapambano ya Palestina ni uhalifu na zilipiga marufuku maandamano ya kupinga jinai za Wazayuni Ukanda wa Gaza. Hata hivyo matabaka mbalimbali ya watu wanaopinga maangamizi ya kizazi cha Wapalestina yalimiminika kwa wingi katika mitaa ya miji mbalimbali, kinyume na ilivyotazamiwa na tawala za Ulaya, na kutaka kusitishwa mara moja uhalifu wa Israel. Waandamanaji dhidi ya Israel tarehe 11 mwezi huu wa Novemba walielekea katika ubalozi wa Marekani baada ya kukusanyika katika bustani ya Hyde Park mjini London. Waandamanaji hao pia walipiga nara na kulaani sera za nchi za Magharibi za kuukingia kifua utawala wa Kizayuni na kimya cha nchi hizo mbele ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na Israel.
Kuchukukizwa kwa walimwengu na jinai za Wazayuni dhidi raia wa Ukanda wa Gaza si jambo linaloweza kupuuzwa kwa urahisi. Uchunguzi rasmi wa maoni unaonyesha kuwa, sehemu kubwa ya vijana wa Kimagharibi hawaafikiani na hatua na vigezo vya kindumakuwili katika suala la haki za binadamu. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, hata huko Marekani asilimia ya watu wenye umri wa miaka 18 hadi 29 ambao wana mtazamo hasi kuhusu Hamas haizidi asilimia 40. Kiwango ambacho ni kidogo kuwahi kushuhudiwa nchini Marekani ambako vyombo vya habari vnaiarifisha Hamas kuwa ni kundi la kigaidi! Aidha uchunguzi wa maoni katika tovuti ya You-Gov huko Uingereza hadi kabla ya maafa ya karibuni unaonyesha kuwa: Idadi ya vijana walio na umri wa miaka 18 hadi 24 walioonyesha mshikamano wao kwa Palestina walikuwa karibu mara sita ya vijana walioiunga mkono Israel. Kwa maafa haya ya sasa tunaweza kusema kuwa, fikra za waliowengi duniani pia zimeeleza hisia zao kwa kiasi kikubwa. Palestina na watu wa nchi hiyo hawajawahi kuwa wahanga wa vigezo kama hivi vinavyoshudiwa vya unafiki na undumilakuwili vya nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu tangu kuasiwa utawala bandia wa Israel.
Kitu ambacho kimeibua zaidi hisia za fikra za waliowengi duniani kuhusu jinai kubwa na za kutisha za Israel katika Ukanda wa Gaza ni mauaji ya maelfu ya watoto. Takwimu zinaonyesha kuwa Wapalestina zaidi ya elfu 13,300 wameuawa shahidi tangu Oktoba 7 mwaka huu hadi sasa; ambapo miongoni mwao ni watoto kkaribu ya elfu sita. Mashahidi wengi waliosalia ni wanawake, wasiojiweza na wazee. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa takwimu hizi zinaongezeka kila baada ya saa moja. Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) limetangaza katika ripoti yake kuwa mtoto mmoja huuawa huko Gaza kila baada ya dakika kumi. Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametangaza kuwa Ukanda wa Gaza umekuwa kaburi la watoto, na kwamba jinamizi la Gaza ni zaidi ya maafa ya binadamu. Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa UN kutumia neno "kaburi la watoto" kuhusiana na hali ya Ukanda wa Gaza.
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) pia limetangaza kuwa Ukanda wa Gaza umekuwa kaburi la watoto. Watoto katika Ukanda wa Gaza hawapotezi tu maisha kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Israel bali pia kwa kukosa huduma za afya.
Licha ya takwimu zote hizi na picha za kutisha kuhusu hali mbaya ya maafa yanayowasibu raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza, serikali za nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zimezuia mara tano azimio la Baraza la Usalama la UN kwa ajili ya kusitisha vita katika eneo hilo. Marekani na nchi za Ulaya zimezuia usitisha vita na badala yake zimetuma misaada ya hali na mali ya kijeshi kwa serikali ya Tel Aviv ambayo inatumia misaada hiyo ya kijeshi kuua idadi kubwa zaidi ya watu wa Plestina.
Pamoja na haya yote, utawala wa Kizayuni hautaweza kufuta muqawama na mapambano ya kupigania uhuru huko Palestina. Hata Elon Mask, tajiri mashuhuri duniani na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X amekiri kuhusu jambo hili. Mask amesema: "Ukiua mtoto mmoja wa Gaza, unatengeneza wanachama wengi wa Hamas ambao wako tayari kufa kwa ajili tu ya kuua Mwisraeli mmoja".