Apr 14, 2024 11:11 UTC
  • HAMAS: Shambulio la Iran ni haki ya kimaumbile na jibu linalostahiki dhidi ya Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, shambulio lililofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) dhidi ya utawala wa Kizayuni ni jibu la kimaumbile na linalostahiki.

Kwa mujibu wa IRNA, Hamas imetangaza katika taarifa yake kwamba, operesheni ya kijeshi ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni ni haki ya kimaumbile na jibu linalostahiki kwa jinai ya kushambulia sehemu ya ubalozi wa Iran mjini Damascus.

Huku ikisisitizia haki ya kimaumbile ziliyonayo nchi na mataifa ya eneo hili ya kujihami dhidi ya hujuma na uchokozi wa utawala wa Kizayuni, Hamas imeutaka Umma wa Kiarabu na Kiislamu, watetezi wa uhuru duniani na vikosi vya Muqawama kuendeleza uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina. 

Shambulio la makombora ya Iran

Siku 10 baada ya shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel lililolenga sehemu ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, ambao unahesabika kuwa sehemu ya ardhi ya Iran na kupelekea kuuawa shahidi washauri saba wa Iran walioko kisheria nchini Syria na kutochukuliwa msimamo wowote wa wazi na jamii ya kimataifa dhidi ya hatua hiyo haramu ya utawala wa Kizayuni, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu usiku wa kuamkia leo Jumapili limerusha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea maeneo ya utawala wa Kizayuni ili kuutia adabu utawala huo kwa jinai uliyofanya.

Vyombo vya habari vyenye mfungamano na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani vinajaribu kufifilisha ukubwa wa uharibifu na madhara uliyopata utawala ghasibu wa Kizayuni kutokana na mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, lakini picha na mikanda ya video iliyosambazwa inaonyesha kuwa, makombora na droni hizo zimepiga vituo muhimu vya kijeshi vya utawala wa huo wa Kizayuni.../

Tags