Apr 28, 2024 07:20 UTC
  • Wapalestina 37 wauawa shahidi katika mashambulio ya Israel huko Gaza

Wapalestina 37 wameuawa shahidi katika mashambulio ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel katikati na kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni zimeshambulia kwa bomu nyumba moja katika kitongoji cha al-Nasr katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza na kupelekea Wapalestina 10 kuuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa.

Zikiwa zimepita zaidi ya siku 200 tangu kuanza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, wachambuzi kadhaa wa Kizayuni wanatahadharisha kuhusu hali ya hatari ya sasa ya utawala wa Kizayuni na uwezekano wa kushindwa vibaya katika hali yake ya usalama wa ndani.

Wakati huo huo, Israel Kats Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel ametangaza kuwa shambulio la kijeshi dhidi ya Rafah litaahirishwa ikiwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa yatafikiwa.

Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala wa Kizayuni pia amesema, "ikiwa chaguo ni kati ya kusimamisha vita huko Gaza na kufikiwa makubaliano ya mateka, basi tunapaswa kuelekea kwenye makubaliano."

 

Katika hali ambayo zaidi ya Wapalestina milioni moja wamekimbilia Rafah, eneo lililo kusini mwa Gaza, jeshi la Israel limelenga kwa mabomu mara kadhaa eneo hilo kutoka angani, na hofu ya mashambulizi ya ardhini dhidi ya Rafah inazidi kuongezeka.

Kwa muda wa karibu miezi saba sasa, utawala katili wa Israel umekuwa ukidondosha mabomu kila siku katika Ukanda wa Gaza na sasa Umoja wa Mataifa unasema zoezi la kutegua mabomu ambayo hayajalipuka eneo hilo linaweza kuchukua muda miaka 14.

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 34,000 wameuawa shahidi na wengine 77,200 kujeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Tags