Kuzaliwa kwa Nabii Isa Masih (as)
(last modified Sun, 24 Dec 2023 11:14:57 GMT )
Dec 24, 2023 11:14 UTC
  • Kuzaliwa kwa Nabii Isa Masih (as)

Disemba 25 inasadifiana na siku aliyozaliwa Masih Isa bin Maryam (AS) kwa mujibu wa imani ya Wakristo waliowengi.

Mtume huyo mwema alikuwa mtoa bishara njema na mlinganiaji wa kweli, upendo na itikadi na Mungu Mmoja. Isa Masih alizungumza kwa amri ya Mwenyezi Mungu akiwa katika susu na kuwaambia watu waliokuwa katika mghafala wa zama hizo kwamba: "Na akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na kunifanya Nabii. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo na ameniusia Swala na Zaka maadamu ni hai. Na kumtendea wema mama yangu. Wala hakunifanya jeuri, muovu. (Aya ya 30 hadi 32 Suratu Maryam)

Nabii Isa alizaliwa katika zama ambazo makundi mbalimbali ya Kiyahudi yalikuwa yamezama katika hitilafu na migawanyiko mikubwa. Makundi mawili makuu ya Wasadukayo (Sadducees) na Mafarisayo (Pharisees) yalikuwa yakidhibiti na kutawala itikadi za watu wa zama hizo. Wasadukayo (Sadducees) lilikuwa kundi la mabwanyenye na aghlabu yao walikuwa makuhani na wanazuoni wa kidini ambao walikuwa wakishirikiana na utawala wa kifalme wa Roma kwa ajili ya kulinda mafundisho na ada za kidini na hawakukabiliana kwa njia yoyote ile ya utamaduni wa Kigiriki.

 Mkabala wake, Mafarisayo (Pharisees) lilikuwa kundi lisilo la makuhani lakini lenye ushawishi mkubwa zaidi kuliko Wasadukayo (Sadducees). Kundi hili liliamini kuwa, kaumu ya Mayahudi inapaswa kuwa kaumu tofauti na iliyojitenga na kaumu nyinginezo, na haipasi kufuata kaumu hizo au kuchanganyika nazo. 

Nabii Isa Masih alizaliwa katika mazingira kama haya. Wakuu wa kaumu ya Mayahudi katika kila kundi walijua vyema sifa na alama zake kutokana na utabiri wa hapo kabla na habari walizosoma na kukusanya katika vitabu vya kale. Hata hivyo walipuuza utabiri na alama hizo tangu hapo mwanzoni na kukabiliana na Nabii huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu. Hatua ya kwanza kabisa ya Mayahudi hao ilikuwa kumtuhumu mama yake Masih, Bibi Maryam AS kuwa ni fasiki na muovu ili wapate kumrujumu kadamnasi. Hata hivyo njama hiyo ilifeli, na Isa na mama yake, Bibi Maryam, wakaokoka kifo na vitimbi vya Mayahudi baada ya Masih kuzungumza akiwa kwenye susu na kusema: "Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na akanijaalia kuwa Nabii."

Nabii Isa AS alibaathiwa na kuamrishwa kutangaza ujumbe wa Mwenyezi Mungu baina ya Bani Israel akiwa na umri wa karibu miaka 30. Alifanya jitihada kubwa za kuwaongoza katika ukweli na haki na kuwaondoa katika upotovu. Aliwabainishia halali na haramu na kuwahalalishia mengi waliyokuwa wamekatazwa. 

Mbali na kuwaongoza watu katika njia ya haki, Nabi Isa alikuwa akitibu wagonjwa. Alikuwa akitibu vipovu na barasi au mbalanga na kufufua wafu kwa uwezo wake Mola Muumba. Vilevile alikuwa akitengeneza ndege kutoka kwenye udongo. Daima alikuwa msaidizi wa watu waliokuwa wakidhulumiwa na kukandamizwa na aliwakirimu na kuwafanyia ihsani sana watoto na wanawake. Wakati huo huo alipinga vikali sheria kali za baadhi ya Mafarisayo (Pharisees) na misimamo ya kuchupa mipaka ya Zealots.   

Nabii Isa AS alipata mashaka na tabu kubwa katika kuwaongoza Wayahudi na kuwaelekeza katika njia sahihi. Katika mashaka hayo alielewa kwamba, Wayahudi wanashikilia maasi na hawakuwa tayari kuachana na dhambi na njia potovu. Alisimama katika kaumu yake na kusema: "Nani kati yenu atakayenisaidia katika njia ya Mwenyezi Mungu?" Watu wachache kati ya Mayahudi walijitokeza na kuitikia wito wake. Kundi hilo lilikuwa na watu wasafi ambao Mwenyezi Mungu SW anawataja katika Qur'ani tukufu kwa jina la "Hawariyyun". Kundi hili la Hawariyyun lilitangaza utayarifu wao wa kumsaidia Nabi Isa Masih katika njia ya Mwenyezi Mungu kama inavyosimulia Qur'ani tukufu katika Aya ya 52 hadi 53 za Suratu Aal Imran zinazosema:

 "Isa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba, sisi hakika ni Waislamu. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia."

