Apr 21, 2024 04:09 UTC
  • Jumapili, tarehe 21 Aprili, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 12 Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 21 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1195 iliyopita, Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza alichukua madaraka baada ya vita vya muda mrefu.

Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiongozwa na wafalme wa kiukoo huku ikiwa imegawika katika sehemu kadhaa za kijiografia na kila mtawala akitawala eneo lake maalumu. Egbert aliyekuwa mfalme wa Wessex, eneo lililokuwa Kusini mwa Uingereza ya sasa, baada ya kupambana na watawala wa kitabaka na kuwashinda, mwaka 829 alifanikiwa kuingia madarakani akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi silsila ya utawala wa Wasaxoni wa Magharibi. 

Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza

Siku kama ya leo miaka 415 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai.

Sheikh Bahai ambaye alikuwa mtaalamu wa fiqhi, nujumu na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 952 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Sanamu la Sheikh Bahai

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Allamah Muhammad Iqbal Lahori mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu aliaga dunia huko Bara Hindi.

Alizaliwa mwaka 1873 katika mji wa Sialkot kwenye jimbo la Punjab. Baada ya kumaliza masomo ya awali na ya juu na kupata shahada ya uzamili, Allamah Muhammad Iqbal Lahori alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne. Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya sekondari. Baada ya kurejea India, Iqbal Lahori alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi.

Mwanafalsafa huyo anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi na waasisi wa Pakistan huru.

Iqbal Lahori

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapambano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui.

Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.

 

Tags