Feb 11, 2024 04:28 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu, kuandaliwa mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (a.t.f.s)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea mwaka 1979 kwa uongozi wenye busara na hekima wa Imamu Ruhullah Khomeini (MA).

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa mwanzo wa mapinduzi makubwa ya ulimwengu wa Kiislamu yatakaoongozwa na mbeba bendera wake, mtukufu Imamu wa zama, Imam Mahdi (atfs). Mapambano ya wananchi wa Iran ya kuiangusha serikali dhalimu ya Pahlavi na kuleta mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa na heka heka nyingi, kujitolea muhanga na hali ya panda shuka. Kuwasili Imamu Ruhullah Khomeini (RA), kiongozi kipenzi na mwanamapinduzi wa watu, Februari 1, 1979, akitokea uhamishoni nchini Ufaransa, kulipelekea mwendo wa harakati za mapinduzi hayo kuongezeka na kushika kasi na baada ya siku kumi tu tangu kuwasili kwake, mapinduzi haya yakapata ushindi tarehe 11 Februari 1979.

Kwa muktadha huo kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kupinduliwa kwa utawala wa kiimla wa mfalme Shah kulikuwa na maana ya Iran kuingia katika historia nyingine na kufungua ukurasa mpya. Takriban mwezi mmoja na nusu baadaye, katika kura ya maoni, zaidi ya 98% ya washiriki walipiga kura ya kuunga mkono kuundwa mfumo unaozingatia maadili ya Kiislamu chini ya jina la "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran". Kwa msingi huo kukapatikana mfumo wa Kiislamu wenye ridhaa ya wananchi.

Yumkini wakati huo, ni watu wachache sana wangeweza kukisia kwamba, serikali hii ya Kiislamu itakuwa na nafasi na taathira gani nchini Iran na ulimwenguni kkwa ujumla katika siku zijazo. Bila shaka, ilikuwa wazi kwamba serikali kama hiyo ingefuatilia utekelezaji wa mafundisho ya Kiislamu, lakini kwa kuzingatia hatua za chuki na kiuadui za Marekani na serikali nyingine za Magharibi na machafuko ya ndani; baadhi ya watu na makundi yaliamini kwamba maisha ya Jamhuri ya Kiislamu yangekuwa mafupi kiasi kwamba isingepata fursa ya kutekeleza ahadi hizo. Kwa maana kwamba, Mapinduzi haya yasingedumu muda mrefu. 

 

Wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini, waliunga mkono kikamilifu mapinduzi hayo. Kutokana na hali hiyo, mche huu mchanga sio tu ulinusurika na kuvuka migogoro yote ya utengano na mauaji ya watu na viongozi wengi kutoka kwa kundi la Mojahedin-e- Khalq (MKO), vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, vita vya miaka minane vya Saddam dhidi ya Iran na vitendo vingine vya njama, bali baada ya miaka 45, mche huu umekuwa na umebadilika na kuwa mti mkubwa imara na madhubuti. Tangu mwanzo kabisa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mfumo wa serikali ulioibuka kutoka kwake ulitangaza kutambua maadili na thamani za Uislamu halisi kama lengo lake.

Bila shaka, kufikia lengo hili ni jambo gumu na la hatari katika ulimwengu wa sasa uliojaa dhulma, ufisadi na kupenda mambo ya kimaada. Kwa ajili hiyo, Imam Khomeini na mrithi wake, Ayatullah Khamenei, amesema mara nyingi kwamba: Sisi tuko kwenye njia ya kusimamisha serikali na jamii ya tauhidi na ya Kiislamu, na tuna safari ndefu ya kufikia malengo matukufu ya Kiislamu, na utimilifu kamili wa haya malengo ya Mwenyezi Mungu hauwezekani isipokuwa kwa kuundwa serikali ya kilimwengu ya mwokozi wa wanadamu, mtukufu Imam Mahdi (as).

Kuhusiana na hilo, Imam Khomeini anasema: “Mapinduzi yetu ndiyo kianzio cha mapinduzi makubwa ya Ulimwengu wa Kiislamu chini ya bendera ya Imamu Mahdi." Kwa hakika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kuwa inatayarisha mazingira na kutekeleza sera na mipango yake ndani na nje ya Iran kwa mujibu wa itikadi za Kiislamu na itikadi ya Mahdi. Hata hivyo, serikali za Magharibi zinazingatia maadili ya kiroho ambayo Jamhuri ya Kiislamu inatangaza na kuyapigia debe kama kikwazo na kizingiti dhidi ya njama zao za kueneza kupenda mali, kujinufaisha, ubeberu na ufisadi wa kimaadili, na kwa kadiri iwezekanavyo wanafanya njama za kuzuia kuenea kwa upepo mwanana wa kimaanawi na mielekeo ya Kimungu. 

Imam Khomeini (MA), muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Kuna baadhi ya hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saww) na Ahlul-Baiti (as) ambazo zinaashiria kutokea harakati ya mapinduzi kabla ya mapinduzi ya kilimwengu ya Imam Mahdi (atfs).

Utendaji wa miaka 45 wa Jamhuri ya Kiislamu pia unaonyesha kwamba, unafuata malengo na maadili ambayo yametajwa katika hadithi kuhusu harakati na utawala wa Sahib al-Zaman yaani Imamu wa zama ambaye ni Imamu Mahdi (a.t.f.s). Hatua ya kwanza ya Mwenyezi Mungu ni kupiga vita dhulma na ubeberu na kukabiliana na tawala fisadi na za kivamizi.

Tangu mwanzo kabisa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza upinzani wake dhidi ya dhulma na ubeberu; na kivitendo, imeonyesha kushikamana na kanuni hii muhimu ya Kiislamu. Kiasi kwamba, hii leo akthari ya watu wa mataifa mengine wanajifunza somo la kupinga dhulma na kutafuta uadilifu kutoka kwa taifa la Iran. Kusimamisha uadilifu ni sifa nyingine ya serikali ya Imam Mahdi.

Kufikiwa kwa lengo hili adhimu licha ya kuwa ni jambo gumu na halijafikiwa katika serikali yoyote hadi sasa, lakini juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ni kujaribu kadiri inavyowezekana kusimamisha uadilifu. Akizungumzia ghaiba ya Imam Zaman, Ayatullah Khamenei, kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema:

Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

 

“Ni miaka elfu moja sasa ambapo Umma wa Kiislamu umekuwa ukiomba dua. Mfumo huu wa Kiislamu ambao umeundwa; kazi yake ya kwanza ni kutekeleza uadilifu na usawa. Uadilifu, haki na usawa ni mambo ya faradhi zaidi. Sisi tunataka ustawi pia kwa ajili ya uadilifu na haki. Viongozi na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejaribu kueneza maadili na thamani za imani na itikadi ya Mahdi katika jamii na wameandaa uwanja na mazingira kwa ajili ya kueneza thamani hizi.

Hii leo, upendo na shauku ya wananchi Waislamu kwa mwokozi wa ulimwengu wa mwanadamu na juhudi za kujiandaa kwa ajili ya kusubiri kudhihiri mwokozi huyo zinaweza kuonekana zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Katika upande mwingine, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina moja ya majeshi bora zaidi duniani yenye wapiganaji waaminifu na shujaa na silaha za hali ya juu. Bila shaka, kwa kudhihiri kwa mrekebishaji wa mwisho wa ulimwengu, nguvu hizi na vifaa vitawekwa katika mamlaka yake. 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki maalumu cha kuadhimisha miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umefikia tamati hivyo basi sina budi kukomea hapa kwa leo. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri. Wassalaamu Alaykum warahmatullah Wabarakaatuh

Tags