Isa na wanafunzi wake hao walielekea maeneo ya kaskazini mwa Palestina na kuwafundisha watu dini halisi ya Mwenyezi Mungu. Maarifa ya dini yaliyofundishwa na Nabi Isa yaliwashangaza wengi na kuwakasirisha wanasiasa waliokuwa wakitawala jamii.

Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu alipinga vikali tabia ya watawala na makuhani wa dini ya Kiyahudi ya kuzama katika anasa na dunia. Hakuvumilia ufuska na ufisadi wa aina yoyote, na kwa msingi huo makundi yote ya Wayahudi yalianza kumkadhibisha na kumpiga vita. Makundi hayo yalitayarisha uwanja na mazingira ya kumuua mjumbe huyo mwema wa Allah SW. Ili kufikia lengo hilo chafu, Mayahudi hao walimchochea Kaizari wa Roma na kumwambia: "Kama hali hii itaendelea, ufalme wako pia utatoweka, hivyo ili kulinda utawala na ufalme wako huna budi kumuua Isa Masia!"

Isa Masih AS aling'amua njama yao na akajificha katika shamba moja akiwa pamoja na wanafunzi wake. Hata hivyo mtu mmoja kati ya wanafunzi wake aliyejulikana kwa jina la Yuda aliwaonesha maadui mahali alipokuwa amejificha. Maafisa wa utawala walivamia eneo hilo nyakati za usiku na kulizingira. Wanafunzi wa Isa Masih walipohisi hatari walimkimbia na kumuacha peke yake, lakini Mwenyezi Mungu SW kamwe hakumuacha peke yake Mtume wake mwema katika kipindi hicho hatari. Mwenyezi Mungu SW alimlinda Mtume wake na kumdhihirisha Yuda aliyekuwa akifanya ujasusi dhidi ya Nabii huyo, katika sura ya Isa, na maadui wakamkamata yeye wakidhani kuwa ni Isa Masih. Yuda alichanganyikiwa kutokana na hofu na machungu mengi na hatimaye akashindwa kuzungumza na kujiarifisha. Hata wakati alipoweza kufungua mdomo na kuzungumza, hakuna mtu aliyekuwa tayari kukubali maneno yake. Yuda alipandishwa msalabani na kusulubiwa. Watu walioshuhudia tukio hilo wote walidhani kuwa Isa Masih AS ameuawa, lakini kama inavyosisitiza Qur'ani tukufu, Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu hakusulubiwa wala kuuawa. Aya za 157 na 158 za Suratu Nisaa zinasema:

Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masih Isa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na hawakumuuwa wala hawakumsulubu, lakini walifananishiwa tu. Na hakika wale waliohitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Hawana ujuzi ila kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimwinua Kwake, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima"

Tunakamilisha kipindi chetu hiki kwa kusimulia kisa cha maisha ya unyenyekevu na upole wa Mtume huyu adhimu wa Mwenyezi Mungu.

Siku moja Isa Masih alikwenda kwa wanafunzi wake na kuwaambia: Nina haja na kama mnaahidi kunikidhia nitawaambia. Hawariyyun walisema: "Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Tuko tayari kutii na kutekeleza amri yako." Isa AS aliinuka na kisha akaelekea upande wao na kuanza kuosha miguu ya kila mmoja wao. Hawariyyun waliona haya na kujihisi vibaya, lakini walisalimu amri na kumuacha Isa Masih akiosha miguu yao, kwa kuwa walikuwa tayari wameahidi kutii na kukidhi haja yake. Baada ya kukamilisha kuosha miguu yao, Hawariyyun walisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wewe ni mwalimu wetu na unastahiki zaidi tukuoshe miguu yako badala ya wewe kuosha miguu yetu." Mtukufu Isa Masih alisema: "Nimefanya hivi ili kuonesha unyenyekevu na kuwafunza jinsi ya kunyenyekea na kufanya tawadhu'i, na baada yangu mtakaposhika usukani wa kufunza na kuwaongoza watu, mutangulize mbele njia hii ya unyenyekevu na kuhudumia viumbe wa Mwenyezi Mungu...."

Amani iwe juu yako ewe Nabii Isa siku uliyozaliwa, na siku utakayokufa, na siku utakayofufuliwa."